BAADA ya kukamilisha usajili wa beki wa kulia raia wa DR Congo, Djuma Shabani, kisha kupaa kwenda Afrika Kusini, sasa unaambiwa injinia Hers Said anaendelea na usajili wa kimataifa ambapo kituo kinachofuata ni Misri, Sudan na Ethiopia.
Hersi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga na Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM, bado yupo katika harakati za usajili wa wachezaji wa kimataifa kwa ajili ya kukiboresha kikosi cha Yanga kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao.
Yanga ambayo inatarajiwa kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, harakati za kujenga upya kikosi chao imeanza mapema hata kabla ya msimu huu haujamalizika.
Ni rasmi tayari Yanga imempa mkataba wa miaka miwili Djuma Shaban aliyekuwa AS Vita ya DR Congo, baada ya Injinia Hersi hivi karibuni kutua nchini humo na kumaliza dili hilo.
Sasa basi, licha ya Injinia Hersi kuondoka DR Congo baada ya kukamilisha dili la Djuma, unaambiwa kiongozi huyo itabidi arejee tena kwa ajili ya kukamilisha usajili wa mshambuliaji mwingine.
Inaelezwa kwamba, kiongozi huyo atamrejea DR Congo mshambuliaji Obassi Ngatsongo Bersyl anayekipiga AS Otôho d’Oyo ya nchini humo.Kurejea kwake DR Congo itategemea kama atashindwa kumnasa mshambuliaji wa kimataifa wa Ethiopia, Abubeker Naser na Lazarous Kambole wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Chanzo chetu cha uhakika kutoka Yanga, kimeliambia Soka la Bongo kuwa, injinia Hersi ziara zake hizo katika kusaka wachezaji bora ambao watakuja kuitumikia Yanga kwa msimu ujao, anapita DR Congo, Afrika Kusini, Misri, Ethiopia na Sudan.
“Tupo katika harakati za kukiboresha kikosi chetu, hivyo kama ambavyo unaona kiongozi wetu wa masuala ya usajili anazunguka nchi tofauti hapa barani Afrika kwa ajili ya kusajili wachezaji wa kimataifa.
“Baada ya kukamilisha dili la Djuma, siwezi kukutajia moja kwa moja majina ya wachezaji wengine ambao tunataka kuwasajili, hivyo kuweni na subira, muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi.
“Ieleweke wazi kwamba, sio lazima katika kila nchi anayokwenda apate wachezaji maana inawezekana makubaliano yakashindikana, lakini ni uhakika lazima kuna wachezaji atafanikiwa kuwapata huko anapopita.
“Wanayanga wanatakiwa wawe watulivu katika hili, Injinia yupo kazini,” kilisema chanzo hicho.
Soka la Bongo limebaini kwamba, Injinia Hersi akienda Ethiopia, ni kwa ajili ya kukamilisha dili la mshambuliaji Abubeker Nassir Ahmed mwenye umri wa miaka 21 anayekipiga Ethiopian Coffee.
Mshambuliaji huyo msimu huu amefanikiwa kuifungia timu yake mabao 29 katika michezo 36 aliyocheza, huku akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Ethiopia.