Home Habari za michezo KWA SIMBA HII, TATIZO NI MZAMIRU, ISHU IKO HIVI

KWA SIMBA HII, TATIZO NI MZAMIRU, ISHU IKO HIVI

Simba imeanza kusaka taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar. Lakini kwa tathmini ya haraka shida ni pale kati kwa Mzamiru Yassin. Kwa namna yoyoye ile staa huyo mzawa ndiyo suluhisho la dharura la kurejesha amani miongoni mwa mashabiki wa Simba ambayo bado wanaonekana hawaridhishwi na ubora wa kikosi chao uwanjani.

Wamefikia hatua ya kudiriki kuupiga presha uongozi ufikirie mara mbili kuhusu benchi la ufundi. Lakini shida ni Mzamiru. Mtanielewa tu. Twendeni pamoja mstari kwa mstari. Badae nitapokea maoni yenu kwenye simu yangu hapo chini.

Shida ni Mzamiru. Suluhisho la dharura la furaha ya Simba ni Robertinho sasa kuchagua, kumwanzisha Mzamiru na Ngoma ama na Kanoute, lakini ni lazima Mzamiru kuwapo uwanjani kama anataka safu yake ya ulinzi kuwa salama.

Kumbuka Simba ilitwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga penalti 3-1 wikiendi iliyopita jijini Tanga. Kabla ya Yanga, walicheza na Singida Fountain Gate na kuamuliwa kwa penalti kwa Simba kushinda 4-2.

Lakini katika michezo hiyo mitatu ya kimashindano (dhidi ya Singida Fountain Gate, Yanga na Mtibwa), kikosi hicho kinachonolewa na kocha Reberto Oliveira ‘Robertinho’ kimepata wakati ugumu kiuchezaji na kufanya mashabiki waangalie mechi kwa wasiwasi tofauti na matarajio yao wakati vyuma vinadondoshwa kwenye App.

Simba mpya bado haijaonyesha matumaini kuwa inaweza kucheza vizuri kama ilivyoaminika. Haitembezi boli kama ilivyokuwa msimu uliopita na imekuwa ikihenyeka kwani hata katika mechi dhidi ya Singida, mchezo ulionekana kuwa upande wa wapinzani wao kuliko Simba, jambo ambalo lilitokea pia dhidi ya Yanga, ambao ulionyesha zaidi upungufu wa Mnyama. Jambo ambalo linaibua hofu kwa mashabiki itakuwaje kwenye Ligi ya Mabingwa na Super Cup?

Katika mechi hizo za ndani, Simba ilitumia wengi wapya, Willy Onana, Luis Miquissone, Che Fondoh Malone na Fabrice Ngoma, huku Aubin Kramo akikosa nafasi hadi sasa kikosini.

Lakini pale kati kwa Ngoma, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin pana shida. Dhidi ya Singida, kocha Robertinho aliwatumia Mzamiru na Kanoute, ambao licha ya kushambuliwa mara kadhaa waliilinda safu yao ya ulinzi.

Ingawa Robertinho alimtoa Kanoute, ambaye anaonekana kutokuwa bora msimu huu na nafasi yake kuchukuliwa na Ngoma, ambaye alimalizia vizuri licha ya kutokuwa na kasi.

Katika mchezo dhidi ya Yanga ndiy ikawa balaa zaidi. Licha ya Mzamiru na Kanoute kuanza, bado hali ilikuwa mbaya eneo la katikati muda wote wa mchezo, hata Kanoute alipompisha Ngoma katikati ya kipindi cha pili.

Robertinho aliona huenda shida ikawa kwa kumtumia Mzamiru katika michezo hiyo miwili na kukosa ubora kuanzia katikati, akaamua kuwatumia Ngoma na Kanoute kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa.

Kocha huyo alipata mabao mawili ya haraka kabla ya lile la tatu ndani ya dakika 45, lakini alijikuta akikumbushwa na kiwango kuwa Mzamiru si mchezaji wa kukaa benchi kwenye kikosi cha Simba.

Licha ya mabao matatu ya dakika 45, Simba iliruhusu mawili ya haraka yaliyopishana dakika mbili, ambayo yote yalimwonyesha ni jinsi gani safu ya ulinzi ilikosa udhibiti mbele ya Ngoma na Kanoute.

Bao la kwanza la Mtibwa , lilitokana na beki Che Malone kutaka kupiga chenga baada ya kushindwa kuona kiungo yeyote kati ya Ngoma na Kanoute karibu yake, jambo lililosababisha matatizo na Matteo Antony mwenye zali la kuitungua Simba kutupia kambani dakika ya 20.

Bao la pili lililofungwa dakika ya 22, lilitokana na mpira mrefu, ambao ulianguka nyuma ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, ambaye licha ya kumfukuza mfungaji Matteo, alishindwa kuwa na msaada wa haraka kutoka katikati.

Ni wazi kuwa katika mechi hizo tatu, Simba haiwezi kuwa bora eneo la kati bila Mzamiru, ambaye kwa uwepo wake uwanjani, Simba imecheza dakika 225 bila kuruhusu bao, lakini dakika 45 bila mzaliwa huyo wa Morogoro.

Mzamiru amekosa dakika 45 za kwanza kwenye Uwanja wa Manungu Complex, ambazo Simba iliruhusu mabao mawili, jambo ambalo Robertinho alilithibitisha kwa vitendo kuwa alikosea kumwacha nje nyota huyo wa zamani wa Mtibwa.

Kuingia kwake kulibadilisha vingi katika eneo la katikati, ambalo lilikuwa chini ya Mtibwa kwa vipindi vingi uwanjani, huku pia akiongeza kitu katika kuulinda mstari wa safu ya ulinzi.

Suluhisho la dharura la furaha ya Simba ni Robertinho sasa kuchagua, kumwanzisha Mzamiru na Ngoma ama na Kanoute, lakini ni lazima Mzamiru kuwapo uwanjani, vinginevyo inaweza kuwa majanga kwake na timu kwa ujumla.

WASIKIE WADAU

Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema Mzamiru ni mchezaji bora zaidi kuliko Ngoma na Kanoute na ana mchango mkubwa kwenye timu kutokana na uchezaji wake.

“Mzamiru ana nguvu, anapambana sana katikati ya uwanja, pia ni mfia timu kwa maana huwa yupo tayari aumie ili timu ipate inachokitaka, hivyo huwezi kumlinganisha na viungo wengine wa timu hiyo.

“Kitu ambacho watu wengi wanasahau, Mzamiru tangu ametua Simba amekuwa akipata nafasi ya kucheza mara zote kwa makocha wote waliopita pale,” alisema Julio na kuongeza;

“Wamekuja viungo wengi eneo la Mzamiru lakini hawajamtoa kwenye reli na makocha wengi wanampenda kwakuwa anafuata maelekezo na kutimiza majukumu yake kwa ufasaha, usiangalie Simba tu hali ipo hivyo hata akiwa Taifa Stars. Watu waache kusifia wageni tu, bali na hawa wazawa wanaofanya vizuri wapewe heshima yao.”

Kocha wa mzawa, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema; “Namuamini sana Mzamiru, na bado ataendelea kuwa tegemeo kwa Simba katika eneo la kiungo.

“Kocha yeyote anapenda kumtumia mchezaji anayefanya vyema mazoezini na hadi sasa sifa hiyo Mzamiru anayo ndio maana anapata nafasi,” alisema Mwaisabula.

SOMA NA HII  CHANONGO AWAONYA MASTAA WENZIE KWENYE ISHU HII