Home Habari za Yanga Leo YANGA KUWEKA KAMBI YA PRE SEASON URUSI…KILA KITU KIMEKAMILIKA

YANGA KUWEKA KAMBI YA PRE SEASON URUSI…KILA KITU KIMEKAMILIKA

Habari za Yanga leo

KLABU ya Yanga imepokea mualiko wa kuweka kambi ya maandalizi ya msimu wa 2024/25 huko Ulaya,  hii ni baada ya miaka mitatu ya klabu hiyo kufanya pre season yao hapa nchini Tanzania maeneo ya  Avic town.

Yanga imepata mwaliko mzito kutoka klabu ya CSKA Moscow ya Urusi, kupeleka wachezaji kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

Klabu hizo ziliingia makubaliano ya ushirikiano utakaoifanya Yanga kupeleka wachezaji wa timu ya vijana wenye vipaji.

Hivyo kwa kuanzia ni hapa katika kipindi cha pre-season na Yanga itaweka kambi huko, ambapo tayari wameshaanza kutengeneza mchakato wa safari hiyo kwa kuwaombea visa wachezaji.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Yanga kwenda huko, kwani kabla ya kuamua kujichimbia Avic, klabu hiyo ilikuwa na utamaduni wa kuipeleka timu Uturuki na mara moja ilienda Morocco ambako hata hivyo haikuwa kambi nzuri kwa afya ya timu hiyo.

Hata hivyo, kwa upande wa Kocha Miguel Gamondi hii itakuwa ni mara ya kwanza kutoka na kikosi hicho nje ya Tanzania kwa ajili ya mapumziko na maandalizi ya msimu mpya, kwani msimu uliopita hakutoka na hata ilipokuwa chini ya Nasreddine Nabi pia tangu ilipozinguliwa Morocco mwaka juzi hakuitoka kabisa nje.

Ofisa wa Habari wa Yanga, Ali Kamwe aliweka wazi, msimu huu utakuwa tofauti, kwani hawatakuwa na maandalizi ya pre season Avic Town.

“Rais wetu alishaweka wazi katika mkutano mkuu wikiendi iliyopita, tuna mialiko sehemu tatu, Afrika Kusini tumealikwa na Kaizer Chiefs baada ya kuwaalika katika kilele cha Wiki ya Wananchi, Kenya tulipokea mwaliko wa Raila Odinga na Ulaya, hivyo ni wazi msimu huu tutakuwa nje ya nchi,” alisema Kamwe na kuongeza;

“Wakati ukifika tutaweka wazi mahali kambi yetu inapoandaliwa na itakuwa Ulaya hivyo kila kitu tutakisema ila bado maandalizi yanaendelea.”

Katika misimu yote ambayo Yanga haikuweka kambi nje ya nchi ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, na Kombe la Shirikisho mara tatu mfululizo na Ngao ya Jamii mara mbili pamoja na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika.

Tayari dirisha la usajili kwa klabu za soka nchini kwa ajili ya msimu ujao limefunguliwa jana na linatarajiwa kufungwa Agosti 15, hivyo inaweza kuirahisishia Yanga kuondoka na majembe yote itakayowasajili kabla ya kurejea nchini kuzindua msimu na Tamasha la Mwananchi na mechi za Ngao ya Jamii mapema Agosti.

SOMA NA HII  HII HAPA NJIA YA MAYELE KUIBUKA MFUNGAJI BORA AFRIKA...MECHI MBILI TU ANABEBA KIATU CHA DHAHABU....