Home Uncategorized SIMBA YATOA TAMKO ISHU YA CHAMA KUIBUKIA YANGA

SIMBA YATOA TAMKO ISHU YA CHAMA KUIBUKIA YANGA

 


UONGOZI wa Simba umesema kuwa kwa sasa nyota wao Clatous Chama ataendelea kuwa ndani ya kikosi hicho kwa kuwa ni mali yao.


Chama mwenye mabao mawili ndani ya Ligi Kuu Bara na pasi tano kwa msimu wa 2020/21 kati ya mabao 22 yaliyofungwa na Simba anatajwa kuingia kwenye rada za watani wa jadi Yanga.


Kwenye wakati wa usajili wa dirisha kubwa msimu uliopita, Fredrick Mwakalebela ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga alisema kuwa wamefanya mazungumzo na kiungo huyo.


Baadaye alikanusha taarifa hizo baada ya uongozi wa Simba kumjibu na kupeleka malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) kwa kuwa Yanga ilikiuka vigezo vya usajili wa mchezaji kwa mujibu wa Fifa kwa kuzungumza na mchezaji ambaye bado ana mkataba.


Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amesema kuwa Chama ni mali ya timu hiyo na hakuna mpango wa yeye kuibukia timu nyingine kwa sasa.


“Hizo ni habari tu ambazo zinaeleza kwamba Chama anaondoka anakwenda sijui wapi, lakini ukweli ni kwamba mwamba bado yupo ndani ya Simba na suala la kuondoka bado sana.


“Kwa sasa akili zetu tumeziwekeza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kisha mambo hayo mengine yatafuata,” amesema.


Simba inawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo ina kazi ya kusaka ushindi mbele ya Plateu United ya Nigeria.


Mchezo wa kwanza kwa Simba unatarajiwa kuwa nchini Nigeria Uwanja wa Jos kati ya Novemba 27-29 na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa kati ya Desemba 4-6, Uwanja wa Mkapa.  

SOMA NA HII  WAWILI, BABA NA MWANA NDANI YA AC MILAN WAGUNDULIKA NA CORONA