Home news KUELEKEA MECHI YA LEO…SIMBA WAPENYEZEWA MBINU YA KUICHAPA MTIBWA MANUNGU…CHAMA ATAJWA..

KUELEKEA MECHI YA LEO…SIMBA WAPENYEZEWA MBINU YA KUICHAPA MTIBWA MANUNGU…CHAMA ATAJWA..


WAKATI mashabiki wa Yanga wanawacheka Simba baada ya kuchapwa na Mbeya City bao 1-0, wataalamu wa soka wametabiri na kuonyesha njia ambazo wanaweza kuzitumia kupindua meza.

Makocha na wachambuzi wanasema Simba kufungwa na Mbeya City haimanishi imechoka bali walikutana na timu inayocheza kaunta, ambapo walikuwa wanashambulia kwa machale na kujilinda zaidi.

Kwa mujibu wao, jambo waliloliona kwa aina ya uchezaji wa Simba inayotumia pasi fupifupi isingekuwa rahisi kupenyeza kwa Mbeya City ambao walikuwa na lengo la kujilinda zaidi. Makocha na wachambuzi hao, walitaja kikosi cha Simba ambacho ni hatari zaidi, huku wakiihofia Mtibwa Sugar kunyeshewa mvua ya mabao mengi.

Katika majina yaliyotajwa kiungo Clatous Chama ambaye ni ingizo jipya dirisha dogo ametajwa mara nyingi, wakiamini kuwa uzoefu wake na ligi ya Tanzania unaweza ukawa chachu ya mafanikio kwenye mchezo huo.

Makocha waliokitaja kikosi kipya kinachoweza kuibeba Simba ni Mathias Lule (Mbeya City), Francis Baraza (Kagera Sugar) na Meja mstaafu wa Jeshi, Abdul Mingange (African Lyon), wakati wachambuzi ni George Ambangile na Dk Liki Abdallah.

Kikosi walichokitaja ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Henock Inonga, Joash Onyango, Clatous Chama, Kibu Denis, Ousmane Sakho, Sadio Kanoute, Jonas Mkude na Meddie Kagere.

Kocha wa Mbeya City, Lule alisema kuwa wachezaji kama Clatous Chama, Pape Ousmane Sakho, Sadio Kanoute na Kibu Denis wanapaswa kuaminiwa na kuendelea kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara na kocha Pablo Franco.

“Sina shaka na eneo la ulinzi licha ya kuwa wachezaji waliopo wamecheza kwa muda mrefu, naamini wakifanyia kazi hususani ushambuliaji naona watakuwa bora maana wamekuwa wakipitia wakati mgumu licha ya washambuliaji wao kufanya vizuri msimu uliopita,” alisema Lule.

Naye Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Baraza alisema kuwa ujio wa kiungo Clatous Chama utaiongezea timu hiyo makali yake kutokana na uhodari alionao nyota huyo kwenye kufunga na kutengeneza nafasi kwa washambuliaji wengine kikosini.

“Maingizo yote ambayo yamepata nafasi ya kucheza mara kwa mara yameonyesha uwezo ni suala la kocha kutuliza akili zake vizuri kwenye machaguo ya kikosi hususani eneo la ushambuliaji ambapo ningependekeza aanze na Meddie Kagere badala ya John Bocco na Chris Mugalu.”

SOMA NA HII  HAJI MANARA AKWEA PIPA NA BOSI WAKE

Naye Kocha wa African Lyon, Mingange alisema kuwa Simba inaonekana inacheza kwa kupaniki hasa baada ya kuwaona wapinzani wao Yanga wanacheza vizuri ingawa hakusita kuwataja Pape Sakho, Clatous Chama, Kibu Denis na Peter Banda kama watu muhimu sana.

“Nimewaangalia kwenye Ligi Kuu Bara na hata Kombe la Mapinduzi, wana timu zuri ambayo wakitulia na kuacha kucheza kwa presha za timu nyingine wataendelea kuwa bora licha ya wachezaji wao wengi hasa eneo la ulinzi kutumika kwa muda mrefu,” alisema Mingange.

Liki yeye alisema kocha hahitaji kuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi hasa kwenye safu ya ulinzi ambayo inahitaji wachezaji waliocheza pamoja muda mrefu duniani kote ni sehemu za kiungo na ushambuliaji ndio zinafanyiwa mabadiliko mara kwa mara.

Naye Ambangile alitilia mkazo kwenye mabadiliko ya kikosi kwa kumtaja Chama kuwa ana imani naye kama atapewa nafasi anaweza kuongeza kitu huku akitaja kuwa hawezi kufahamu sababu za kocha kutokumpanga huenda hayupo fiti lakini akipewa nafasi anaweza kuonyesha kitu kutokana na uzoefu wake.

Mbeya City iliwachukua miezi sita kuifunga Simba na kuiharibia rekodi yao kwenye Ligi Kuu Bara kwani mara ya mwisho Wekundu wa Msimbazi kufungwa ilikuwa ni Julai 3, 2021 wakati walipofungwa bao 1-0 na watani zao Yanga, bao lililowekwa kimiani na kiungo Zawadi Mauya.

Baada ya kupoteza mechi iliyopita, Simba itakuwa na kibarua kingine ugenini leo Jumamosi, itakapopambana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turian Morogoro ambao walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Ruvu Shooting kwenye mchezo uliopita.