Home Habari za michezo INONGA MAYELE NDANI YA JAHAZI MOJA CONGO

INONGA MAYELE NDANI YA JAHAZI MOJA CONGO

Habari za Simba na Yanga

Licha ya kuendelea kuuguza majeraha aliyoyapata katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, Septemba 21 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, beki Enock Inonga ameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo.

Kikosi hicho cha DR Congo kinajiandaa na mechi mbili za kimataifa za kirafiki dhidi ya New Zealand na Angola zitakazochezwa baadaye mwezi huu.

Kocha Sebastien Desabre amemjumuisha Inonga katika kikosi chake cha wachezaji 26 ambacho kinaundwa na kundi kubwa la nyota wanaocheza soka la kulipwa nje ya Afrika.

Nahodha Chancel Mbemba anayechezea Marseille ya Ufaransa, Cedrick Bakambu wa Galatasaray ya Uturuki na Arthur Masuaku wa Besiktas ni miongoni mwa majina makubwa yaliyoitwa na kocha Desabre.

Nyota wa zamani wa Yanga anayeitumikia Pyramids FC ya Misri, Fiston Mayele, ameendelea kujumuishwa na benchi la ufundi la DR Congo ambalo pia limeendelea kuwaamini makipa watatu, Mpasi Lionel, Siadi Biaggio na Dimitri Berthaud ambao liliwaita katika mechi mbili zilizopita za timu hiyo dhidi ya Sudan na Afrika Kusini.

Katika hali ya kushangaza, kocha Desabre amemuweka kando nyota wa Brentford ya England, Yoane Wissa kama alivyofanya kwa Jordan Ikoko anayechezea Pafos ya Cyprus.

Kikosi hicho cha DR Congo kilichotangazwa na Desabre kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki kinaundwa na makipa Mpasi, Berthaud na Baggio wakati mabeki ni Brian Bayeye, Gedeon Kalulu, Dylan Batubinska, Enock Inonga, Chancel Mbemba, Arthur Masuaku, Rocky Bushiri na Joris Kayembe.

Eneo la kiungo, kocha Desabre ana wigo mpana wa uteuzi wa wachezaji kutokana na uwepo wa Aaron Tshibola, Edo Kayembe, Samuel Moutousammy, Elia Meschack, Joel Kakuta, William Balikwisha, Theo Bongonda, Charles Pickel na Grady Diangana.

Washambuliaji walioitwa ni Mayele, Bakambu, Jackson Muleka, Ben Malango, Silas Katompa na Simon Banza.

SOMA NA HII  WALIOIVURUGA REKODI YA YANGA WAPO SANA