Home Uncategorized ISHU YA MORRISON MAMBO NGOMA NZITO, KESI YAANZA UPYA

ISHU YA MORRISON MAMBO NGOMA NZITO, KESI YAANZA UPYA


 UONGOZI wa Yanga umesema kuwa Klabu ya Yanga inaaamini kwamba haki yao ya mchezaji wao wa zamani Bernard Morrison itatendekeka kwa kuwa kesi itasikilizwa baada ya Fifa kuwapa jaji atakayesikiliza kesi hiyo.

Fredrick Mwakalebela, Makamu Mwenyekiti wa Yanga amesema kuwa Fifa imesema kuwa maelezo ambayo aliyatoa mlalamikiwa Morrison baada ya kutakiwa kufanya hivyo hayana mashiko hivyo kesi itaendelea kusikilizwa na haki itatendeka. 

Mwakalebela amesema:-“Tumepewa barua mbili na Fifa baada ya kupeleka malalamiko yetu kuhusu Morrison. Tumepokea barua ambayo inaeleza kuwa tayari tumepata jaji ambaye atasimamia kesi yetu na kila kitu kinakwenda sawa.

“Awali mlalamikiwa ambaye ni Morrison alitakiwa kuandika barua ya kutaja sababu baada ya sisi kumlalamikia Fifa ambapo sababu zake tumeambiwa kwamba hazina mashiko.

“Inatakiwa kulipa fedha kwa pande zote mbili ili kesi isikilizwe na kiasi ambacho kinatakiwa ni fedha za Kifaransa ambazo ni 12,000 jumla 24,000 mlalamikaji na mlalamikiwa anapaswa kulipa.

“Sisi tumedhamiria kulipa fedha hizo ili kesi iweze kusikilizwa na jukumu letu ni kuona kwamba haki inatendeka na kila upande una kazi ya kulipa fedha hizo na ikiwa upande mmoja utashindwa kulipa basi kesi itafutiliwa mbali,” .

Morrison amekuwa kwenye mvutano na mabosi wake wa zamani Yanga ambapo kabla ya kuibukia ndani ya Simba alikuwa akiwatumikia.


Mvutano wake unatokana na ishu ya mkataba ambapo mchezaji amekuwa akisema kwamba mkataba wake ndani ya Yanga ulikuwa ni wa miezi sita huku mabosi wake wakidai kwamba alisaini dili la miaka miwili.

Mpaka anajiunga na Simba kwa kandarasi ya miaka miwili bado alikuwa kwenye mvutano ambapo kesi yake ilisikilizwa kwa muda wa siku tatu mfululizo makao makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).

Maamuzi ambayo yalitolewa awali yaliweka wazi kwamba mkataba wa Morrison na Yanga ulikuwa na mapungufu hivyo mchezaji huyo alipewa ruksa ya kuchagua timu ambayo anahitaji.

SOMA NA HII  WATANZANIA WATWAA KOMBE LA KWANZA MBELE YA UD SONGO YA MSUMBIJI