Home Habari za michezo KUELEKEA DABI YA KARIAKOO MASTAA HAWA SIMBA SASA NI MTEGO

KUELEKEA DABI YA KARIAKOO MASTAA HAWA SIMBA SASA NI MTEGO

Habari za Simba

Simba ipo kambini ikijifua na mechi ijayo ya Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga lakini mastaa wawili wa Mnyama, washambuliaji Moses Phiri na Luis Miquissone wameonekana kuwa mtego nje ndani.

Presha ya ndani ya Simba inakuja baada ya baadhi ya mashabiki wa soka nchini kuhoji kwanini Phiri na Luis hawapati muda mwingi wa kucheza ndani ya kikosi hicho ilihali wana viwango vikubwa na rekodi nzuri.

Jambo hilo ni kama linatoa presha kubwa kwa benchi la ufundi la Simba chini ya Kocha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ambaye amekuwa akiwapa nafasi mara chache katika nyakati tofati.

Aidha wawili hao wamekuwa wakitoa presha nje ya Simba kwani wamekuwa na madhara ya moja kwa moja kwa timu pinzani pale wanapoingia mchezoni.

Phiri hadi sasa anashika rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza dakika chache na kufunga mabao mengi (matatu), kwenye Ligi Kuu msimu huu, akiwa amecheza jumla ya dakika 143 ambazo nyingi ametokea benchi.

Pia Luis ameshikilia rekodi hiyo kwa upande wa pasi za mwisho ‘asisti’ ambapo amecheza dakika 139, tu kwenye ligi lakini ametoa asisti tatu akiwa namba mbili kwenye msimamo huo nyuma ya Attohoula Yao wa Yanga anayeongoza akiwa nazo nne hadi sasa.

Bila shaka namba hizo zinawabeba wawili hao na kutoa presha kwa benchi la ufundi la simba kwa maana ya muda wanaowapa na makubwa wanayofanya lakini pia kwa wapinzani kupata presha namna ya kuwadhibiti.

Sambamba na hilo, wawili hao ni silaha zenye muunganiko bora ndani ya Simba kwani wamehusika kuipa Simba ushindi kwenye mechi mbili muhimu za ligi.

Katika mechi iliyopita dhidi ya Ihefu, wakati ubao wa matokeo ukisomeka 1-1, wawili hao waliingia uwanjani kipindi cha pili na kuipatia Simba ushindi ambapo Luis alipiga asisti kwa Phiri aliyeifungia Simba bao la pili na la ushindi na mechi kumalizika 2-1.

Halikadharika kwenye mechi dhidi ya Singida Big Stars, Phiri na Luis waliingia na kuipatia Simba ushindi ambapo Phiri alifunga bao la pili kwa Mnyama akimalizia asisti ya Luis na mechi kulala 2-1.

Hayo yote yanaongeza presha kwa wapinzani kwani ni mabadiliko ambayo yakifanywa mara nyingi yamekuwa na faida kwa Simba lakini presha kwa benchi la ufundi la Simba inabaki kuwa ile inayotoka kwa mashabiki ikishinikiza wapewe muda mwingi wa kucheza kwani wamekuwa na faida kuliko hata wanaoanza.

Mwanaspoti lilimtafuta Robertinho kuzungumzia hali hiyo amesema Phiri na Luis ni wachezaji muhimu katika kikosi chake na wamekuwa wakifanya vizuri kila anapowapa nafasi.

Robertinho amefafanua kuwa anapanga timu kutokana na mbinu na namna wanavyokuwa wakitaka kucheza hivyo hawawezi kuanza wote lakini wanakuwa kwenye mipango.

“Ni wachezaji wazuri na wamekuwa wakitupa kile tunachotaka. Napenda maendeleo yao na wanaisaidia timu kuhakikisha inapata ushindi,” amesema Robertinho ambaye ameiongoza Simba katika mechi 14 za mashindano yote msimu huu bila kupoteza na kuongeza;

“Wachezaji wa Simba wote wanaumuhimu kwetu na wanafanya vizuri, hauwezi kuwapanga wote kwani kila mechi inanamna yake ya kuicheza. ukiona mtu yupo kwenye orodha ya wachezaji wa mechi flani, jua yupo kwenye mpango wa mechi hiyo bila kujali ataanza ndani au benchi. Kwa sasa tunajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Yanga, hivyo tusubiri mtaona.”

Phiri na Luis wanacheza eneo la mbele la ushambuliaji ambalo kwa mara nyingi, Jean Baleke, John Bocco, Kibu Denis, Clatous Chama na Saidi Ntibanzokiza ndio wamekuwa wakipata muda mwingi wa kucheza katika maeneo hayo.

DETAILS BY NUMBERS

139- Dakika alizocheza Luis ligi kuu msimu huu.

143- Dakika alizocheza Phiri Ligi Kuu msimu huu.

3-Mabao aliyonayo Phiri Ligi Kuu, Simba ikiwa imecheza mechi sita

3-Asisti alizonazo Miquissone Ligi Kuu, Simba ikiwa imecheza mechi sita

SOMA NA HII  LIGI YA MABINGWA AFRIKA: SIMBA 1-0 AL AHLY