Home Habari za michezo KIVUMBI LEO BENCHIKHA AINGIA KATIKA MTIHANI MWINGINE

KIVUMBI LEO BENCHIKHA AINGIA KATIKA MTIHANI MWINGINE

Habari za Simba

Simba inarudi tena uwanjani jioni ya leo Ijumaa dhidi ya Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara, ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutoonja ushindi kwenye michezo mitano, huku kocha na mastaa wa timu hiyo wakipiga mkwara lazima kieleweke ili kutengeneza morali kabla ya kurejea kwenye michuano ya CAF.

Simba itavaana na Kagera kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni, ikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha ambaye anasaka ushindi wa kwanza tangu awe na timu hiyo, lakini tayari wageni, Kagera wamesisitiza hata wao wanazitaka pointi tatu.

Kagera imepoteza mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union baada ya awali kutoka sare ya 1-1 na KMC na kocha wa timu Mecky Maxime amesema wanashuka Uhuru wakiwa na kiu ya kutaka ushindi licha ya kukiri wapinzani wao sio timu ya kubezwa kulingana kikosi chao kilivyo kwa sasa.

Rekodi zinaonyesha, Simba ilionja ushindi mara ya mwisho Oktoba 28 ilipoifunga Ihefu kwa mabao 2-1, lakini baada ya hapo imecheze mechi mbili za Ligi Kuu Bara, ikipoteza 5-1 kwa Yanga na kuambulia sare ya 1-1 na Namungo, huku michezo mitatu iliyofuata ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilitoka sare mbili dhidi ya Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy kisha kulala 1-0 kwa Wydad Casablanca.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa aina yake kutokana na kiu ya mashabiki ya kutaka kumuona Kocha Benchikha ataanzaje Ligi Kuu baada ya kuiongoza timu hiyo kwenye michezo miwili ya michuano ya CAF ikiwamo ile ya suluhu na Jwaneng kule Botswana na Wydad, huku ikiupiga mwingi.

Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Benchikha nyumbani na ya kwanza kwake kwenye ligi akiwa amechukua mikoba baada ya kutemwa kwa Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ mara baada ya kichapo cha Yanga na kocha huyo raia wa Algeria alisema kulingana na ratiba ilivyo, katika kikosi chake cha leo kutakuwa na mabadiliko makubwa kimbinu na nafasi ambapo mastaa wengi waliocheza mechi mbili zilizopita.

“Kulingana na ratiba ilivyo, kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye kikosi, lakini pamoja na hilo hatutapoteza lengo letu la kushinda mechi hiyo,” alisema Benchikha, aliyesisitiza anaweka nguvu kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Wydad itakayopigwa Jumanne ijayo Kwa Mkapa.

Kocha wa Kagera, Mecky Maxime alisema kikosi chake kilijiandaa na mechi hiyo tangu kikiwa kambi Bukoba kabla ya kwenda Tanga kucheza na Coastal Union, hivyo wako tayari kuikabili Simba na mchezaji pekee atakayekosekana kwenye mechi hiyo Allen Ngeleka aliyepata kadi nyekundu kwenye mechi ya Coastal.

“Hapa tumekuja kukamilisha tulichofanya Bukoba, wachezaji wapo tayari kwa mechi hiyo.

“Tunaiheshimu Simba ni timu bora Afrika, imetoka kucheza na vigogo wa Afrika hivyo ina morali ya juu. Tutaingia uwanjani kwa tahadhari huku tukitafuta matokeo mazuri,” alisema Maxime nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars.

Kagera haijawa na matokeo bora kwenye mechi tano zilizopita imepata ushindi mechi moja tu, sare mbili na kupoteza mbili, lakini ikiwa na tatizo butu na kufumania nyavu kama Simba kwa sasa.

Kama Simba itashinda au kutoa sare mechi hiyo itazishusha Singida Fountain Gate na KMC zilizo juu yake na alama 20 kila moja na kukaa kwenye nafasi ya tatu nyuma ya Azam na Yanga na kama Kagera itashinda itapaa hadi nafasi ya nane na kama ikipata sare basi itakaa nafasi ya tisa.

Simba inarekodi nzuri mbele ya Kagera katika michezo 10 ya mwisho walipokutana Simba imeshinda saba, Kagera ikishinda miwili na sare moja.

Katika mechi hizo 10, za mwisho timu hizo zilipokutana, mechi zilionekana kuwa ngumu huku yakifungwa mabao machache kwani hakuna mchezo baina yao uliozidisha mabao matatu.

Mechi ya Ligi iliyopigwa Aprili 20, 2019 na kumalizika kwa Kagera kushinda 2-1 na ile ya Septemba 29, 2019 ambayo Simba ilishinda 3-0 ndiyo michezo pekee ambayo imetoa mabao matatu tu kati ya mechi 10 za mwisho.

Kipa wa Simba, Ally Salim alisema kwa upande wa wachezaji wamejipanga vyema na mechi hiyo huku kiungo Abdallah Seseme wa Kagera akisema chama lake linasubiri mechi tu.

“Kama wachezaji tuna morali nzuri, tunatambua ubora wa Kagera lakini tunatarakjia kuwa na mechi bora na kushinda,” alisema Ally. “Ni mechi ngumu lakini tupo tayari kupambana. Tunasubiri muda ufike na dakika 90 zitaamua,” alisema Seseme.

Vikosi tarajiwa; SIMBA: Ally Salim, Israel Mwenda, David Kameta, Kennedy Juma, Che Malone, Sadio Kanoute, Moses Phiri, Mzamiru Yassin, Jean Baleke, Clatous Chama na Luis Miquissone.

KAGERA: Ramadhan Chalamanda, Datius Peter, Charles Luhende, Deus Bukenya, Abdallah Mfuko, Ally Nassoro, Cleophas Mkandala, Abdallah Seseme, Anuary Jabir, Nicholaus Kasozi na Obrey Chirwa.

SOMA NA HII  KAMA UNAMPENZI HII INAKUHUSU ..PATA ZAWADI YA VALENTINE NA UUMPENDAYE ...SIMPLE TU NA Infinix...