Home Habari za michezo GOLI LA KIBRAZILI LAITAKATISHA SINGIDA BIG STARS MBELE YA TZ PRISONS…AMISI TAMBWE...

GOLI LA KIBRAZILI LAITAKATISHA SINGIDA BIG STARS MBELE YA TZ PRISONS…AMISI TAMBWE ‘MIBICHWA’ ATIKISA…


Kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Singida Big Stars ugenini kwenye Uwanja wa CCM Liti, Singida leo, kimefanya mkosi wa Tanzania Prisons kutopata ushindi katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kufikisha siku 1817.

Bao la dakika ya 36 la Peterson Cruz aliyefunga kwa staili ya Tik Tak akimalizia pasi ya kichwa ya Amissi Tambwe lilitosha kuifanya Singida Big Stars kuanza vyema msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2022/2023 lakini kwa Maafande wa Tanzania Prisons lilikuwa ni muendelezo wa historia isiyofurahisha ya kutopata ushindi katika mechi ya kwanza ya ligi kwa muda mrefu.

Matokeo hayo yameifanya Tanzania Prisons kucheza misimu mitano mfululizo ya Ligi Kuu bila kupata ushindi katika mechi ya kwanza ya ligi.

Mara ya mwisho kwa Tanzania Prisons kupata ushindi katika mechi ya kwanza ya ligi ilikuwa ni Agosti 26, 2017 ilipoichapa Lipuli ya Iringa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Samora mjini Iringa,

Baada ya hapo, Tanzania Prisons haikupata ushindi tena katika mechi za mwanzo za msimu ikicheza michezo mitano ambayo miwili walitoka sare huku mingine mitatu wakipoteza.

Baada ya msimu ambao Prisons waliifunga Lipuli katika mechi ya kwanza, msimu uliofuata walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba na katika msimu wa 2019/2020 walianza kwa kutoka sare tasa na Mbeya City.

Katika msimu wa 2020/2021 walianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga na msimu wa 2021/2022 walijikuta wakipoteza mbele ya Mbeya City kwa bao 1-0 na mechi nyingine ni leo ambayo wamepoteza mbele ya Singida Big Stars.

SOMA NA HII  SLOT YA PLANET 67 INAKUPA UHAKIKA WA MKWANJA NDANI YA MERIDIANBET CASINO....