Home Simba SC PABLO – HAKUNA WAKUTUZUIA …TUTAWAFUNGA TENA KWAO…

PABLO – HAKUNA WAKUTUZUIA …TUTAWAFUNGA TENA KWAO…

 


BAADA ya kuanza vizuri mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika Kundi D kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco Martin, amefunguka kuwa kwa namna mipango yao ilivyo, hakuna wa kuwazuia kufikia malengo.

Pablo aliongeza kuwa, ASEC Mimosas licha ya kutajwa kuwa ni timu ngumu, lakini watakwenda kuwafunga tena nyumbani kwao katika mechi ya marudiano.

Kocha huyo raia wa Hispania, alibainisha kwamba, awali wakati anakwenda kucheza nao, alikuwa hajapata nafasi nzuri ya kufahamu udhaifu na ubora wao, hivyo kwa sasa ameshapata kitu baada ya kuwachakaza nyumbani.

Akizungumza baada ya juzi Jumapili Simba kushinda 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, Pablo alisema anachohitaji kwa sasa ni kupata alama tatu kwenye kila mchezo iwe nyumbani au ugenini.

“Nimewaona vizuri ASEC wanavyocheza, kuna uwezekano wa kushinda tena tukiwa kwao. Sikuwa nawafahamu vizuri uchezaji wao, ila nimewaona na kujua nguvu na ubora wao.

“Tutafanyia kazi mapungufu yetu ili kujiboresha zaidi na kuwaadhibu kwenye yale mapungufu tuliyoyaona kwao. Muhimu ni kupata alama tatu kwenye kila mchezo na huo ndiyo mpango wetu,” alisema.

Katika Kundi D, Simba wanashika nafasi ya pili nyuma ya RS Berkane ya Morocco, huku zote zikiwa na alama tatu kutokana na kushinda mechi za kwanza. Wanatofautishwa na mabao ya kufunga na kufungwa.

Wakati Simba ikishinda 3-1 dhidi ya ASEC Mimosas, RS Berkane wenyewe waliikandamiza US Gendarmerie ya Niger mabao 5-3.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUMALIZA MATIBABU YAKE....DILUNGA APASUA UKWELI WA KUENDELEA KUBAKI AFRIKA KUSINI...