Home kimataifa JORGINHO ALIFUNDISHWA SOKA NA MAMA YAKE

JORGINHO ALIFUNDISHWA SOKA NA MAMA YAKE


 KIUNGO Muitalia Jorginho kwa sasa amekuwa gumzo kutokana na mafanikio yake ambayo ameyapata kwenye klabu yake ya Chelsea na timu ya taifa ya Italia.

Kote huko kwa msimu huu ametwaa mataji makubwa, akibeba Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea na ubingwa wa Euro 2020 akiwa na Italia. Mataji hayo mawili makubwa yamemfanya kiungo huyo kutajwa kuwania tuzo ya Ballon d’Or kwa msimu huu.

Lakini watu wengi wasichokijua ni kwamba kiungo huyo ana historia kubwa kabla ya kuwa staa wa soka sasa. Jorginho ambaye ni mzaliwa wa Brazil wakati akiwa mdogo alifundishwa soka na mama yake katika fukwe za nchi hiyo ambayo imetoa wachezaji wakubwa kwenye soka.

Kiungo huyo alikuwa anafundishwa soka na mama yake kwenye fukwe za Imbituba ambazo zipo Kaskazini mwa Brazil ambapo hapo ndipoi msingi mzima wa soka lake la sasa ulianzia.

“Mama yangu alikuwa mchezaji mpira, hivyo nilijifunza vingi kutoka kwake,” Jorginho alifichua hivyo mwaka 2013 na kuongeza.

“Bado anacheza mpira hadi sasa na anajua vingi kuhusu mchezo huo. Alikuwa ananichukua kwenda ufukweni nikiwa na mpira na nilikuwa natumia mchana yote kujifunza mambo ya ufundi mchangani.”

Mazoezi yote hayo ya mama yake Jorginho, Maria Tereza Freitas alikuwa anamuandaa mwanae kwa ajili ya lolote na chochote akiwa uwanjani na akimtaka awe hatua moja mbele ya eneo lake ambalo anacheza.

“Nilimuandaa kukabiliana na matatizo,” anasema mama huyo ambaye alianza kumlea mwanae peke yake akiwa na miaka sita tu baada ya kutengana na mumewe.

Tangu wakati huo mama huyo akachukua nafasi ya kuwa mzazi na mwalimu wa mpira wa mwanae. Alikuwa anatumia muda wake wa mchana kufanya kazi ya usafishaji na fedha kiduchu ambazo anazipata alikuwa anamnunulia viatu vya kuchezea mwanae na muda wa jioni alikuwa akimpeka kucheza mpira kwenye timu ya mtaani ya Bruscão.

Kiungo huyo alilazimika kuondoka kwao na kwenda zaidi ya kilomita 180 kwa ajili ya masuala ya soka, kitu ambacho kinamuumiza sana nyota huyo. Alifanya hivyo akiwa na miaka 13 tu.

Alienda huko akiwa miongoni mwa vijana 50 ambao walichukuliwa na mfanyabiashara raia wa Italia kwa ajili ya kuunda timu ambayo ingekuwa na msaada kwa taifa hilo kwa miaka ya baadaye.

Jorginho akiwa kwenye kambi hiyo anakumbuka walivyokuwa wanaoga kwenye mabafu yenye barafu ndani yake lakin I pia kula chakula ambacho hakikumpendeza na ambacho kilikuwa kinabadilika mara chache sana.

SOMA NA HII  MANCHESTER UNITED HOFU TUPU

Baada ya kukaa hapo kwa miaka miwili akapata ofa ya kujiunga na Verona, ambayo ilikuwa daraja la pili Italia.

Mkataba wa Jorginho klabuni hapo ulikuwa wenye maslahi makubwa lakini alishuhudia wakala wake akichukua £27,000 (milioni 73,962,400) huku yeye akiambulia £18 (4,930,830).

“Nilikuwa siwezi kufanya kitu,” anasema. “Nilikuwa natumia euro tano kiwango kidogo kwa ajili ya kununua vifaa vya usafi na kilichobaki nilikuwa natumia kwa ajili ya kuwapigia familia yangu kuzungumza nao.

“Ilikuwa hivyo kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu,”

“Lakini mwaka wa pili ambapo nilipokutana na kipa raia wa Brazil, Rafael Pinheiro, ambaye alikuwa kama kaka kwangu nilimwambia stori yangu na hakuamini.

“Tangu hapo hakuwahi kuniacha nikose kitu chochote.”

Akiwa ndani ya kikosi hicho cha Verona, Jorginho alipewa jina la utani la ‘Mbwa mwitu wa baadaye’.

Mtendaji mkuu wa zamani wa Hellas Verona, Riccardo Prisciantelli, akimzungumzia Jorginho anasema: “Kila mtu alikuwa anakubali juu ya uwezo wake ambapo alikuwa anaitwa simba, ila kwangu alikuwa mbwa mwitu. Alikuwa anafanya mazoezi mara tatu zaidi uwanjani zaidi ya mtu mwingine.

“Nilinunua vifaa na kutengeneza gym ndogo ambayo alikuwa anakuja mapema na kuchelewa kuondoka hadi pale tutakapomtaka aondoke.”

Akiwa Verona, Jorginho aliwahi kutolewa kwa mkopo kwenye timu ya Daraja D Italia ya Sambonifacese, ambapo aliwasha moto kabla ya kurudishwa tena kikosini na alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na miaka 18 Septemba 2011.

Lakini anakumbukwa kutokana na kuwepo kwenye kikosi cha timu hiyo ambayo ilishuka daraja mwaka 2013 kabla ya kuipandisha na hapo ndipo akapata nafasi ya kuelekea Napoli miezi sita baadaye alipokutana na kocha Maurizio Sarri ambaye amekifanya kiwango cha kiungo huyo kuwa cha hali ya juu.

Aliijua zaidi Chelsea wakati akiwa hapo kutokana na uwepo wa kiungo Nathaniel Chalobah, ambaye alikuwa akicheza Napoli kwa mkopo mwaka 2015.

Baada ya miaka mitatu akatua Chelsea ambapo alienda kukutana na bosi wake Maurizio Sarri ambaye yeye alikuwa ameshatungulia kujiunga na timu hiyo yenye maskani yake London.

“Jorginho sio mchezaji wa mwili, ni mchezaji wa kiufundi,” anasema Sarri na kuongeza

“Ubora wake mkubwa ni kutokana na kufikiria kwa haraka sana.”

Kiungo huyo kwa sasa anafaidika na mshahara mkubwa anaolipwa na Chelsea lakini kamwe hawezi kusahau darasa ambalo alikuwa anapewa na mama yake katika fukwe za Imbituba.