Home Habari za Simba Leo SIMBA YAFUNGUKA INSHU YA FREDDY FUNGAFUNGA

SIMBA YAFUNGUKA INSHU YA FREDDY FUNGAFUNGA

Habari za Simba- Freddy

UONGOZI wa Simba uko katika hatua za mwisho za kuachana na mshambuliaji, Freddy Michael Koubalan baada ya kuitumikia kwa miezi sita akitokea Green Eagles ya Zambia.

Hatua ya Simba kuachana na nyota huyo inakuja baada ya kukamilisha dili la mshambuliaji Mcameroon, Leonel Ateba aliyetua huu akitokea USM Alger ya Algeria.

Afisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema Freddy yupo hatua za mwisho za kuondoka huku akiweka wazi kuna moja ya timu kutokea Nigeria inayomuhitaji.

“Siwezi kusema ni timu gani anayokwenda kwa sababu tumeshamuachia wakala wake afanye hiyo kazi ila ni kweli tunamuuza na klabu ni ya Algeria, dili hilo liko hatua za mwisho kukamilika hivyo tutaweka wazi kila kitu kitakapokamilika,” alisema Ahmed.

Wakati Ahmed akizungumza hayo, kuna taarifa kuwa, nyota huyo huenda akatua JS Kabylie ya Algeria inayonolewa na aliyekuwa Kocha wa Simba Mualgeria, Abdelhak Benchikha aliyeondoka Aprili 28, mwaka huu.

Benchikha amekuwa na mawasiliano mazuri na baadhi ya wachezaji wa Simba na katika kudhibitisha hilo tayari ameondoka na nyota kadhaa wakiwemo viungo, Sadio Kanoute na Babacar Sarr waliojiunga na JS Kabylie huku Freddy akiwa miongoni mwao.

Freddy raia wa Ivory Coast alijiunga na Simba Januari 19, mwaka huu baada ya kuachana na Green Eagles ya Zambia ambapo alionyesha kiwango bora na kikosi hicho cha Msimbazi na kufunga jumla ya mabao sita ya Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita.

Licha ya kujiunga na Simba dirisha dogo la Januari, Freddy ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zambia (MTN Super League) msimu uliopita baada ya kufunga mabao 14 na kufikisha mabao 20 katika ligi zote mbili tofauti.

Nyuma ya Kouablan walikuwa Enock Sakala wa Zesco aliyefunga mabao 12, Andrew Phiri wa Muza FC akimaliza na mabao 11 huku washambuliaji wawili wa mabingwa wapya wa nchi hiyo, Ricky Banda na Saddam Phiri wote wakimaliza na mabao 10 kila mmoja.

Freddy ameweka rekodi hiyo akiwa Zambia ya kuchukua tuzo ya ufungaji bora huku akiichezea timu ya Green Eagles katika michezo 16 pekee, japo licha ya kiwango hicho kizuri ila Simba imeachana naye baada ya kuhudumu kwa miezi yake sita tu.

SOMA NA HII  MUKWALA AKIRI KUWA NA DENI KUBWA SIMBA