Home Uncategorized SAKATA LA KICHUYA LAWAPASUA KICHWA NAMUNGO

SAKATA LA KICHUYA LAWAPASUA KICHWA NAMUNGO


 UONGOZI wa Namungo FC umesema kuwa adhabu ya kiungo wao mshambuliaji Shiza Kichuya ambayo ameipata kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa, (FIFA) litawagharimu kwa kuwa wanahitaji huduma ya mchezaji huyo.


Kichuya ambaye ni mali ya Namungo amekutana na rungu kutoka FIFA kwa kufungiwa kutocheza mpaka pale Simba itakapolipa faini ya milioni 300 baada ya kumsajili mchezaji huyo kinyume na utaratibu wa kimkataba.


Habari zinaeleza kuwa FIFA ilituma ujumbe kwa Namungo ikiwataka waache kumtumia mchezaji huyo ambaye alisajiliwa akiwa huru baada ya kumaliza mkataba wake na Simba wa miezi sita aliosajiliwa msimu wa 2019/20.


Taarifa hiyo ilitolewa Desemba 8 ambapo Ofisa Habari wa Namungo FC, Kidamba Namlia amesema kuwa ilikuwa ina maagizo kwa timu ya Namungo pamoja na Simba ambao walikuwa waajiri wake wa zamani.

“Kuhusu masuala ya wachezaji mimi huwa ninasimamia kila kitu na nilipokea barua kwa njia ya email ambayo imetutaka tusimtumie mchezaji Kichuya, (Shiza) mpaka pale ambapo mabosi wake wa zamani watalipa faini.


“Kufungiwa kwa Kichuya kwetu ni pigo kwa kuwa Simba kwa sasa hawana hesabu naye hasa kwa kuwa walimuacha na ni mchezaji huru, sisi tayari alishaingia kwenye mfumo.

“Adhabu hiyo ikiwa haitatekelezwa na Simba basi kuna uwezekano wa mchezaji huyo kufungiwa kucheza ikiwa haitalipwa kwa wakati,” amesema.


Kichuya alisajiliwa na mabosi wake wa zamani Simba ambao walimuuza nchini Misri kutoka Klabu ya Pharco ambayo imedai kuwa alikatisha mkataba ndani ya timu hiyo na kuibukia Simba.


FIFA inaelezwa kuwa imeitaka Simba kulipa faini ya dola za kimarekani 130,000 ambazo ni sawa na milioni 300.


Jana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Namungo FC dhidi ya Biashara United wakati wakitoshana nguvu bila kufunga, Kichuya hakuwa sehemu ya kikosi hicho.

SOMA NA HII  OBREY CHIRWA ATOA NENO LA KISHUJAA AZAM FC