Home Uncategorized IBRAHIM AJIBU WA SIMBA HAYUPO TENA KIKOSINI

IBRAHIM AJIBU WA SIMBA HAYUPO TENA KIKOSINI

 


NAUKUMBUKA utambulisho wa Ibrahim Ajib ulivofanywa kibabe na Simba. Katikati ya umati wa mashabiki waliokuwa uwanja wa taifa kwa sasa unaitwa Uwanja wa Mkapa kushiriki sherehe za Simba day, MC wa shughuli Haji Sunday Manara aliamuru watu wote wanyamaze kwa sababu mtu anayefuata ni wa kipekee sana.

 

 Watu elfu sitini wakanyamaza kimya, wakaacha kupiga vuvuzela zao wakimsubiri Ibrahim Ajib wa Migomba atoke chumbani. Ni mtoto wao wa nyumbani, aliondoka Simba akaenda kung’aa zaidi Yanga.

 

Sasa alikuwa anarejea nyumbani. Utambulisho wake ulifanyika kipekee sana. Hata Meddie Kagere  na Clatous Chama hawakufanyiwa kama yeye.

Alitambulishwa wa mwisho kabisa. Sababu ya kwanza ya Simba kumtambulisha Ajib kwa mbwembwe vile ilikuwa kuwaumiza nafsi watani zao Yanga, kwamba sasa huyu ni wetu. Kipindi hicho Ajib anatua Simba, alikuwa mchezaji muhimu zaidi kwa Yanga.

 

 Yeye pamoja na mkongo Heritier Makambo. Alihusika kutengeneza mabao mengi zaidi kuliko mchezaji yoyote yule wa ligi kuu. Isitoshe alikuwa mchezaji wa timu ya taifa. Hata siku hiyo ya Simba day hakucheza kwasababu alikuwa ametokea Kenya na timu ya taifa.

 Sababu ya pili ya utambulisho wake ni uwezo waliouona Simba ndani ya Ibrahim Ajib. Waliamini anaenda Simba kuendeleza yale makali aliyokuwa nayo Yanga. Lakini haijawa hivyo.

Si tu kwamba Ajib hajapata makali yake ndani ya Simba lakini hata nafasi katika kikosi cha kwanza hajawahi kuipata. Nini kimemkumba?

Kwanza uhaba wa nafasi amekumbana nayo kwasababu ya eneo analocheza. Eneo la kiungo, haswa kiungo wa ushambuliaji ndilo eneo gumu zaidi kupata nafasi ndani ya Simba.

Fikiria labda Simba inacheza na mabeki wanne, viungo wawili wakabaji na washambuliaji wawili. Zinabaki nafasi ngapi za viungo washambuliaji ili watimie wachezaji kumi na moja? Nafasi mbili.

 

Pale Simba kuna viungo wangapi washambuliaji? Tunaweza kuwahesabu. Clatous Chama, Francis Kahata, Luis Miquissone, Hassan Dilunga, Said Ndemla, Rally Bwalya na Bernard Morrison. Tusisahau pia alikuwepo Miraji Athumani kabla hajapata majeraha.

SOMA NA HII  YANGA YAMWAGA MAWAKALA MIA UWANJA WA TAIFA KWA AJILI YA MASHABIKI

 Hapo sasa vaa viatu vya kocha, unamchezesha nani katika hizo nafasi mbili zilizopo? Kichinichini utakuwa umetaja majina mawili bila Ibrahim Ajib.

Ndiyo maana wakati mwingine kocha wa Simba anaamua kuanza na mshambuliaji mmoja ili kupata nafasi ya kiungo mwingine mchezeshaji. Ana wachezaji wengi sana katika hili eneo. Kinachomuumiza zaidi Ajib ni kwamba, wachezaji wengi wa hili eneo ndio mastaa pale Simba. Nani atakuelewa ukiwaweka nje?

Sitaki kushiriki dhambi kwa kusema Ibrahim Ajib ni mvivu sana mazoezini kama wanavyosema watu huku mtaani. Labda wanamsingizia tu. Ninachokumbuka ni kwamba, makocha wote waliowahi kumfundisha Ibrahim Ajib wanasema ana kipaji kikubwa sana ila anatakiwa aongeze juhudi.

 

Hili neno ‘kuongeza juhudi’ ndilo linatafsiriwa kama ‘hana juhudi’. Utamuambia vipi mtu aongezee juhudi wakati tayari anafanya juhudi?

Nimemkumbuka Ibrahim Ajib baada ya kuitazama mechi ya Simba na Polisi Tanzania. Moja ya hoja iliyotolewa katikati ya mijadala ya ile mechi ni kuwa, Simba ilipumzisha wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza. Licha ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kupumzishwa bado Ibrahim Ajib hakupata nafasi.

Hata benchi hakukaa. Kibaya zaidi hakuna aliyemkumbuka. Kwa umri wake wa miaka 24 ni muda anaotakiwa kuwepo uwanjani kama ana ndoto za kufika mbali zaidi ya Simba. Ila kama ameridhika na anaona pesa za Msimbazi zinamtosha. Hakuna shida. Yupo sahihi pia.