Home kimataifa FRANK LAMPARD AKUPAMBANA NA TALAKA…ILIYOJAA MACHOZI JASHO NA DAMU

FRANK LAMPARD AKUPAMBANA NA TALAKA…ILIYOJAA MACHOZI JASHO NA DAMU

FRANK LAMPARD AKUPAMBANA NA TALAKA...ILIYOJAA MACHOZI JASHO NA DAMU

Miongoni mwa maswali magumu yaliyowahi kuulizwa. Nani alimuua Rais wa Marekani JF Kennedy? Kwanini? Kisa kilikuwa nini? Kusudio lilikuwa nini? Dunia kila siku inakutana na maswali magumu. Katika mpira pia huwa tunakubaliana na maswali magumu.

Kwa mfano, nani alimchagua Frank Lampard kuwa kocha tena wa Chelsea? Kwanini? Kusudio lake lilikuwa nini? Na kwanini Lampard alikubali kurudi tena? Kwanini hasa?. Dunia haijawahi kuacha kuwa na maswali magumu.

Lampard alikuwa kocha wa Chelsea. Nadhani alitaka kutimiza ndoto zake. Na nadhani hata mashabiki walitaka kutimiza ndoto zao. kwamba mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea Chelsea amekuwa kocha wao na amepata mafanikio makubwa kama kocha kama ilivyokuwa akiwa mchezaji.

Lampard ndiye mfungaji bora wa muda wote Chelsea. Mmoja kati ya wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Chelsea.

Mmoja kati ya wachezaji wenye mafanikio zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Chelsea.

Labda walitaka itokee kama Barcelona na Pep Guardiola. Au labda walitaka itokee kama Johan Cruyff na Barcelona. Hata hivyo haikuwezekana.

Chelsea ilifungwa ovyo chini ya Lampard kiasi kwamba tajiri wa wakati huo, Roman Abramovich akaamua kumuondoa.

Kumbuka kwamba Lampard na Roman walikuwa marafiki. Mambo yalifika shingoni na hata mashabiki walinyoosha mikono. Ilikuwa picha ya kusikitisha kumuona mmoja kati ya wapendwa wao wakuu akifukuzwa katika timu. Zilikuwa nyakati ambazo mume alikuwa anaandika talaka huku analia.

Baadaye Lampard akaenda zake Everton. Ilionekana kwamba ingeweza kuwa timu ya saizi yake. aliikuta inapambana kutoshuka daraja. Akafanikiwa katika dakika za mwisho. Alipouanza msimu upya hakuwa na jipya. Timu ikabaki maeneo ya chini kabisa. Hakuonekana kama ana mbinu mpya.

Alifukuzwa kazi. Hakukuwa na huzuni kubwa kutoka kwa mashabiki wa Everton kwa sababu Lampard sio mwenzao.

Labda kama siku moja nafasi hiyo angepewa Mikel Arteta au Wayne Rooney halafu wakafukuzwa basi wangeweza kuhuzunika. Hawa ni wenzao. Lampard hakuwa mwenzao.

Kuanzia hapo Lampard alikuwa mtaani tu na mkewe Christina wakilea watoto. Ghafla Chelsea ikapata tajiri mpya Mmarekani, Todd Boehly. Ghafla kocha wa kwanza, Thomas Tuchel akafukuzwa. Ghafla kocha wa pili, Graham Potter akafukuzwa.

Ghafla tajiri mpya wa Chelsea akamrudisha kibaruani Lampard kuwa kocha wa muda. Rudia maswali yangu ya juu. Nani alimrudisha Lampard katika kiti hiki ambacho alikishindwa? Mbaya zaidi akenda zake Everton ambako kiti alikishindwa.

Walau kama angefanya vema Everton kiasi cha kuipeleka hadi nafasi ya tano tungesema kwamba amegundua makosa yake na sasa anaibuka upya kuwa kocha bora kama tulivyodhania awali wakati anaanza kazi. Lakini hapa alikuwa anarudishwa kibaruani kocha ambaye alionekana hafai Chelsea, kisha akaonekana hafai Everton.

Na sasa Chelsea imefungwa mechi tano mfululizo chini ya Lampard. Frank anawahuzunisha watu waliompenda na kumuweka moyoni kama mchezaji.

Anawahuzunisha kwa mara ya pili. hawawezi kubeba mabango yanayoonyesha ‘Lampard OUT’ kwa sababu ni mwenzao lakini kwa mara nyingine tena amezusha manung’uniko kutoka kwa watu waliompenda na kumuhusudu.

Jambo la kwanza ni Uingereza uliotawala. Kinachotokea Chelsea ni kibaya lakini Lampard ni Muingereza mwenzao. Hausikii sana kelele kwa sababu ni Muingereza mwenzao. Ndivyo walivyo. Haya yanayotokea ingekuwa yanamtokea Tuchel au Patrick Vieira wangepiga kelele nyingi.

Hapo hapo la pili ni hili hapa ambalo tunawaachia Chelsea wenyewe waamue. Ni kweli kwamba Frank hatakuwa kocha wa kudumu pale Chelsea na muda wowote, Mauricio Pochettino atateuliwa kuwa kocha mpya wa Stamford Brigde. Lakini kumbuka kwamba hata Tottenham wamemfukuza kocha wa muda.

Baada ya kufukuzwa kwa Antonio Conte, Spurs walimchagua Cristian Stellini kuwa kocha wa muda. Akafanya vibaya katika mechi nne tu na akafukuzwa. Nadhani pia kwa sababu ni Muitaliano. Vipi kuhusu Lampard ambaye ameshafungwa mechi tano mfululizo? Naona anayoyoma tu.

Kuna aibu kwao kumuondoa Lampard kama kocha wa muda. Hivi ndivyo Waingereza walivyo. Lakini vyovyote ilivyo Waingereza wanaumia na hiki ambacho kinamtokea Lampard kwa sababu mbalimbali.

Kwanza waliamini kwamba huenda Lampard angefuata nyayo za makocha wapya wa kizazi kipya wanaong’ara katik nchi zao kama makocha wa Hispania. Labda kama vile Pep Guardiola au Mikel Arteta. Sio kwa Lampard tu lakini hata kwa Steven Gerrard. Waliamini kwamba wawili hawa wangeingia katika kundi la makocha hodari wa kizazi kipya.

Ilikuwa ndoto pia kama nilivyosema kuona Lampard akiiongoza Chelsea kwa mafanikio kama kocha. Na ilikuwa ndoto pia kuona Gerrard akiiongoza Liverpool kwa mafanikio kama kocha. Lakini Aston Villa tu imemshinda, sembuse Liverpool? Na sasa walau Gerrard ana nafasi ya kurekebisha kwingine lakini Lampard inaonekana kama vile shughuli imemshinda jumla.

Kuna wasiwasi kwamba ameendelea kujikusanyia wasifu wa ovyo kama kocha na mwishowe anaweza asirudi katika timu kubwa.

Katika hili tunarudi katika swali. Kwanini hakukataa kuichukua nafasi hii? pesa anayo. Anajua jukumu ambalo lilikuwa linamkabili? Alikwenda kuchukua nafasi ya Potter ambaye binafsi naamini licha ya kwamba Chelsea ilimshinda lakini yeye ni kocha bora kuliko Lampard.

Kwanini hasa alichukua nafasi hii? inashangaza kidogo. Angeweza kukaa nje na kupumzika zaidi na zaidi huku akichungulia timu ambayo haina presha. Lakini sasa hata yeye mwenyewe anapata fadhaa kwa sababu anajua kwamba anawaangusha washkaji zake.

Anajua kwamba anawaangusha mashabiki wa Chelsea. Ni vile tu wanamuonea aibu. Hata kama ni ukocha wa muda lakini haikuwa kazi nzuri kwake kuichukua. Hata kama hatafukuzwa kipindi hiki lakini katika kazi hii ya ukocha mashabiki wa Chelsea watakuwa wamempa talaka ya kudumu. Haitatokea akarudi tena kuwa kocha mkuu klabuni hapo.

SOMA NA HII  ISHU YA OUATTARA NA SIMBA YAZIDI KUPASUA KICHWA...BOSI AFUNGUKA NAMNA JAMBO LILIVYO NDANI KWA NDANI...