Home Habari za michezo KUEPUSHA AIBU KESHO….MGUNDA AHAIDI ‘KUNG’ATA MENO’ DHIDI YA WAMALAWI…TSHABALALA ATAJA ‘UCHAWI’….

KUEPUSHA AIBU KESHO….MGUNDA AHAIDI ‘KUNG’ATA MENO’ DHIDI YA WAMALAWI…TSHABALALA ATAJA ‘UCHAWI’….


KOCHA mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema bado hawajamaliza kazi licha ya kushinda 2-0 dhidi ya Nyasa Big Bullets katika mchezo wao wa kwanza.

Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Big Bullets nchini Malawi katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kesho saa 10:00 jioni watacheza mchezo wa marudiano katika uwanja wa Mkapa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mgunda amesema matokea ambayo waliyapata Malawi yalikuwa ni kipindi cha kwanza, kipindi cha pili kitakuwa katika uwanja wa Mkapa.

“Kule Malawi ilikuwa ni kipindi cha kwanza kwahiyo bado tuna tuna kipindi cha pili hapa nyumbani kuhakikisha tunaendelea pale tulipoishia, tunalijua lililotokea na wachezaji wapo tayari kupambana na kwa uwezo wa Mungu tutafanikiwa.” amesema Mgunda.

Akizungumzia upande wa kuepuka yaliyotokea msimu uliopita baada ya Simba kutolewa katika raundi ya pili ya Ligi hiyo dhidi ya Jwaneng Galaxy (Botswana) licha ya kushinda 2-0 ugenini, Mgunda amesema hilo ni historia na yeye hakuwepo.

“Mimi sikuwepo ila niliambiwa kuhusu historia hiyo na makosa ambayo yalifanyika nimeambiwa licha ya Simba kushinda ugenini wakaja kupoteza hapa, mimi kwangu ushindi ni hadi filimbi ya mwisho.” amesema Mgunda.

Wakati huo huo nahodha wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ amesema mechi hiyo ni muhimu kwao kuhakikisha wanaenda hatua nyingine.

“Mechi haijaisha bado, sisi tuna malengo yetu kama klabu na kuyafikia ni lazima kwanza tushinde mchezo wetu huu,”amesema Tshabalala na kuongeza;

“Mashabiki wetu wamekuwa wakituunga mkono, sisi tutaipambania timu kwa ajili yao, viongozi na sisi wenyewe kwa sababu mpira ni kazi yetu.”

Msimu huu Simba inatakiwa kuhakikisha inapambana na kuingia kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa kisha ipambane kutinga hatua ya nusu fainali baada ya kucheza robo fainali msimu wa 2018-2019 na 2020-2021.

Simba inaingia kwenye mchezo huo huku ikiwa imetoka kushinda 1-0 dhidi ya Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu, mechi ambayo wachezaji wake walipambana mpaka dakika ya mwisho.

SOMA NA HII  SIRI HII YAVUJA...KUMBE DUBE NDIO SABABU...AZAM KUFUNGWA NA SIMBA