NYOTA wawili wa kimataifa, Libasse Gueye na Khadim Diaw, wanatarajiwa kutua nchini muda wowote kuja kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusaini mikataba ya kuitumikia klabu ya Simba SC, ikiwa ni sehemu ya mipango ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo.
Katika dirisha dogo la usajili, Simba imekuwa ikifanya mambo yake kwa siri kubwa, ikilenga kuongeza ubora wa kikosi kuelekea mashindano muhimu yaliyopo mbele yao, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika na michuano mingine ya ndani.
Imeelezwa kuwa Libasse Gueye, anayekipiga katika nafasi ya kiungo mshambuliaji kutoka klabu ya Teungueth FC ya Senegal, yuko tayari kutua nchini muda wowote kwa ajili ya kukamilisha zoezi la usajili na kuungana rasmi na wekundu hao wa Msimbazi.
Chanzo cha kuaminika kimesema kuwa viongozi wa Simba wamehakikisha wanaboresha kikosi kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi.
“ Gueye akiwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakihitajiwa pia na klabu ya USM Alger, lakini Simba imefanikiwa kushinda mbio za kupata saini yake baada ya kufikia makubaliano na klabu pamoja na mchezaji,” amesema.
Ameongeza kuwa Gueye aliwahi kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Senegal katika michuano ya AFCON, aliibuka mchezaji bora wa mechi katika pambano dhidi ya Nigeria, jambo linaloonyesha ubora wake uwanjani.
Kwa upande wa Khadim Diaw, ambaye ni beki wa kushoto wa timu ya Taifa ya Mauritania, naye ni miongoni mwa usajili uliolengwa na Simba kwa lengo la kuimarisha safu ya ulinzi na kuongeza ushindani ndani ya kikosi.
Mtoa habari huyo amesisitiza kuwa usajili wote unaofanywa na Simba umezingatia mahitaji ya benchi la ufundi, huku lengo kuu likiwa ni kujenga kikosi imara kitakachoweza kushindana kwa mafanikio katika mashindano yote yanayowakabili msimu huu.