NYOTA wa Azam FC, Sospeter Bajana yupo kwenye wakati mgumu ndani ya kikosi hicho baada ya kukwaruzana na kocha wake, Yousouph Dabo.
Bajana ambaye alitarajiwa kuwa nahodha msimu huu baada ya kustaafu kwa Aggrey Morris amejikuta akiipoteza nafasi hiyo sambamba na ile ya kucheza katika kikosi cha kwanza.
Kwa sasa Dabo amemchagua raia wa Ghana, Daniel Amoah kuwa nahodha akisaidiwa na Lusajo Mwaikenda pamoja na Idris Mbombo.
Mabadiliko hayo yalianzia kwenye mchezo dhidi ya Singida Big Stars ambapo Amoah alianza kwa kuvaa kitambaa na Bajana akaanzia nje.
Lakini hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Amoah kuvaa kitambaa cha unahodha pindi nahodha mkuu anapokuwa hayumo uwanjani, ila mara zote huwa anakivua na kumkabidhi nahodha mkuu kama ataingia baadaye.
Lakini kwenye mchezo huo Amoah hakumpa kitambaa Bajana alipoingia kuchukua nafasi ya Yahya Zaydi.
Hii ndiyo ilikuwa ishara kamili kwamba Bajana siyo tena nahodha wa Azam FC. Wakati wa kambi ya maandalizi ya msimu kule Tunisia, Dabo alimpa kitambaa cha unahodha Mbombo kwenye mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Al Hilal jijini Tunis, katika mechi ambayo Bajana alianza kwenye kikosi cha kwanza.
Lakini baada ya mchezo huo Bajana akawa anavaa kitambaa cha unahodha kama kawaida katika mechi zote ambazo alikuwa akicheza hadi ilipokuja hii ya Singida Big Stars.
Bajana na Dabo kugombana kwao kunafikirisha sana kwani kocha huyo raia wa Senegal ndiye aliyeshinikiza Bajana aongezewe mkataba.
Awali uongozi wa Azam FC haututaka kumuongezea mkataba mchezaji huyo kutokana masharti aliyoweka.
Bajana alitaka mkataba wa miaka mitatu kwa thamani Sh100 milioni kila mwaka (Sh300 milioni kwa jumla) na mshahara wa Sh5 milioni.
Uongozi ulitaka kumpa mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh70 milioni kwa mwaka (Sh140 milioni kwa ujumla) na mshahara kama alioutaka.
Yeye hakutaka kupunguza hata shilingi na wao hawakutaka kuongeza hata shilingi.
Ndipo Dabo alipoomba kikao na mabosi wa Azam FC kuwaambia kwamba Bajana yupo kwenye mipango yake na anaomba abakishwe kwa gharama yoyote. Mabosi hawakuwa na namna zaidi ya kumsikiliza kocha, wakampa Bajana alichotaka.
Lakini ghafla mambo yamebadilika. Wawili hawa hawaivi kabisa. Haijulikani sababu ya moja kwa moja, lakini kuna vitu vingi vinatajwa kuwa sababu ya kugombana kwao.
1. KUVUJA KWA SIRI KAMBINI
Inasemekana Dabo alipoteza imani na Bajana baada ya meneja wa mchezaji huyo kudaiwa kutoa siri za ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mchezo wa marudiano wa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bahir Dar ya Ethiopia.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, meneja huyo alisema mambo mengi sana ya ndani kabisa ya Azam FC kuhusu uhusiano wa kocha huyo na wachezaji wake.
Dabo anaamini kwamba ni Bajana ndiye aliyetoa siri hiyo hivyo hafai kuwemo kwenye timu.
Kwenye moja ya vipindi vya mazoezi baada ya sakata la kitambaa cha unahodha, Dabo alimsema Bajana mbele ya wenzake kwamba anaweza akamtoa wakati wowote kwenye timu. Lakini sababu haikuwa meneja wake bali kutojituma kwake kwenye mazoezi.
Dabo alimlaumu Bajana kwamba anatembea muda mwingi mazoezini badala ya kukimbia.
2. UTHUBUTU WA BAJANA
Inasemekana Dabo amekuwa akikwaruzana na wachezaji mara kadhaa mazoezini. Na ikitokea hivyo, wachezaji hao hutolewa nje ya uwanja na mechi inayokuja hawapati nafasi kama sehemu ya adhabu.
Lakini siku moja kabla ya mchezo dhidi ya Singida Big Stars, Dabo aligombana na Gibril Sillah kiasi cha kushikana mashati.
Sillah alikuwa na mpira na alitakiwa atoe pasi kwa mtu aliyekuwa karibu naye, lakini hakutoa pasi. Akataka kukokota na kupiga chenga, akanyang’anywa mpira.
Dabo akasimamisha mazoezi ili atoe maelekezo kwa Sillah…akakasirika na kuupiga mpira nje.
Dabo akamtoa Sillah nje ya uwanja na kisha akamfuata huko huko kuendeleza ugomvi.
Wakashikana mashati na ikabidi wachezaji wengine waache mazoezi kwenda kuwaamulia.
Baada ya mazoezi, ugomvi ukaendelea tena huku wakitukanana.
Lakini siku iliyofuata kwenye mchezo dhidi ya Singida Big Stars, Sillah alikuwa sehemu ya kikosi na aliingia kipindi cha pili.
Kitendo cha Sillah kupangwa kwenye mechi hiyo kilimkera Bajana na akamfuata kocha baada ya mechi palepale uwanjani na kuzungumza naye.
Akamwambia kwamba anavyofanya siyo sawa na anaigawa timu. Sillah hakupaswa kupangwa kwenye mchezo wa leo kutokana na alichokifanya jana.
“Wachezaji wengine huwa unawaadhibu kwa makosa madogo tu ya kuupiga mpira nje mazoezini na huwapangi mechi zijazo.
“Lakini Sillah amekuonyesha dharau kubwa kwa kuupiga mpira nje, kukutukana na kutaka kupigana na wewe…na bado unampanga. Wale wengine watajisikiaje?”
Hii ilimkera sana Dabo na kuongeza hasira zake kwa Bajana.
3. HAYUPO KWENYE MIPANGO TENA
Japo awali alisema Bajana yupo kwenye mipango yake, lakini baada ya mechi ya Bahir Dar kule Addis Ababa Ethiopia, Bajana hayupo tena kwenye mipango ya Dabo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani kabisa, Dabo anamuona Bajana kama mchezaji ambaye hawezi kuendana na mifumo yake hivyo anamtafutia sababu ya kumuondoa kikosini.
Dabo anamuona Bajana kama mchezaji wa kawaida anayepewa sifa zisizostahili na kumfanya ajione mkubwa.
Ukiacha sababu hizo za kiufundi, Dabo anataka kumuondoa Bajana ili usitokee mpasuko hasa kwa wachezaji wa ndani ambao ni watiifu kwa nahodha wao.
Anaamini kwamba endapo Bajana atabaki ndani ya kikosi, anaweza kumyumbisha na kumsababishia wakati mgumu. Hata hivyo, hayo yote ni ya kudhania, ukweli halisi haijulikani japo kilichopo wazi ni kwamba Bajana siyo tena nahodha wa Azam FC, nahodha ni Daniel Amoah.
Dabo hamtumii Bajana siku hizi na badala yake amemchagua Yahya Zaydi.
Lakini yawezekana Bajana akarudi kutokana kuumia kwa Yahya ambaye atakaa nje kwa wiki tatu.
Lakini pia yupo Yannick Bangala ambaye bado hajaanza kupata nafasi.
Yawezekana naye akapata nafasi mechi yao ijayo dhidi ya Dodoma Jiji kwa sababu James Akaminko naye atakosekana kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.
Kadi mbili alizipata kwenye Ngao ya Jamii na moja kwenye mechi dhdi ya Singida Fountain Gate ‘Big Stars’. Lakini baada ya hapo, yawezekana Bajana asirudi tena kikosini na chochote kinaweza kutokea kwenye dirisha lijalo, tukianza na dirisha dogo la Januari.
SOMA NA HII KOMBE JIPYA LIGI KUU HILI HAPA....KUHUSU KUKABIDHIWA KWA YANGA AU LAH..UKWELI HUU HAPA..