ALIYEWAHI kuwa kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amemtaja kocha wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck kuwa ndio chanzo cha matokeo mabaya kwenye michezo miwili iliyopita.
Simba imepoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya awali kufungwa dhidi ya Tanzania Prisons bao 1-0 kisha Ruvu Shooting bao 1-0, ikiwa nafasi ya nne ya msimamo wa ligi ikibaki na pointi zake 13, baada ya kucheza michezo saba.
Sven ambaye alifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi msimu uliopita, alianza vizuri ligi ya msimu huu wa 2020/21, kwa kushinda michezo minne na kutoa sare moja, lakini mambo yameanza kuharibika katika michezo miwili iliyopita huku majeruhi yakitajwa kuwa tatizo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Julio alisema kuwa, Kocha Sven alifanya makosa awali kwa kuwataka waamuzi kuwalinda wachezaji wake mastaa jambo ambalo limewapa kichwa hivyo kusababisha matokeo haya kwa kujiona wao ni bora kuliko wengine.
“Mwalimu alifanya makosa kwa kusema wachezaji wake ni mastaa na waamuzi wawalinde, naamini wachezaji mastaa wanalindwa lakini kwa levo ya mastaa wa Simba bado hawajafikia huko.
“Sasa lile ni tatizo kwa wachezaji, unawapa sifa ambayo hawana wachezaji wanaotakiwa kulindwa kwa Afrika kama vile kina Didier Drogba, Samuel Eto’o na wengineo siyo hawa.
“Unavyosema hivyo unawaweka wachezaji wako kwenye levo kubwa ambayo hatujafikia, hivyo inapelekea wakajiona bora zaidi kuliko wachezaji wengine, hivyo ni vyema wachezaji wakajiangalia na kujitathmini, japo naamini Simba ni timu kubwa ina uwezo mzuri na inaweza kufanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema Julio ambaye ni kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 20.