Home Habari za Simba Leo SIMBA KUANZA NA FAD FC YA DJIBOUT

SIMBA KUANZA NA FAD FC YA DJIBOUT

Habari za Simba

KLABU ya Simba Queens, inatarajia kuanza kampeni yao Ligi ya Mabingwa Afrika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuanza kucheza na klabu ya FAD FC ya Djibout kwenye michuano hiyo.

Simba imepangwa kwenye kundi B katika michuano hiyo na itashuka uwanjani Agosti 18 kucheza na mabingwa hao wa Djibout.

Katika droo iliyochezeshwa juzi nchini Misri, Simba Queens ambao ni Mabingwa wa Tanzania Bara, wamepangwa na PVP Buyenzi ya Burundi, Kawempe Musilim Ladies kutoka Uganda na FAD FC.

Kwenye Kundi A ya michuano hiyo Kati kuna timu za CBE ya Ethiopia, Polisi ya Kenya, Yei Joint FC ya Sudan Kusini, Warriors Queens ya Zanzibar na Rayon Sport ya Rwanda.

Droo hiyo pia imehusisha pia mabingwa kutoka nchi za kanda zingine Afrika kama ya kanda ya Kusini, Kaskazini na Kati, ambapo nao wamepangwa kwa makundi.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), washindi wa kwanza wa michuano hiyo kila kanda watafuzu fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika zinazotarajiwa kufanyika nchini Morocco, Julai sita hadi 26 mwakani, ikizishirikisha jumla ya timu 12.

Ili Simba Queens icheze fainali ya michuano hiyo, inatakiwa kuwa mabingwa wa CECAFA, kama ilivyofanya Agosti 17, 2022 ilipotwaa ubingwa huo katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kwa kuifunga Corporate ya Uganda bao 1-0 na kufuzu kucheza fainali hizo za Afrika Novemba mwaka huo nchini Morocco na kufika hatua ya nusu fainali.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda alisema anatarajia ugumu kwenye michuano hiyo, lakini ana wachezaji ambao wanaweza kupambana na kutwaa ubingwa wa CECAFA.

“Tunakwenda kushindana, kwa hiyo ni lazima tujiandae vizuri kuhakikisha tunafanya vyema kwenye michuano hiyo, najua itakuwa migumu kwani timu zote zinazoshindana ni mabingwa wa nchi zao, lakini mwisho wa yote tunatarajia kuwa mabingwa,” alisema.

SOMA NA HII  MABOSI SIMBA WATUA NYUMBANI KWA KINA PACOME...MIPANGO YATEKELEZWA KIMYA KIMYA