Home news SIMBA MPYA YA MO DEWJI NI BALAA NA NUSU…ZAIDI YA BIL 27...

SIMBA MPYA YA MO DEWJI NI BALAA NA NUSU…ZAIDI YA BIL 27 KUTUMIKA KUJENGA UWANJA…

Habari za Simba

KATIKA mkutano mkuu wa mwaka wa Simba, Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji (maarufu kama Mo), alitoa ahadi kabambe kuhusu maendeleo ya klabu hiyo. Alitoa mipango ya kujenga miundombinu ya kisasa na madhubuti inayolenga kuibadilisha Simba kuwa klabu bora Afrika.

Pamoja na matarajio hayo makubwa, swali linalobaki ni je, Mo Dewji itamchukua muda gani kutekeleza ahadi zake ambazo kwa makadirio zinaweza kugharimu kati ya Dola 4.75 milioni hadi 10 milioni ambazo ni zaidi ya Sh12.9 bilioni hadi 27.2 bilioni. Na je, ni changamoto zipi zinazoweza kutokea wakati wa utekelezaji wake?

AHADI YAKE

Katika hotuba yake siku chache zilizopita, Mo Dewji alieleza malengo yake ya muda mrefu ndani ya Simba, akisisitiza kuwa lengo lake kubwa ni kuijenga Simba kuwa klabu inayoweza kushindana vilivyo katika michuano ya kimataifa, hasa Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika kufanikisha hilo, Mo aliahidi miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu.

Alisema mpango wa klabu ni kujenga miundombinu inayojumuisha kambi yenye viwanja vitano vya kisasa kwa ajili ya mazoezi, gym ya kisasa, hosteli ya wachezaji, eneo la chakula, makumbusho ya klabu na chuo cha kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana. Hiyo ni miundombinu muhimu kwa ajili ya kuiwezesha Simba kuwa na maendeleo endelevu, siyo tu kwenye soka la ndani, bali pia kimataifa.

Katika hotuba yake, Mo Dewji alisema: “Hizi ni ramani mpya za Simba Mo Arena. Tunatarajia kujenga kambi yenye gym, eneo zuri la wachezaji, sehemu ya chakula, viwanja vitano vya kisasa, makumbusho ya klabu na chuo (akademi) cha maendeleo ya vijana ili kukuza na kuendeleza vipaji.”

Kauli hiyo inaonyesha dhamira ya kuhakikisha kuwa Simba inakuwa na miundombinu bora zaidi ambayo itawezesha klabu hiyo kufikia malengo yake ya muda mrefu.

MCHAKATO WA MABADILIKO

Pia Mo alizungumzia mchakato wa mabadiliko wa Simba ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka saba sasa. Alisema klabu hiyo ipo katika hatua za mwisho za mabadiliko na ni muda mwafaka wa kujenga Simba mpya ambayo itakuwa na uwezo wa kushindana na klabu kubwa barani Afrika.

“Mchakato huu umechukua miaka saba na tumefikia mwisho. Tutajenga Simba yetu mpya. Tukishirikiana tutajenga Simba imara ambayo itashindana Afrika na hii ndio ndoto yetu. Shabaha yangu ni Simba kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Kauli hiyo pia ilionyesha kuwa lengo siyo tu kuiwezesha Simba kushinda mashindano ya ndani, bali kufika mbali zaidi kwenye michuano ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika. Hii ni ndoto kubwa inayohitaji juhudi za pamoja na uwekezaji mkubwa wa kifedha.

Pamoja na kuzungumzia maendeleo ya miundombinu, aliwataka wana Simba kuacha migawanyiko na kuweka kipaumbele kwenye umoja wa klabu.

Aliwaasa wanachama kuacha fitna na kuelekeza nguvu kuijenga Simba mpya.“Naomba tuache fitna. Umoja ni nguvu. Kila anayejitolea kuongoza hatupaswi kumuangusha kwa maneno ya fitna. Mimi nipo nanyi, naomba tujenge Simba yetu.”

MAKADIRIO YA GHARAMA

Licha ya mipango hiyo kabambe, utekelezaji wa ahadi za Mo Dewji utahitaji gharama kubwa. Kwa mujibu wa makadirio ambayo gazeti la  Mwanaspoti limeyafanya kwa kushirikiana na wataalamu huenda tajiri huyo zikamtoka kati ya Sh12.9 bilioni hadi 27.2 bilioni kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya Simba.

Kuchambua miradi hiyo kwa undani, hii hapa picha ya gharama zinazoweza kutumika:

VIWANJA VITANO VYA MAZOEEZI

Mo Dewji aliahidi kujenga viwanja vitano vya kisasa kwa ajili ya mazoezi ya wachezaji. Viwanja hivyo vinatarajiwa kuwa na nyasi halisi au za bandia, mabomba ya mifereji ya maji, mfumo wa uzio na taa za usiku.

Kulingana na makadirio ya wastani, kila kiwanja kinaweza kugharimu kati ya Dola300,000 hadi 600,000 kutegemea na ukubwa wa uwanja na vifaa vitakavyotumika. Jumla ya gharama kwa viwanja vyote vitano inaweza kufikia kati ya Dola 1.5 milioni hadi milioni tatu.

HOSTELI YA KISASA

Mo Dewji pia aliahidi kujenga hosteli kubwa ya kisasa kwa ajili ya wachezaji wa Simba. Hosteli hiyo itakuwa na vyumba vya kulala, vifaa vya umeme na mawasiliano kama vile Wi-Fi na AC pamoja na huduma nyinginezo muhimu kama mifumo ya usalama na mabafu. Gharama za ujenzi wa hosteli inakadiriwa kuwa kati ya Dola 1.5 milioni hadi milioni tatu.

Makumbusho ya Klabu

Kwa lengo la kulinda historia na urithi wa Simba, Mo aliahidi kujenga jengo la makumbusho la kisasa. Makumbusho hayo yatakuwa na vifaa vya kisasa kama TV za kuonyesha video, mabango, picha na teknolojia ya kidijitali. Ujenzi wa makumbusho unaweza kugharimu kati ya Dola 500,000 hadi Dola 1 milioni kutegemea na ukubwa wa jengo na ubora wa teknolojia zinazotumika.

Gym Kubwa ya Kisasa

Gym ya kisasa kwa ajili ya wachezaji wa Simba pia ni sehemu ya mipango ya Mo. Gym hiyo itakuwa na vifaa vya mazoezi kama vile mashine za uzito na cardio, pamoja na huduma nyingine kama bafu na lockers. Ujenzi wa gym unakadiriwa kugharimu kati ya Dola 750,000 hadi milioni mbili.

Eneo Maalumu la Chakula

Eneo la chakula nalo ni sehemu muhimu ya kambi hiyo. Eneo hilo litatumika kuhudumia chakula kwa wachezaji na wafanyakazi wa Simba likiwa na vifaa kama vile meza, viti, majokofu na jiko la kisasa. Gharama za ujenzi wa eneo hilo zinakadiriwa kuwa kati ya Dola 500,000 hadi milioni moja.

GHARAMA ZA MIRADI

Kwa kujumlisha gharama za miradi yote iliyopendekezwa na Mo Dewji, jumla inaweza kufikia kati ya Dola 4.75 milioni hadi Dola 10 milioni. Hii ni sawa na kati ya Sh11.875 bilioni hadi Sh25 bilioni.

CHANGAMOTO

Licha ya ahadi hizi kabambe, utekelezaji wa miradi ya miundombinu unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo Mo Dewji na Simba SC wanapaswa kuzizingatia.

Gharama za ujenzi zinaweza kubadilika kutokana na hali ya soko la ujenzi, hali ya kiuchumi, upatikanaji wa vifaa na mfumuko wa bei unaoweza kusababisha ongezeko la gharama. Hivyomakadirio hayo yanaweza kuongezeka au kupungua.

Kuweka miundombinu ya kisasa ni hatua ya kwanza, lakini kuendesha na kudumisha miundombinu hiyo ni changamoto kubwa. Simba itahitaji kuwekeza katika uendeshaji endelevu wa viwanja, gym, hosteli na makumbusho ili kuhakikisha kuwa zinafanya kazi vizuri kwa muda mrefu. Hii itahitaji rasilimali zaidi za kifedha na usimamizi bora.

Mradi wa kujenga miundombinu kama viwanja, gym na hosteli unahitaji ardhi kubwa na bahati nzuri eneo la Bunju inalomiki klabu hiyo lina zaidi ya ekari 20, hivyo linaweza kutosha.

WASIKIE WADAU

Mhandisi ujenzi Johnson Oliver ambaye amehusika katika makadirio haya akiwa London, Uingereza kutokana na uzoefu wake anasema: “Hiyo ni miradi mikubwa sana. Nadhani Simba inaweza kuwa moja ya klabu za mfano Afrika, hivyo ni vitu ambavyo vimekuwa vikifanywa na klabu nyingi za Ulaya. Naamini kama kila kitu kitakwenda vizuri basi kitaiweka Simba na Tanzania katika ngazi nyingine.”

Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar, Gwambina na timu za vijana za Azam FC, Mohamed Badru ambaye amefanya kazi ya kuendeleza vijana kwa zaidi ya miaka 10 nchini Uingereza naye alikuwa na machache.

“Natamani kuona klabu nyingine nazo zikisimama na kuonyesha vile wanaweza kuwa sehemu ya mabadiliko na ukuaji wa soka la Tanzania, najua ni gharama kubwa kufanikisha hayo lakini ni hatua moja mbele,” anasema Badru.

TAKWIMU ZA MAKADIRIO

1. Viwanja Vitano vya Mazoezi

-Eneo la viwanja (ekari, ukubwa wa viwanja)

-Aina ya nyasi/uwekaji: Nyasi asilia au za bandia.

-Mfumo wa maji na mifereji.

-Mfumo wa uzio na taa za usiku.

-Vifaa vya michezo; Magoli, alama, na vyombo vingine vya mazoezi.

-Kuandaa eneo na ujenzi.

MAKADIRIO: Dola 300,000 – Dola 600,000 kwa kila kiwanja (inategemea ukubwa, aina ya nyasi, na vifaa).

2. Hosteli ya Kisasa

-Ukubwa wa majengo na vyumba.

-Samani na vifaa; Vitanda, makabati, meza, vifaa vya umeme.

-Huduma za kisasa; Wi-Fi, AC, mfumo wa usalama.

-Gharama za jengo, mabomba na umeme.

MAKADIRIO: Dola 1,500,000 – Dola 3,000,000 (inategemea ukubwa wa hosteli na ubora wa huduma).

3. Jengo la Makumbusho Kuhusu Timu

-Ubunifu wa ndani; Maonesho, makabati ya kuhifadhia vifaa vya kihistoria.

-Teknolojia; Vifaa vya kidigitali, maonyesho ya video, mifumo ya sauti.

-Samani na vifaa; Mabango, picha, TV za kuonyesha taarifa.

-Ujenzi wa jengo; Gharama ya ujenzi wa jengo na huduma za msingi.

MAKADIRIO: Dola 500,000 – Dola 1,000,000 (inategemea ukubwa na ubora wa teknolojia inayotumika).

4. Gym Kubwa ya Kisasa

-Vifaa vya mazoezi: Vifaa vya uzito, mashine za mazoezi ya cardio, nk.

-Jengo: Eneo la gym, saizi ya jengo.

-Huduma za ziada: Bafu, lockers, mfumo wa muziki na sauti, AC.

MAKADIRIO: Dola 750,000 – Dola 2,000,000 (kutegemea ukubwa na vifaa vya kisasa).

5. Eneo Maalum la Chakula

-Ukubwa wa eneo: Inategemea na idadi ya watu wanaotarajiwa kuhudumiwa, kwani inaweza kuwa ndogo au kubwa kulingana na mahitaji.

-Majengo na vifaa: Eneo la la chakula, meza na viti, jiko la kisasa, sehemu ya kutayarisha chakula, vifaa vya kuhifadhia chakula (majokofu) na sehemu za huduma.

-Huduma za kisasa: Vifaa vya usafi, mfumo wa uingizaji hewa (AC), na vifaa vya umeme kama vile microwave, mashine za kahawa na kadhalika.

-Usalama na usafi: Mfumo wa usalama wa chakula, vifaa vya kusafisha, na mfumo wa taka.

MAKADIRIO: Dola 500,000 – Dola 1,000,000 (inategemea ukubwa, vifaa vya kisasa, na ubora wa huduma zinazotolewa).

JUMLA YA MAKADIRIO:

-Viwanja 5 vya mazoezi: Dola 1,500,000 – Dola 3,000,000

-Hosteli ya kisasa: Dola 1,500,000 – Dola 3,000,000

-Jengo la makumbusho: Dola 500,000 – Dola 1,000,000

-Gym kubwa ya kisasa: Dola 750,000 – Dola 2,000,000

-Eneo maalum la chakula: Dola 500,000 – Dola 1,000,000

JUMLA YA GHARAMA ZOTE: Makadirio ya jumla ni kati ya Dola 4.75 milioni hadi Dola 10 milioni (sawa na TZS 11.875 bilioni hadi Sh25 bilioni).

Credit and C/P:- Gazeti la MwanaSpoti

SOMA NA HII  DAWA YA KIBU KUCHEZA KIKOSI CHA KWANZA SIMBA HII HAPA