Home Yanga SC MAKAMBO, DJUMA NA MAYELE WAVUNJA REKODI YANGA…MZEE MPILI AKIIBUKA KWA STAILI MPYA

MAKAMBO, DJUMA NA MAYELE WAVUNJA REKODI YANGA…MZEE MPILI AKIIBUKA KWA STAILI MPYA


MASTAA watatu wa Klabu ya Yanga wamefunika katika mauzo ya jezi mpya za aina tatu tofauti zilizozinduliwa juzi Dar es Salaam chini ya mbwembwe za Msemaji mpya, Haji Manara.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari, Hassan Bumbuli Yanga ina mastaa kibao lakini jezi za Fiston Mayele, Heritier Makambo na Shabaan Djuma zinauliziwa zaidi kila duka.

Alisema jezi zao hazina majina ya wachezaji lakini ikitokea mteja akahitaji kutengenezewa wanafanya hivyo na mpaka jana majina yaliyokuwa yakiuliziwa na kununulika zaidi ni hayo matatu kwa Dar es Salaam na baadhi ya mikoa ya jirani.

“Pale klabuni kuna duka letu na jana tu walionunua jezi walihitaji majina hayo matatu zaidi na wametengenezewa hivyo mtu akija akihitaji ya mchezaji fulani anapata tu lakini sisi tunauza ambazo hazina majina,” alisema.

Aidha Bumbuli alisema, kwa haraka haraka bado hawajajua wala kufahamu ni jezi ngapi zimeuzwa toka juzi walipozindua kutokana na jografia lakini punde watajua.

“Kujua zimeuzwa ngapi kwa sasa ni ngumu kwani zimesambazwa maeneo mbalimbali sasa jana, hii leo kufahamu ni ngumu ila kama wiki hivi ndio unaweza kufahamu,” alisisitiza Bumbuli.

Sikia matawi ya Yanga

Matawi ya Yanga Dar es Salaam yamempokea kwa furaha kubwa aliyekuwa Msemaji wa Simba Haji Manara huku wakiamini atawasaidia kuipaisha zaidi timu yao kama alivyokuwa akifanya upande wa pili.

Katibu Mkuu wa Matawi ya Yanga, Kais Edwine alisema; “Wanayanga wote nawaomba tuwe bega kwa bega na Haji kwa kuwa viongozi wetu makini wameona ana kitu na ndio sababu iliyowafanya kumpa ajira, Haji ana kitu fulani hivi ambacho alikifanya Simba hivyo tunaamini atakileta kwetu kwani hakuna mwanasoka ambaye hajui tambo za Haji, tunajua na tunatambua kuna kitu kwake kitaisaidia timu yetu,”alisema Kais.

MPILI NA MANARA

Katika hatua nyingine, Manara ametamba Jijini Dar es Salaam kuwa siku ya Mwananchi Jumapili hii itakuwa ya aina yake na haijapata kutokea kwenye historia ya Yanga na soka la Tanzania.

SOMA NA HII  NAMBA 6 WA YANGA, BEKI AFUNGUKA BALAA LAKE

Alisisitiza kwamba ameandaa staili ya aina yake na anaamini mashabiki watajaa kuona ubora wa wachezaji wao pamoja na mkongwe wa muziki, Koffi Olomide atakayetumbuiza.

Mzee Mpili naye tangu juzi amekuwa karibu na viongozi wa Yanga akihakikisha kila kitu kinakwenda sawa kuelekea Jumapili kwenye shoo yao.

Mzee huyo hajaonekana hadharani kwa kipindi kirefu tangu Yanga ilipofungwa bao 1-0 na Simba kwenye fainali ya FA mjini Kigoma.

Nandy, G-Nako nao ndani

Mambo yakiwa hivyo, Kilele cha Siku ya Mwananchi kumenoga zaidi baada ya wasanii kadhaa nyota nchini nao kujumuisha kumsindikiza Koffi Olomide kwenye tamasha hilo litakalofanyika Jumapili ndani ya Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Baadhi ya wakali hao watakaopambana tamasha hilo litakaloanza mapema asubuhi kwa shughuli na burudani mbalimbali ni Nandy, BillNass, Mhe. Temba, Chegge, G-Nako, Mzee wa Bwax, Kiherehere wa Yanga, Baba Levo na wengine ili kuthibitisha kuwa, kweli Yanga kuna watu.

Kilele kitaahimishwa na utambulisho wa kikosi kipya cha msimu sambamba na pambano la kirafiki la kimataifa liotakaloikutanisha Yanga dhidi ya miamba ya soka ya Zambia, Zanaco FC.