Home Habari za Yanga Leo KESI YA MAGOMA NA YANGA ILVYOKUWA…KWA UNDANI ZAIDI MAMBO YALIKUWA HIVI.

KESI YA MAGOMA NA YANGA ILVYOKUWA…KWA UNDANI ZAIDI MAMBO YALIKUWA HIVI.

Habari za Yanga

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeruhusu Klabu ya Yanga kufanya mapitio ya marejeo ya shauri la madai namba 187/2022 lililofunguliwa na Juma Magoma na mwenzake Geofrey Mwaipopo.

Pia mahakama hiyo imetupilia mbali mwenendo mzima wa kesi hiyo ya madai namba 187/2022 na kuweka kando amri zote zilizotolewa katika katika hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023.

Kuhusu gharama za shauri hilo la mapitio, mahakama hiyo imeamuru Magoma, Mwaipopo na Abeid Mohamed Abeid, wailipe Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga.

Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, wakati akitoa uamuzi katika shauri la maombi ya marejeo namba 17939/2024 iliyofunguli na Bodi ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga ambao ndio waombaji dhidi ya Juma Magoma na Geofrey Mwaipopo.

Bodi hiyo ya Wadhamini wa Klabu ya Yanga kupitia mawakili wake, Kalaghe Rashid na Respicius Didace na Mkurugenzi wa Sheria wa Klabu hiyo, Simon Patrick wameiomba mahakama ifanye marejeo na watupilie mbali hukumu iliyotolewa Agosti 2, 2023 ambayo ilifunguliwa na Magoma na Mwaipopo.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Kiswaga ameisema waombaji katika shauri hilo la marejeo waliwasilisha maombi yao chini ya kifungu 78(1) A na B cha amri ya 42 kanuni 1A na B na 2 ya sheria ya usikilizwaji wa mashauri ya madai sura 33 iiyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Hakimu Kiswaga amesema bodi hiyo iliwasilisha sababu nne katika maombi yao dhidi ya Magoma na Mwaipopo.

Hakimu Kiswaga ameizitaja sababu hizo kuwa, Magoma na Mwaipopo walipeleka maombi yao katika Mahakama ambayo haina Mamlaka ya kusikiliza maombi yao.

“Sababu ya pili, Magoma na Mwaipopo walikuwa hawana haki ya kuwashtaki Bodi ya Wadhamini na Klabu ya Yanga kwa wababu hawakutoa uthibitisho wa kadi ya uanachama wao mahakamani,” amesema Hakimu Kiswaga.

Sababu ya tatu, Magoma na Mwaipopo walifungua kesi yao kwa njia ya maombi ya madai na sio kesi ya madai.

“Kwa maana Magoma na Mwaipopo walifungua shauri lao kwa njia ya maombi badala ya kufungua shauri la madai,” amesema Hakimu.

Sababu ya nne, Bodi ya Wadhamini ya Yanga ilidai kuwa walinyimwa haki ya kusikilizwa katika shauri lililofunguliwa na Magoma pamoja na wenzake na kwamba hawakuwahi kupewa hati yoyote ya wito wa mahakama wala hawajawahi kumruhusu mtu yoyote kuwawakilisha mahakamani hapo katika kesi hiyo ya madai namba 187/2022.

Hakimu Kiswaga ameendelea kuchambua uamuzi kwa kusema mjibu maombi namba nne katika shauri hilo, Abeid Mohamed Abeid alisimama kama Mwenyekiti wa Bodi na alisimama pia kama mjibu maombi na alisimama kwa niaba ya Fatuma Karume ambaye ni mjibu maombi wa pili katika.hukumu hiyo ya madai namba 187/2022.

“Niliangalia na kuipitia hukumu hiyo ya madai namba 187/2022 iwapo Abeid alipewa mamlaka ya kuwawakilisha Fatma Karume na Bodi ya Wadhamini,” amesema

Hakimu Kiswaga amesema sababu ya kwanza iliyowasilishwa na Bodi ya wadhamini anakubaliana nayo na kwamba shauri la Magoma na Mwaipopo lilipaswa kufunguliwa Mahakama Kuu na sio Mahakama ya Kisutu

“Ni wazi kwamba shauri 187/2022 lilipaswa kufunguliwa Mahakama Kuu kwa sababu ndio yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na sio Mahakama ya Kisutu kwa mujibu wa kifungu cha 26 cha sheria inayohusu masuala ya sheria ya bodi ya wadhamini,” amesema Hakimu.

Kuhusu sababu ya pili iliyowasilishwa na waleta maombi ya marejeo, Hakimu Kiswaga amesema mahakama imeona haina mashiko kwa sababu ili mahakama iweze kufanya marejeo haipaswi kwenda kuangalia ushahidi, suala la Magoma na wenzake kuwa na kadi ya uanachama ni suala la kiushahidi hivyo halina mashiko.

Kuhusu sababu ya tatu ambayo Magoma na mwenzake kufungua shauri lao kwa njia ya maombi badala ya kufungua kesi ya madai, Hakimu Kiswaga amesema jambo hilo halikiwa sahihi kisheria.

“Hivyo, mahakama inaona hii ni sababu moja wapo ya mahakama kufanya marejeo ya shauri hili,” amesema hakimu huyo na kuongeza;

“Baada ya mahakama kupitia kumbukumbu ya shauri la madai namba 187 ya mwaka 2022 imeona Abeid Mohamed Abeid alijitanabaisha kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Yanga na alijiwakilisha kama Fatma Abeid Karume bila kuwa na idhini au mamlaka au udhibitisho kutoka kwa wahusika hao.”

Ameongeza wahusika hao waliwasilisha maombi kuwa hawajawahi kuleta uthibitisho huo na Abeid Mohamed Abeid ambaye ni mjibu maombi hajawahi kujibu chochote na wala Fatuma Abeid Karume na Bodi ya Wadhamini hawajawahi kutuma mtu kuwawakikisha hivyo walinyimwa haki yao ya kusikikizwa.

“Hivyo kwa sababu hizi, mahakama inaona maombi haya ya marejeo yana mashiko na yamekubaliwa na mahakama,” amesema Hakimu Kiswaga na kuongeza

“Pia mahakama hii inatupilia mbali mwenendo mzima wa kesi ya madai namba 187/2022 na kuweka kando amri zote zilizotolewa katika hukumu hiyo na tuzo zilizotolewa Agosti 2, 2023.”

Kuhusiana na gharama za kesi ya maombi ya marejeo, Hakimu Kiswaga amesema mahakama yake inaamuru Magoma, Mwaipopo na Abeid Mohamed Abeid wailipe waombaji ambao ni Bodi ya wadhamini wa Klabu ya Yanga.

Awali kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, wakili wa waleta maombi ya marejeo, Rashid na Patrick walidali wapo tayari kusikiliza uamuzi na upande wa wakili wa Magoma na Mwaipopo, Jacob Mashenene wakati mjibu maombi namba nne Abeid Mohamed Abeid yeye alijisimamia.mwenyewe.

Hata hivyo, leo Magoma na Mwaipopo hawakuwepo mahakamani wakati uamuzi huo unatokewa na badala yake alikuwepo wakili wao.

KESI YA MSINGI

Katika shauri hilo klabu ya Yanga kupitia wakili wake, Rashid na Didace waliiomba mahakama hiyo irejee uamuzi uliobatilisha Katiba yake ya mwaka 2011.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Pamela Mazengo, Agosti 2, 2023 ilibatilisha Katiba ya sasa ya Yanga ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011.

Uamuzi huo ulitokana na kesi iliyofunguliwa Agosti 4, 2022 na Magoma na mwenzake Mwaipopo, wanaojitambulisha kama wanachama wa klabu hiyo.

Katika kesi hiyo, Magoma na Mwaipopo walipinga Katiba hiyo ya mwaka 2011 kuwa si halali kisheria na kwamba Katiba halali inayotambulika ni ile ya mwaka 1968.

Hivyo, waliiomba mahakama hiyo itamke kuwa Katiba ya mwaka 2011 ni batili na Wajumbe wa Bodi waliopo kwa Katiba ya sasa hawana uhalali na miamala yote ya kifedha waliyoifanya ni batili.

Kesi hiyo ilisikilizwa upande mmoja bila wadaiwa wengine kuwepo kwa madai kuwa walipelekewa wito wa mahakama lakini hawakuitikia.

Katika uamuzi, mahakama hiyo ilikubaliana na madai na maombi ya kina Magoma, ikatamka kuwa Katiba ya sasa ya Yanga, (2011) haitambuliki kisheria na kwamba Katiba halali ya klabu hiyo ni ya mwaka 1968.

Hivyo, ilisema Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya mwaka 2011 si halali na chochote kilichofanywa na bodi hiyo ni batili na ikaamuru Bodi ya Wadhamini ya mwaka 1968 ndio irejeshwe katika uongozi kuendesha klabu hiyo.

Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Yanga kwa sasa ni George Mkuchika (Mwenyekiti ), Fatma Karume, Dk Mwigulu Lameck Nchemba, Tarimba Abbas na Anthony Mavunde.

Pia mahakama hiyo iliamuru kuwa miamala yote ya kifedha iliyofanywa na Bodi ya Wadhamini wa Klabu hiyo iliyoingia madarakani kwa Katiba ya sasa ni batil.

Hata hivyo, hukumu hiyo haikuwahi kujulikana hadi Julai 16, 2024, mwaka mmoja baadaya ilipoibuka katika vyombo vya habari likiwemo Mwananchi, baada ya walalamikaji hao kurudi mahakamani hapo kuomba utekelezaji wa hukumu hiyo.

Uongozi wa klabu hiyo, kupitia Mkurugenzi wa Sheria, Wakili Simon Patrick ulieleza hakuwa unafahamu kuwepo kwa kesi na hukumu hiyo, huku akibainisha kuwa klabu hiyo itavhukua hatua za kuupinga, Kwa kuwa haikukubaliana nao.

Hata hivyo, hadi wakati huo ilipoupata uamuzi huo ilikuwa imeshachelewa kuchukua hatua zozote za kuupinga.

Hivyo ililazimika kuomba kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya marejeo kupinga uamuzi huo nje ya muda, ikakubaliwa ndipo wakafungua maombi haya ya marejeo.

Shauri hilo lilisikilizwa Jumatatu, Agosti 5, 2024, ambapo Klabu ya Yanga iliwasilishwa na mawakili Rashid na Didace, huku wajibu maombi, Magoma na Mwaipopo waliwakilishwa na Mashenene.

Wakati wa usikilizwaji huo,awakili wa Yanga walibainisha kile wanachokiona kama.kasoro katika hukumu ya awali wanayoipinga.

SOMA NA HII  KISA YANGA KUKUTANA NA WASAUZI...ABDI BANDA AIBUKA NA HILI JIPYA...'AMFUNDISHA KAZI' NABI...