Home Uncategorized BOSI SIMBA AWACHOKONOA KIMTINDO YANGA

BOSI SIMBA AWACHOKONOA KIMTINDO YANGA

 


MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’, ni kama amepiga kijembe kwa watani wao wa jadi, Yanga, hiyo ni baada ya kutamka kuwa wanatamani kupata upinzani kwenye Ligi Kuu Bara, kauli ambayo inamaanisha kuwa wapinzani wao hao wa jadi wasitegemee kuambulia chochote.

 

Kauli hiyo aliitoa kwenye hafla fupi na Wabunge ambao ni mashabiki wa Simba iliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma iliyokwenda sambamba na utambulisho wa jezi mpya watakazozitumia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka huu.

 

Simba hivi sasa wanapata jeuri ya kutamba kutokana na mataji matatu mfululizo ya ligi kuu waliyoyachukua kwa kuanzia msimu wa 2017/18, 2018/19 na 2019/20. Mo alisema kuwa ana malengo makubwa na Simba kati ya hayo ni kuijenga Simba ili iwe klabu endelevu hadi vizazi vijavyo kwa kuhakikisha wanafanya usajili wenye tija kwa timu.

 

 

Bilionea huyo alisema kuwa anafahamu kile wanachokihitaji mashabiki wa Simba na kikubwa ni kuona timu inatandaza ‘Pira Biriani’ huku wakipata matokeo mazuri ya ushindi yatakayowapa pointi tatu muhimu ili wautetee ubingwa wao wa ligi.

 

Aliongeza kuwa hakuna kitakachowazuia kubeba ubingwa wa ligi msimu huu, hiyo ni kutokana na ubora wa kikosi chao ambacho kinaundwa na wachezaji wengi wenye sifa na ubora wa kuichezea Simba.

 

“Imefikia wakati tumekuwa tukitamani kupata upinzani kidogo wa wapinzani wetu kwani tumekuwa tukiongoza hadi inachosha, tunawaomba wapinzani wetu waongeze upinzani ili watupe changamoto.

 

“Nikiwa bado nipo Simba, nimedhamiria kuijenga klabu itakayokuwa endelevu hadi vizazi vijavyo, na hilo linawezekana kwangu, nina malengo makubwa ndani ya Simba. 


“Na tunadhamiria kujenga klabu iliyo endelevu ili tuendeleze kutandaza Pira Biriani na mwisho wa siku tuwe mabingwa wa ligi, kwani ubingwa maana yake ni Simba na Simba maana yake ni ubingwa,” alisema Dewji.

SOMA NA HII  WINGA WA CONGO ATAJA SIKU YA KUTUA YANGA