BAADA ya kupangwa na wanaotetea taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi za robo fainali, kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amesema ; ‘Hawa mbona freshi tu’.
Mechi ya kwanza itachezwa Dar es SalaamAprili 21-22, kabla kurudiana wiki moja baadae, lakini Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mara ya mwisho dhidi ya Wydad ndani ya dakika sita za mwisho.
Ikitinga nusu fainali itakutana na mshindi kati ya Mamelodi Sundowns ya Sauzi au CR Boulizdad ya Algeria.
Mashabiki kupitia mitandao ya kijamii wameonekana kupata ganzi kutokana na rekodi za timu za Morocco na wakikumbuka kipigo cha mabao 3-0 ilichopewa na wapinzani wao hao mwaka 2011, lakini kocha Robertinho amewatuliza na kuwaambia wamejipanga.
Kocha Robertinho aliliambia SOKA LA BONGO kuwa, kwa hatua hii waliyofikia hakuna timu nyepesi hivyo alitarajia kukutana na yoyote ili kuonyesha ukubwa wao na kwamba hata hao Wydad anaona ni sawa na watajipanga ili kuthibitisha kuwa hata Simba ni timu kubwa barani Afrika.
“Hakuna namna zaidi ya kupambana na aliyekuwa bora, tunakwenda kwenye hatua ngumu, hivyo tunahitaji kujiandaa vyema ila natambua hata wao pia wanahofia ubora wetu vilevile,”alisema na kuongeza kuwa ni ngumu kuwa bingwa bila kuwapiga mabingwa wenzio.