Home Habari za michezo BAJETI YA SERIKALI 2022/2023….VIWANJA VITANO KUWEKWA NYASI BANDIA KWA MPIGO…MBEYA WAKUMBUKWA…

BAJETI YA SERIKALI 2022/2023….VIWANJA VITANO KUWEKWA NYASI BANDIA KWA MPIGO…MBEYA WAKUMBUKWA…


Serikali imesema itaweka nyasi bandia kwenye viwanja vitano katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Tanga, Dodoma na Mbeya ili kukuza michezo.

Hayo yalisemwa Bungeni Dodoma jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2022/2023.

“Nitumie nafasi hii kuwahakikishia Watanzania kuwa tutaweka nyasi bandia kwenye viwanja vitano kukuza michezo hapa nchini,”alisema na kuongeza kuwa, msamaha wa kodi kwenye nyasi bandia na vifaa ambata utakwenda mpaka ngazi ya halmashauri.

Pia, alisema serikali itarejesha bahati nasibu ya taifa kwa utaratibu wa kutumia sekta binafsi.

“Sambamba na hilo, serikali kupitia Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, TRA na sekta binafsi itaanza kuendesha bahati nasibu kwa kupitia risiti za EFD ili kuchochea wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa,” alisema.

Dk Mwigulu alizipongeza timu za soka za taifa ikiwamo timu ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls) na timu ya taifa ya wenye ulemavu (Tembo Warriors) zilizofuzu michuano ya Kombe la Dunia na kuitakia kila la kheri Taifa Stars ambayo iko kwenye kampeni za kufuzu michuano ya Afrika, Afcon. Katika hatua nyingine,

Dk Mwigulu alisema serikali inapendekeza kuanzisha tozo ya asilimia 1.5 kwenye vifaa vinavyotumika kuzalisha, kusambaza, kudurufu na kutunza kazi za sanaa, uandishi na ubunifu mwingine kama vile muziki, filamu, vitabu, picha na aina nyingine za kazi za ubunifu.

Vifaa hivyo ni redio/ televisheni zinazowezesha kurekodi, kinasa sauti na kinasa picha.

Mbali na hayo, Dk Nchemba aliipongeza timu za Yanga na Simba kwa mwenendo wao mzuri mwaka huu kwenye ligi na michuano ya kimataifa.

Alitania: “Namwomba radhi bosi wangu Waziri Mkuu (Kasim Majaliwa) kwa kitendo alichowafanyia mwanangu Fei toto kule Mwanza.

Mniwie radhi, nilipompeleka Fei toto (Feisal Salum wa Yanga) sikujua atakuja kuwafanyia kitu mbaya hivi, mpaka nasikia anatafutwa maliasili eti kaua mnyama bila kibali.”

Pia, aliwapongeza Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kuisaidia Yanga ikiwa katika mapito, wadhamini wa klabu hiyo GSM kwa kurejesha furaha ya Wananchi (Yanga) hasa kwa usajili wa Fiston Mayele. “Mayele amekuwa maarufu kuliko makatibu wenezi wa baadhi ya vyama vya siasa.

SOMA NA HII  ILI KUEPUKANA NA 'FIGISU FIGISU' ZA YANGA....WASAUZI WAAMUA 'KUUCHUNA'...'WASUSA' KILA KITU BONGO...

Nawapongeza sana na marafiki zangu klabu ya Simba kwa kuwakilisha vyema kwenye mashindano ya kimataifa, wananijua mara zote kimataifa tuko pamoja, siwezi kukana bendera ya taifa langu kwa ajili ya utani wa jadi,” alisema.