Home news HITIMANA AZIDI KUFICHUA YA SIMBA…AFUNGUKA KUHUSU MASLAHI YAKE..AMKANA GOMES..AMTAJA PABLO…

HITIMANA AZIDI KUFICHUA YA SIMBA…AFUNGUKA KUHUSU MASLAHI YAKE..AMKANA GOMES..AMTAJA PABLO…


ACHANA na kuondoka kwa makocha watano wa kigeni, habari zilizoshtua wengi ni uamuzi wa aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Thiery Hitimana kufikia makubaliano na mabaosi wake kuvunja mkataba.

Kuondoka kwa kocha huyo raia wa Burundi kunafikisha idadi ya makocha sita wa kigeni waliotimka kwenye timu zao ikiwa ni rekodi na historia kwenye ligi ikiwa haijafika hata nusu.

Kocha huyo anakuwa wa pili ndani ya kikosi cha Simba baada ya aliyekuwapo awali, Didier Gomes naye kuamua kufikia makubaliano ya vigogo hao kuachana nao.

Mbali na makocha hao waliokuwa Simba, wengine ni Ettiene Ndayiragije (Geita Gold), Harerimana Haruna (Mbeya Kwanza), Joseph Omog (Mtibwa Sugar), Salum Mayanga (Prisons) na Patrick Okumu aliyekuwa Biashara United.

Katika mahojiano yake na gazeti la Mwanaspoti Thiery ambaye alikuwa ametua Msimbazi hivi karibuni baada ya kukaimu nafasi ya kocha mkuu kwa muda kabla ya kuletewa bosi wake Mhispania Pablo Franco, ambaye ameelezea sababu za kufikia uamuzi huo.

Ikumbukwe kocha huyo asiye na maneno mengi, anajivunia rekodi na heshima aliyoweka hapa nchini kwa kuipandisha Namungo FC kwenye Ligi Kuu, lakini pia akizifundisha Biashara United na Mtibwa Sugar.

KILICHOMNG’OA

Anasema hawezi kuelezea kwa undani sana sababu zilizomfanya kufikia uamuzi wa kukubaliana na mabosi wake kuvunja mkataba kwani waliridhiana pande zote.

Hata hivyo, anasema kati ya mambo yaliyomfanya kung’atuka ni ishu ya maslahi ambayo viongozi waliahidi lakini hayakutekelezwa.

Anasema hata hivyo anashukuru kuona wanamalizana kwa amani bila kuwepo mgogoro wowote kwa maslahi ya klabu na kwamba hawezi kulaumu chochote kwa muda aliohudumu pale Msimbazi.

“Yapo baadhi ya mambo tuliyokuwa tumekubaliana lakini hadi sasa ilikuwa bado hayajatekelezwa, ila nashukuru tumeridhiana na kuachana salama,” anasema Thiery.

ALICHOJIFUNZA SIMBA

Anasema kwa muda aliohudumu Simba, yapo mengi aliyojifunza kutoka kwa makocha wenzake, viongozi na hata wachezaji kwani timu hiyo ni kubwa.

Anasema tofauti na timu nyingine alizofundisha hapa nchini, ameona kuna tofauti kwani Simba imepiga hatua ikiwa na miundombinu kama uwanja wa mazoezi, na pia wachezaji wa kigeni wenye uwezo tofauti.

Anasema mazingira ya timu hiyo ni tofauti na kwingine alikopitia kwani Msimbazi kuna ofa nyingi ambazo kila mmoja anaweza kufanyakazi vizuri.

“Kwanza mazingira yake ni mazuri kikazi, wanaku-ofa vitu vingi, wana uwanja, wachezaji wengi wa kimataifa wenye majina na uwezo mkubwa hivyo lazima kama kocha ujifunze,” anasema Thiery.

ANAVYOIONA SIMBA

Anasema pamoja na Simba kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado upo uwezekano wa kufanya vizuri Kombe la Shirikisho Afrika ambako tayari wametinga hatua ya makundi na ipo Kundi D pamoja na timu ya RS Berkane ya Morocco anayocheza Clatous Chama na Tuisila Kisinda, Asec Mimosas ya Ivory Coast na US Gendarmerie ya Niger.

Anasema Simba wanaweza kufanya vizuri kama watajipanga na kufanyia kazi mapendekezo ya kocha mkuu hasa kipindi hiki cha dirisha dogo.

Anashauri kuwa kwa namna alivyoiacha Simba, ameona upungufu eneo la ushambuliaji kwani wachezaji wengi eneo hilo wamekumbwa sana na majeraha, jambo linaloipa ugumu kwenye matokeo.

“Utakumbuka hata baadhi ya mechi za mwanzoni tulikuwa tukikosa mabao, wachezaji wengi walikumbwa na majeraha, hivyo kama watafanyia kazi upungufu huo watafika mbali,” anasema.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA ASEC MIMOSAS....MASTAA NA MSHABIKI SIMBA WAPEWA UJUMBE HUU MZITO...

Anaongeza kuwa hata suala la ratiba ngumu kwa timu hiyo inaweza kuwapa wakati mgumu kama hawatapanua kikosi, kwani wana mashindano mengi, ikiwa ni Kombe la Mapinduzi, Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Afrika.

PABLO KUMKATAA

Kocha huyo Mnyarwanda anasema hawezi kuthibitisha moja kwa moja, lakini amekiri kuwa alisikia tetesi kwamba kocha Pablo alikuwa hamtaki yeye aendelee kuwapo Simba.

Anasema suala hilo linaweza kuwa na ukweli au vinginevyo, lakini hakuwa na mawazo au macho ya kutazama upande wa pili badala yake alikuwa akiwasiliana na mabosi wake.

Hitimana anasema kwa muda aliokuwa benchi la Simba upo utofauti kati ya Pablo na Gomes kwani kila mmoja alikuwa na falsafa yake kama kocha mkuu.

Anaeleza kuwa kipindi cha Gomes makombe yalionekana hivyo kwa sasa wamsubiri Pablo kama naye ataweza kufanya kama vile au kuzidi kwani yeye ndiye mwenye uamuzi.

“Hizo tetesi za Pablo kutaka kuvunja benchi lote nilizisikia, japokuwa sikuambiwa, sijui kama alizungumza na viongozi au lah, ila mimi nilikuwa nafanya kazi zangu kwenye eneo langu.

“Utofauti upo kwa sababu kila mmoja ana falsafa yake, wakati wa Gomes yapo makombe tuliyaona, kwa sasa ni wakati wa Pablo tumsubiri naye tuone atakachofanya,” anasema kocha huyo.

JE ALIJIANDAA KUONDOKA?

Anakiri wazi kuwa alijiandaa na alitarajia kuondoka na ndio maana muda ulipofika aliwasiliana na mabosi wake na kufikia uamuzi.

Anasema baada ya kuondoka Gomes aliona dalili za wazi za kuondoka hadi anafanya uamuzi wa kuwafuata viongozi kuzungumza nao kuachana salama.

“Niliona hizo dalili na nilijiandaa kuondoka, ndio maana nilifikia uamuzi wa kuwafuata viongozi tukazungumza na kuelewana hadi kuachana,” anasema kocha huyo.

NI KWELI GOMES ALIMPENDEKEZA SIMBA?

Anakiri kuwa Gomes alipendekeza jina lake Simba na viongozi waliwasiliana naye na kumuomba awasilishe wasifu (CV) ambapo walivutiwa naye kwa kuwa na vigezo vyote.

Anasema hakufahamu mapema kwani mawasiliano mengi alikuwa akiyafanya na viongozi hadi kukamilisha utaratibu wa kuungana na timu.

“Hilo sijui, ila inawezekana yeye ndiye alinipendekeza na uongozi ukanitafuta na kuomba CV yangu na waliikubali kwa sababu ilikuwa bora ukilinganisha na makocha wengine,” anasema Hitimana.

USHIRIKIANO WAKE NA PABLO

Kocha huyo anasema ushirikiano ulikuwepo japo siyo kihivyo, kwani kawaida kocha msaidizi yeye ni kushauri ila uamuzi huwa ni kocha mkuu.

Anasema wao walikuwa wakipendekeza baadhi ya mambo, lakini uamuzi ulikuwa kwa Pablo na hawakumuingilia zaidi pale alipoamua chochote.

“Kazi yetu wasaidizi ni kushauri au kupendekeza, ila yeye ndiye aliamua cha kufanya kulingana na mawazo yake, kwahiyo ilikuwa hivyo na maisha yanaenda,” anasema Thiery.

Anafafanua kuwa hata tukio la Pablo na Pascal Wawa yeye hakuhusika kama wadau wanavyodai, akibainisha kuwa hata mabadiliko hakuyaelewa vizuri hadi kuzua ile sintofahamu.

“Wengi wanazungumzia lile sakata, lakini sikuhusika kwa chochote, japokuwa nilijua atafanya mabadiliko lakini hiyo ya Wawa sikujua kitu hadi kocha analalamika na kurusha chupa na kupiga teke viti,” anasema.

Hitimana pia alisema hayuko tayari kuzungumzia uvumi wa kuingiliwa majukumu wakati akikaimu nafasi ya kocha mkuu wa Simba akisisitiza hatazungumzia mambo yaliyopita.