Home Uncategorized NINJA APATA DILI ULAYA, ASAINI

NINJA APATA DILI ULAYA, ASAINI


WAKATI uongozi wa Klabu ya Yanga ukiendelea kumpigia simu beki wake wa kati, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ inaelezwa tayari mlinzi huyo ameshasaini mkataba wa miaka mitatu na mmoja kati ya timu zinashiriki Ligi Kuu ya Jamhuri ya Czech barani Ulaya.

Ninja amejiunga na klabu ya nchi hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu ambayo imepanga kumtoa kwa mkopo kwenda kucheza katika Ligi Kuu ya Marekani (MSL).

Taarifa za uhakika kutoka kwa mmoja wa marafiki wa mchezaji huyo zinasema kuwa, tayari beki huyo ameshamaliza kila kitu na timu yake mpya na kinachosubiriwa kwa sasa ni kupatikana kwa Visa ili aweze kuondoka nchini.

“Ukweli ni kwamba Ninja tayari ameshasaini katika klabu inayoshiriki ligi ya Jamhuri ya Czech, amesaini mkataba wa miaka mitatu na kuanzia sasa wakati wowote huenda akaondoka nchini.

“Unajua Yanga wameanza kumpigia simu kwa ajili ya kumpa mkataba lakini haitokuwa rahisi kuwezekana kwa sababu sasa anasubiria Visa kuondoka nchini ingawa yeye na uongozi wake hawataki kuweka wazi hadi kila kitu
kikamilike,” alisema mtoa taarifa.

Gazeti hili lilimtafuta beki huyo kwa njia ya simu ambapo alisema: “Mpaka sasa sijui chochote kwa sababu bado nipo kwetu (Jang’ombe, Zanzibar) kwa ajili ya mapumziko, hivyo naomba niachwe hadi hapo masuala ya mpira yakianza.” Upande wa uongozi wa Yanga haukuwa tayari kulitolea ufafanuzi suala hilo.

CHANZO: CHAMPIONI

SOMA NA HII  NI MSALA MWINGINE YANGA, SERIKALI YAMPIGA STOP BALAMA, SABABU ZATOLEWA