Home Habari za michezo GAMONDI APEWA WAKATI MGUMU NA MWAMNYETO

GAMONDI APEWA WAKATI MGUMU NA MWAMNYETO

Habari za Yanga

Kikosi cha Yanga, kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, huku kambi ya timu hiyo ikinoga baada ya nahodha Bakari Mwamnyeto kuongeza mzuka mazoezini baada ya kukosekana kwenye mbili mfululizo zilizopita.

Beki wa kati huyo alikuwa na matatizo ya kifamilia na kuikosa safari ya Yanga kwenda kucheza na Al Merrikh jijini Kigali, Rwanda timu hiyo ikishinda mabao 2-0, pia kulikosa pambano la Ligi Kuu wakati Yanga ikiilaza Namungo kwa bao 1-0, huku kocha Miguel Gamondi akiwatumia Ibrahim Bacca na nahodha msaidizi, Dickson Job kwenye mechi zote mbili.

Hata hivyo, tayari beki huyo ameungana na wenzake na kocha Gamondi amekiri kurejea kwake kunampasua kichwa kutokana na eneo analocheza kuwa na wachezaji waliokamilika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Gamondi alisema urejeo wa Mwamnyeto unamfanya awe na kazi kupanga timu kwenye eneo hilo, kwa vile hakuwa mgonjwa alikuwa nje kwa matatizo hivyo amerudi na kuanza mzoezi akiwa fiti.

“Mwamnyeto yupo fiti na anaendelea na mazoezi na wenzake kurudi kwake kunanipa shida ya kuamua nani aanze na nani akae benchi kutokana na ubora wa wachezaji wangu wote wanaocheza eneo hilo,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Hivyo muda ndio utaamua nani ataamka vizuri kuelekea mchezo wetu ujao ambao nina mpango wa kubadili mfumo wa uchezaji kutokana na kubaini kuwa wapinzani wetu wanafahamu aina yetu ya uchezaji.”

Alisema anafurahi kuona ushindani wa wachezaji wake, huku akikiri wote wana uwezo sawa ndio maana amekuwa akiwiwa na ugumu wa kupanga kikosi na kuweka wazi kila mmoja atapata nafasi ya kucheza kulingana na namna anavyomshawishi kwenye mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo husika.

ISHU IPO KUSHOTO

Kutokana na beki Joyce Lomalisa kuwa majeruhi na kuwa na uwezekano wa kulikosa pambano la marudiano la raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh, kunamfanya kocha Gamondi kutokuwa na presha kwani ana majembe wanaoweza kucheza kwa ufasaha upande huo.

Lomalisa aliumia kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopita dhidi ya Namungo baada ya kuchezewa vibaya na Hashim Manyanya na kumfanya kuomba kutolewa mara baada ya kipindi cha pili kuanza na inaelezwa huenda akawa nje kati ya siku 5-7, lakini kocha Gamondi alisema;

“Lomalisa hakuchezewa mchezo wa kiungwana, alipata shida na kushindwa kuendelea na mchezo daktari kasema anahitaji mapumziko kwa muda hili halina shida kwenye kikosi changu. Kuna Nickson Kibabage na Kibwana Shomari wote wana uwezo mkubwa wa naamini mmoja wao ataanza pale.”

SOMA NA HII  FT: YANGA 2-1 SIMBA...MAYELE AWAFANYIA UNYAMA SIMBA...MORRISON ,MOLOKO WATIBUA TIBUA...SAKHO KIDOOGOOO...