Home Habari za Simba Leo SABABU ZILIZOMFANYA MO DEWJI KUTIMUA WAJUMBE SIMBA

SABABU ZILIZOMFANYA MO DEWJI KUTIMUA WAJUMBE SIMBA

Habari za Simba Leo

Ni takribani siku ya tatu sasa kuna mambo kibao yanaendelea ndani ya Simba. Tajiri Mohamed Dewji ‘MO’ ameingia msituni mwenyewe kufanya mawindo ya wachezaji watakaorudisha heshima ya Simba iliyojiwekea kwa miaka ya nyuma.

MO Dewji Ameamua kufumua kitu kimoja baada ya kingine kwa vitendo katika kuhakikisha Simba inakuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao na kurejesha heshima ambayo imepoteza katika misimu mitatu mfululizo iliyopita.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya baada ya Simba kumaliza msimu ikiwa haijatwaa taji lolote kubwa huku ikimaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, Dewji ameingia kazini kwa kufanya uamuzi mgumu ambao unalenga kuweka mambo kwenye mstari ulionyooka ili timu isiwe na unyonge msimu ujao.

Huenda ukawa unajiuliza ni sababu zipi zilizomfanya MO Dewji kuwashinikiza wajumbe wake wajiuzulu wenyewe? Soka la Bongo tumekuletea sababu hizo ni kama ifuatavyo;

Usajili usio wa kuridhisha wa wachezaji na makocha, kufanya vibaya kwa misimu mitatu mfululizo pamoja na ucheleweshaji wa klabu kuingia kwa asilimia mia kwenye mfumo wa uwekezaji ni sababu tatu zilizomfanya Mwekezaji wa Simba Mohamed Dewji kuwataka wajumbe wa bodi upande wake kujiuzulu kwa mpigo.

Wajumbe watano tayari wameshaachia ngazi, huku mmoja akiwa bado, lakini ikielezwa kuwa mustakabali wake utajulikana siku chache zijazo.

Watano hao ni kati ya sita ambao waliteuliwa na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji na aliyebakia ni mmoja tu ambaye ni Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo.

Watano hao ambao wameamua kujiweka pembeni ni Raphael Chegeni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo, Rashid Shangazi na Hussein Kita.

Inaripotiwa kuwa vigogo hao wameamua kujiwajibisha kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika miaka ya hivi karibuni ambapo kwa kipindi cha misimu mitatu mfululizo, imeshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na ule wa Kombe la Shirikisho la Azam huku mara kadhaa ikiishia hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika.

Lakini pia mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji inaripotiwa hajafurahishwa na usajili wa wachezaji mbalimbali uliofanywa na timu hiyo katika kipindi hicho sambamba na kuchelewa kukamilisha mchakato wa mabadiliko, jambo analoamini limechangiwa na kutokuwepo na usimamizi mzuri kutoka kwa bodi ya wakurugenzi.

SOMA NA HII  KWA SIMBA HII MTAFURAHI WENYEWE