Home Habari za michezo KUHUSU KURUDI TENA SIMBA…SVEN AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA UGUMU ULIOPO…

KUHUSU KURUDI TENA SIMBA…SVEN AVUNJA UKIMYA…AFUNGUKA UGUMU ULIOPO…

Habari za Michezo

Kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck amesifia mashabiki wa klabu hiyo lakini akataja changamoto zilizoko kwenye viwanja vya mikoani.

Amekwenda mbali zaidi na kufunguka kinachoendelea katika kutakiwa na Simba na klabu za Afrika Kusini.

“Niko tayari kufundisha Simba au Afrika Kusini,” Kocha huyo Mbelgiji aliuambia mtandao wa iDiski Times wa Afrika Kusini.

“Naijua klabu na mazingira yake, wana mashabiki wengi wenye mapenzi na timu. Wana faida ya Ligi ya Mabingwa, lakini kwenye mechi za mikoani kuna changamoto.

“Ligi ya Afrika Kusini ni kubwa na rasilimali zao ni nzuri zaidi,” alisema Sven ambaye yupo kwenye orodha ya makocha watano Simba inaowataka.

Kocha huyo mwenye miaka 44, alisema matatizo mbalimbali ndiyo yaliyomsababisha kukaa kwenye klabu za Morocco na Algeria kwa muda mfupi.

“Pale Wydad nilisaini miezi minne kwa sharti la kubeba ubingwa wa Afrika tukapoteza kwa Ahly, CRB ni tofauti nilikataa kupangiwa timu na viongozi,” alisema Sven ambaye baadhi ya viongozi wa Simba wanaamini misimamo yake itawanyoosha baadhi ya mastaa wao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salum Abdallah ‘Try Again’ alisema ni kweli Simba inasaka kocha lakini watawatangazia mashabiki wao watakapompata kocha sahihi.

Akizungumzia suala la kocha baada ya kutajiwa jina la Sven alisema ni kocha mzuri aliacha rekodi nzuri ndani ya Simba na amefanya mambo makubwa Morocco.

“Ni kocha mzuri lakini siwezi kusema ndiye anayeweza kuja kuinoa Simba ila mashabiki na wanasimba wanatakiwa kufahamu tutamleta kocha mzuri anayelifahamu soka la Afrika na Ligi ya Mabingwa;

“Lengo ni kuona anatuongoza kuanzia tulipo na kutufikisha sehemu kubwa ambayo tumekuwa tukiitamani muda mrefu hatua ya Nusu fainali Ligi ya Mabingwa na mchakato wake unaenda vizuri anaweza kuja kabla ya mchezo wetu wa hatua ya makundi nyumbani au baada,” alisema Try Again.

SOMA NA HII  ROBERTINHO AFUNGUKA HAYA KUHUSU LUIS MIQUISSONE