Home Habari za michezo GAMONDI ATAMBA KUHUSU KIKOSI CHAKE AAHIDI MAKUBWA

GAMONDI ATAMBA KUHUSU KIKOSI CHAKE AAHIDI MAKUBWA

Habari za Yanga

Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Gamondi amewataka mashabiki wa klabu hiyo kutarajia mabadiliko zaidi ya uchezaji kwa timu yake tofauti na walivyoishuhudia kwenye mchezo wao wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Kaizer Chiefs katika Tamasha la Kilele cha Siku ya Mwananchi Jumamosi (Julai 22).

Gamondi amesema anahitaji marekebisho madogo kwenye timu yake na anaamini timu hiyo itaendeleza makali yake kwenye ligi na mashindano ya kimataifa.

“Mashabiki wa Young Africans wataendelea kufurahi, naamini kikosi hiki kitafanya vizuri kwenye mashindano yote, yapo marekebisho kidogo nitayafanya mazoezini na timu itakapoonekana kwa mara nyingine mashabiki wataona mabadiliko, nina wachezaji wenye uwezo mkubwa sana,” amesema Gamondi

Amesema siku zilizobaki kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu kuanza hapo Agosti 15, mwaka huu, atazitumia vizuri kuweka kile anachokitaka ndani ya timu hiyo na kuwataka mashabiki kujiandaa kupata furaha.

Alipoulizwa ni mapungufu gani aliyoyaona ndani ya timu hiyo, Gamondi hakutaka kuweka wazi lakini alisisitiza lazima wachezaji wake watengeneze nafasi nyingi za kufunga na wazitumie ipasavyo.

“Siwezi kusema, lakini kama kocha nina ramani yangu kichwani ya namna timu ninavyotaka icheze, ni lazima tutumie vizuri kila nafasi tunayoitengeneza, kwa sasa bado timu haijakaa vizuri kwa namna ninavyotaka,” amesema Gamondi.

Aidha, amesema ameguswa na uwezo wa wachezaji wake na ana uhakika watampa matokeo mazuri kwenye mashindano watakayoshiriki.

Kikosi hicho cha Young Africans kinaendelea na maandalizi yake kwenye kambi waliyoiweka Avic Town Kigamboni kujiandaa na michezo ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu kwa ujumla wake.

Kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Young Africans itafungua pazia dhidi ya Azam FC Agosti 9, huku Simba wakicheza na Singida Fountain Gate FC Agosti 13 mwaka huu.

SOMA NA HII  SIMBA YATOA TIKETI ZA KITIONGA...TANZANIA YAPANDA VIWANGO...YANGA YAAMBULIA POINTI 1