Home Habari za michezo MBRAZILI SIMBA ATAJA MBINU ZA KUMMALIZA MWARABU LEO…MO DEWJI AWEKA MIL 500...

MBRAZILI SIMBA ATAJA MBINU ZA KUMMALIZA MWARABU LEO…MO DEWJI AWEKA MIL 500 MEZANI..

Habari za Simba

HAKUNA ushauri wowote mwingine unaoweza kuwapa Simba leo watakapocheza na Al Ahly ugenini zaidi ya ule wa kupambana kwa jasho lao lote ili kupata matokeo mazuri yatakayowavusha kwenda hatua ya nusu fainali ya Kombe la African Football League.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa saa 11:00 jioni katika Uwanja wa kimataifa wa Cairo na Kocha Robertinho amesisitiza kwamba; “Tunao hawa, lazima tupambane kama timu kubwa kupata matokeo chanya.”

Kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote kikosi cha Simba kinaweza kuwa hivi, Ally Salim, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Enock Inonga, Che Malone, Sadio Kanoute, Clatous Chama, Fabrice Ngoma, Jean Baleke, Kibu Dennis na Saido Ntibazonkiza.

Matokeo ya sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza, Ijumaa iliyopita katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, yanailazimisha Simba kupata matokeo ya aina tatu ili iweze kuitupa Al Ahly nje ya mashindano hayo leo.

MATOKEO MATATU

Kwanza; ni kupata ushindi wa aina yoyote

Mbili; ni sare ya kuanzia mabao 3-3

Tatu; ni kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti baada ya kulazimisha sare ya mabao 2-2 ugenini.

Hata hivyo matokeo hayo yote ya aina tatu yanaonekana sio mepesi kupatikana kutokana na rekodi bora ya kufanya vizuri nyumbani ambayo Al Ahly wamekuwa nayo kuanzia katika mashindano ya ndani hadi ya kimataifa.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa tangu ilipofungwa mabao 2-0 nyumbani na Wydad Casablanca ya Morocco, Mei 30 mwaka jana, Al Ahly haijapoteza mechi nane mfululizo za mashindano ya kimataifa nyumbani, wakishinda michezo saba na kutoka sare moja huku wakifunga mabao 20 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara mbili tu.

BAO LA UGENINI

Tofauti na taarifa zilizosambaa kuwa faida ya bao la ugenini kwenye mashindano hayo haipo, kanuni za AFL zinafafanua kuwa iwapo timu mbili zitamaliza mechi mbili kwa matokeo ya sare, timu iliyofunga idadi kubwa ya mabao ugenini itasonga mbele.

“Kwa tukio la namba sawa ya mabao yamefungwa katika muda wa mwisho kikanuni wa mechi ya pili, kwa robo fainali na nusu fainali, timu yenye idadi kubwa ya mabao ya ugenini itaenda katika hatua inayofuata,” inafafanua kanuni ya 15.3 ya mashindano hayo.

500 MEZANI

Wachezaji wa Simba wanatarajia kuvuna kiasi kikubwa cha fedha ikiwa watafanikiwa kuitupa nje Al Ahly katika mchezo huo wa leo.

Licha ya klabu hiyo kutotangaza hadharani, ila inafahamika kuwa kwamba uongozi wa timu hiyo umepanga kuwapa zaidi ya Shilingi 500 milioni ikiwa mpango wa kupata ushindi ugenini utatimia. Kiasi hicho kilikuwa kimewekwa pia kwenye mechi ya nyumbani lakini ikaisha kwa sare.

REFA WA BAHATI

Mchezo wa leo utachezeshwa na refa Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo ambaye atasaidiwa na Jerson dos Santos wa Angola na Arsenio Marengula wa Msumbiji huku refa wa akiba akiwa ni Messie Nkounkou wa Congo.

Refa Ndala amekuwa na historia nzuri na Simba ambapo katika mechi tatu alizoichezesha, imeibuka na ushindi mara mbili na kupoteza mchezo mmoja.

MISRI PAGUMU

Simba imekuwa haina historia nzuri kwa mechi ambazo imekuwa ikicheza katika ardhi ya Misri kwani haijawahi kupata ushindi wa ndani ya dakika 90 hata mara moja.

Katika mechi 10 za mashindano tofauti ambazo Simba imecheza ndani ya ardhi ya Misri, imefunga michezo tisa na imetoka sare mara moja tu huku ikifunga mabao mawili na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.

Dhidi ya Al Ahly, Simba imekutana nao mara tatu katika mashindano ya kimataifa ambapo imepoteza zote pasipo kufunga bao hata moja huku ikifungwa mabao nane.

UFUNDI, NIDHAMU KUIBEBA

Simba inapaswa kuwa na nidhamu kubwa hasa ya kujilinda ili kuhakikisha Al Ahly hawana madhara makubwa kwao na wao waweze kupata matokeo mazuri yatakayowavusha.

Uimara wa hali ya juu unapaswa kuwepo katika safu ya kiungo ambayo imekuwa ikifanya makosa ya mara kwa mara ya kuruhusu wapinzani kumiliki mpira na kutengeneza nafasi, jambo linalopelekea safu ya ulinzi ishambuliwe mara kwa mara. Wawakilishi hao wa Tanzania wanapaswa kutimiza wajibu kitimu hasa kukaba na kutafuta mpira pindi unapokuwa kwa Al Ahly, jambo ambalo litawanyima uhuru wapinzani wao katika kutengeneza hatari kwao.

Kuepuka makosa binafsi ya kiulinzi kunaweza kuwa msaada mkubwa kwa Simba ambayo siku za jivi karibuni imeonekana kuruhusu idadi kubwa ya mabao kutokana na uzembe binafsi.

KOCHA HANA PRESHA

Kocha Roberto Oliveira wa Simba alisema ingawa wanafahamu watacheza mechi ngumu, upande wake hana wasiwasi na jambo muhimu ni wachezaji kutimiza waliyofanyia kazi mazoezini.

“Ahly ni timu kubwa. Tukirudia makosa kama ya mchezo uliopita yatatuweka kwenye wakati mgumu. Tutaendelea kukumbushana wakati wa mchezo. Tunahitaji kufunga mabao lakini lazima tuwe na kasi. Huu ni mchezo wa soka na nafasi ya kuwatoa Al Ahly tunayo kama tutacheza vizuri na kufanya vitu vya msingi uwanjani,” alisema Robertinho.

DAKIKA 45 TU

Kocha huyo amewataka wachezaji wajitume kama ambavyo walifanya dakika 45 za kipindi cha pili kwenye mchezo uliopita.

Simba inatakiwa kushinda ili kusonga mbele na Robertinho amebainisha kuwa ili kupata matokeo mbele ya miamba hiyo ya soka Afrika wachezaji wanatakiwa kujitoa kwa kucheza kama walivyofanya Dar es Salaam dakika za lala salama zilizomkosha na kutamani muda ungeongezwa huenda wangepata matokeo mazuri zaidi.

“Kipindi cha pili tulicheza vizuri na tunapaswa kufanya vivyo hivyo kesho (leo). Tunakutana na timu kubwa lakini nawaamini wachezaji wangu wapo tayari kwa mchezo,” alisema Robertinho.

CREDIT:- MWANASPOTI

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUAGA MSIMBAZI...CHAMA AFUNGUKA HAYA KUHUSU MO DEWJI NA BARBARA