Home Habari za Simba Leo MAMBO MATANO YALIYOIPA SIMBA UBINGWA…MGUNDA AHUSIKA

MAMBO MATANO YALIYOIPA SIMBA UBINGWA…MGUNDA AHUSIKA

Habari za Simba

Msimu wa 2023/2024 kwa wanawake ulimalizika kwa Simba Queens kufanikiwa kutwaa ubingwa bila kupoteza mchezo wowote, ukiwa ni ubingwa wao wa 4 tangu ligi hiyo ianzishwe mwaka 2017.

Simba ilichukua ubingwa huo wiki moja kabla ligi haijamalizika jijini Mwanza baada ya kuichakaza Alliance Girls kwa mabao 3-0 na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa ajili ya msimu ujao.

Timu hiyo ilibeba ubingwa kwenye mchezo wa raundi ya 16 huku ikiwa imesalia michezo miwili ikifikisha pointi 46 ambazo hazitafikiwa na JKT yenye pointi 43 na Yanga Princess yenye nazo 36, huku juzi ikihitimisha baada ya kufikisha pointi 52 ilipoichapa Geita mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kuna mambo kadhaa yamechangia Simba Queens itwae ubingwa huu msimu huu, na kuzipoteza timu nyingine ikiwemo Yanga ambayo imemaliza nafasi ya ya tatu na JKT ya pili.

SAFU BORA YA ULINZI NA USHAMBULIAJI

Baada ya kupoteza ubingwa msimu uliopita ambao JKT Queens ilibeba, msimu huu ilihakikisha inashinda karibu kila mchezo ili kujiweka sawa.

Mzunguko wa kwanza ambao kila timu inacheza michezo tisa, Simba ilishinda nane na kutoa sare mechi moja dhidi ya Bunda Queens ya mabao 2-2 ugenini.

Tangu raundi ya sita mabingwa hao hawajapoteza mchezo wowote na ikiwa ni miongoni mwa timu zilizoruhusu mabao machache baada ya kufungwa saba pekee msimu mzima.

Mbali na hivyo ndio timu inayoshika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi, ikifunga 55 nyuma ya JKT iliyofunga 59.

Pia msimu huu timu hiyo imefanikiwa kuwafunga wapinzani wao wote, iliichapa JKT nyumbani na ugenini na Yanga nyumbani na ugenini, ikiifunga jumla mabao 6-2.

UBORA WA BENCHI LA UFUNDI

Msimu uliopita Simba ilifukuza Kocha wake mkuu, Charles Lukula ambaye sababu ya kuondoka ni kushindwa kuipatia timu hiyo ubingwa lakini msimu huu ikiongeza gia baada ya kumchukua mzoefu Juma Mgunda kusaidiana na Mussa Mgosi.

Hawa walisaidiana kuhakikisha timu hiyo inatwaa ubingwa huku Mgosi akiwa ndiye kocha mwenye uzoefu mkubwa zaidi kwenye michuano hiyo kwa sasa.

Makocha wote wawili walicheza Simba kwa miaka tofauti lakini pia waliwahi kufundisha timu hizo hivyo kukaa muda mrefu kwenye timu hiyo kuliisaidia kuchukua ubingwa.

USAJILI MZURI.

Mabingwa hao wa nne wa WPL msimu huu wamesajili wachezaji wanne pekee wawili wa kigeni na wawili wazawa ili kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Ni timu ambayo imesajili wachezaji wachache ukiachana na JKT waliosajili wachezaji saba na Yanga Princess 13 wachezaji ambao hawakuisaidia.

Kwenye wachezaji wanne wapya, watatu tu ndio wameingia kikosi cha kwanza, Riticia Nabbosa kwenye eneo la kiungo, Elizabeth Wambui na Joanitha Ainembabazi eneo la winga.

Kitendo cha kuongeza wachezaji hao ambao wana uzoefu na soka hilo kuliisaidia timu hiyo kwanza kupunguza bajeti ya usajili na kuliongeza ushindani wa namba kwenye kikosi hicho.

UWEZO MKUBWA WA WACHEZAJI WAZAWA

Ukitaja mafanikio ya Simba msimu huu huwezi kuacha kutaja juhudi za wachezaji wazawa ambao wamekuwa na mchango mkubwa.

Eneo la ulinzi Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na Violeth Nickolaus wamekuwa na mchango mkubwa wa kuzuia mashambulizi eneo lao kwani kwenye mechi 18 imeruhusu mabao saba pekee ikiwa sawa na JKT.

Wawili hao wamekuwa na utawala kwenye eneo hilo kitendo kilichompa wakati mgumu wa kupata namba kwa Mkenya Ruth Ingosi ambaye amekuwa akipata dakika chache.

Ukiachana na mabeki, eneo la washambuliaji limekuwa chachu kwenye ligi hiyo ambayo hadi sasa Simba kupitia straika wao, Aisha Mnunka ambayeameibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 20 yamekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo msimu huu.

MCHANGO WA MASHABIKI NA VIONGOZI

Kadri ligi inavyozidi kuendelea ndivyo inakuwa na mvuto wa aina yake lakini wanaonegesha hayo ni mashabiki, Simba ndiyo timu pekee kwenye ligi hiyo ambayo ilikuwa na mashabiki wengi zaidi msimu huu na misimu miwili iliyopita.

Mashabiki wa Simba wamekuwa wakisafiri na timu hiyo na mfano mzuri ni mchezo dhidi ya Alliance ambao walisafiri na Coaster kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kuiunga mkono timu hiyo.

Lakini pia timu hii inaweza kuwa ndiyo yenye sapoti kubwa zaidi ya viongozi wa juu wa timu hiyo, ni rahisi mara kwa mara kumuona Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Iman Kajula jukwaani, Ahmed Ally na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Asha Baraka ambaye ndiye msimamizi wa timu hii.

Makombe Ligi Kuu Wanawake

2016/17 – Mlandizi Queens
2017/18 – JKT Queens
2018/19 – JKT Queens
2019/20 – Simba Queens
2020/21 – Simba Queens
2021/22 – Simba Queens
2022/23 – JKT Queens
2023/24 – Simba Queens.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI vs AL AHLY...KADUGUDA AIBUKA NA HILI JIPYA.....AMTAJA BARBARA KUHUSIKA...