Home Uncategorized MASHUJAA WA USWAHILINI; SAMATTA, KIBA, TUWAUNGE MKONO NIA YAO NJEMA YA KUIRUDISHIA...

MASHUJAA WA USWAHILINI; SAMATTA, KIBA, TUWAUNGE MKONO NIA YAO NJEMA YA KUIRUDISHIA JAMII
*Twendeni Taifa Juni 2 tukawaunge mkono

Na Saleh Ally

VIJANA wawili wa Kitanzania, wameamua kukutana pamoja na kufanya kitu kwa ajili ya kurejesha katika jamii.


Mbwana Samatta anayekipiga katika kikosi cha mabingwa wa Ubelgiji, KRC Genk na Ally Saleh Kiba, maarufu kama Alikiba, msanii nyota wa muziki nchini na Afrika. Kiba pia ni mchezaji wa Coastal Union inayoshiriki Ligi Kuu Bara.


Wawili hawa kwa kushirikiana na baadhi ya marafiki zao, wamekubaliana kuchangisha fedha kupitia taasisi ya Samakiba Foundation kwa ajili ya kusaidia jamii.


Wanaisaidia jamii kwa kuelekeza misaada yao kwa watoto wenye matatizo na wale yatima. Wale walioshindwa kulipa ada lakini pia kusambaza vitabu mashuleni.


Wanakusanya fedha hizo na kutoa burudani ambayo italipiwa fedha kwa kiasi kidogo tu licha ya kwamba burudani hiyo itakuwa na thamani kubwa.


Nasema ina thamani kubwa kwa kuwa inawaunganisha watu wenye thamani kubwa kwa maana ya majina, nyota mbalimbali wa taifa letu.


Wao pia wamekubali kuungana na kucheza mechi ya burudani itakayopigwa Juni 2, mwaka huu pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Heshima kwa wachezaji na wasanii  wengine waliokubali kuungana na Kiba na Samatta kwa ajili ya mchezo huo ambao ninaamini utakuwa ni funzo kubwa kwetu.


Ukubwa wa Kiba na Samatta unatokana na Watanzania wenyewe, mapenzi yao kwa wawili hao ndio yamewafanya kuwa wakubwa ingawa tunapaswa kuwapongeza wao kwa kuendelea kufanya vizuri.


Leo Samatta na Kiba, nao wameona kuna kila sababu ya kurudisha kwa jamii yao kwa kucheza mechi ambayo itawakutanisha Watanzania kwa pamoja kwenye Uwanja wa Taifa.


Hii ni siku muhimu sana ambayo inaingia kwenye historia na inalenga kutengeneza upendo, ufahamu wa thamani ya uanadamu na kuwatambulisha wanadamu wanaopeana thamani.


Mmewapenda Samatta na Kiba, nao sasa wameamua kurejesha upendo kwenu. Hakika wangeweza kukaa kimya na kuendelea na shughuli zao lakini wameona usahihi ni kuungana nanyi na kufurahi.


Pamoja na furaha, bado fedha itakayopatikana katika burudani hiyo inakwenda kuisaidia jamii yenyewe. Hili ni jambo kubwa linalopaswa kupewa sapoti kutoka kwenu wananchi.


Waonyesheni Samatta na Kiba wanafanya jambo kubwa lenye upendo. Waonyesheni wengine ambao hawakuwahi kuwaza kwamba vijana hao wanapaswa kuungwa mkono na kuigwa na kikubwa, jitokezeni kwa wingi Juni 2 pale Uwanja wa Taifa.


Twendeni Uwanja wa Taifa kwa wingi tukawaunge mkono ili tuonyeshe tunaweza kuwaunga mkono wale wenye nia ya kuisaidia jamii yetu.


Tujitokeze kwa wingi na kufurahia pamoja ili Samatta na Kiba, waone hawakukosea na wanaweza kupambana kwa ajili ya jamii yao na wakaungwa mkono na jamii yenyewe.


Wote wawili ni vijana kutoka Uswahili, Samatta ni Mbagala na Kiba ni Kariakoo. Leo wanaonyesha upendo huu, ni jambo la kujivunia na kuwasogelea na kuwaunga mkono ili wafanye vizuri na siku zijazo wazidi kufanya vizuri na zaidi na kurejesha upendo.


Kuna maneno mengi sana kuhusiana na sisi vijana tuliozaliwa na kukulia Uswahilini. Huaminika hatuwezi kutoa msaada, hatukumbuki tulipotoka na tunajisahau na mafanikio madogo.


Kiba na Samatta wamekuwa tofauti na wanaonyesha mambo tofauti. Wametoka Uswahilini kweli, leo wanarejea Uswahilini wameijumuisha jamii yote ya Watanzania bila kujali imetokea wapi kuisaidia jamii ya Uswahilini.


Hakuna jingine ambalo unaweza kuweka mbele zaidi ya kusema kwa nia yao, uamuzi sahihi na wanachokifanya, kimoja tu wanastahili. Kuungwa mkono.Panapo majaaliwa, mimi nitakwenda kuwaunga mkono, nitakuwa Uwanja wa Taifa kuungana na Watanzania  wataokwenda hapo. Nakuomba nawe ungana nao pamoja nasi ili tuwe sisi tunaoungana nao.

SOMA NA HII  KAKOLANYA: SIMBA WENYEWE WATANIPENDA