Home Uncategorized AZAM FC: SIO KIPIGO CHA YANGA TU, TIMU ILIKUWA HAICHEZI MPIRA UNAOELEWEKA

AZAM FC: SIO KIPIGO CHA YANGA TU, TIMU ILIKUWA HAICHEZI MPIRA UNAOELEWEKA

 


UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa haukuwa na sababu ya kuendelea na Kocha Mkuu Aristica Cioaba raia wa Romania kwenye benchi lao la ufundi kwa kuwa alikuwa anawatoa kwenye reli ya kutwaa ubingwa.

Cioaba ambaye ana tuzo ya kocha bora kwa mwezi Septemba na jina lake pia liliingia kwenye fainali ya kumsaka kocha bora wa mwezi Oktoba iliyopo mikononi mwa Cedric Kaze wa Yanga, alifutwa kazi  Novemba 26 kwa kile kilichoelezwa kuwa mwendo mbovu wa timu.

Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa kupoteza kwao mbele ya Yanga kwa kufungwa bao 1-0 Novemba 25 sio sababu ya Cioaba kufutwa kazi bali matokeo mabovu yaliyokuwa yanaitoa timu kwenye reli ni sababu kuu ya kufutwa kwake kazi.

“Unajua wengi wanadhani kwamba Aristica Cioaba amefutwa kazi kwa sababu ya kufungwa na Yanga, hapana haipo hivyo hata kidogo, tuligundua kwamba timu inatoka kwenye reli hasa tukiwa na lengo la kutwaa ubingwa mambo yanakwenda tofauti.

“Kwa timu yenye malengo kila baada ya mechi huwa inafanyika uchunguzi wa mwendo mzima wa mechi na namna matokeo yalivyopatikana ndivyo ambavyo tulikuwa tukifanya kuanzia mechi ya kwanza dhidi ya Polisi Tanzania wakati tukishinda bao 1-0.

“Mambo yalianza kwenda kombo baada ya kupoteza mbele ya Mtibwa Sugar hapo kila kitu kilikuwa kinabadilika, timu inacheza lakini huoni kinachoendelea na zaidi inakuwa inategema mchezaji mmoja sasa hapo hakuna maana ya timu.

“Tumeshinda mbele ya Dodoma Jiji lakini hakukuwa na muunganiko, tukapoteza mbele ya KMC tena mbele ya Yanga tukapoteza, hivyo hatukuwa na chaguo, tumekubaliana pande zote mbili hivyo hatujasitisha mkataba wake kwa sababu ya kufungwa na Yanga bali mechi zote 12 tulikuwa tunafuatilia,” amesema Zakaria.

SOMA NA HII  AZIZ KI ATAMBA YANGA, ABEBA MILIONI 4 KIBOSI