Home Uncategorized EXCLUSIVE: RASMI YANGA YAMUACHIA GADIEL SIMBA, WALIRUDISHA JEMBE

EXCLUSIVE: RASMI YANGA YAMUACHIA GADIEL SIMBA, WALIRUDISHA JEMBE


Uongozi wa Yanga umekubali yaishe na kumuachia beki wao wa pembeni, Gadiel Michael kutua Simba kwenye usajili wa msimu ujao baada ya kutofikia muafaka mzuri huku ikifanikisha mipango ya kumuongezea mkataba mpya beki wake, Haji Mwinyi.

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu zianze kuzagaa tetesi za Gadiel kusaini mkataba wa miaka mitatu wa kuichezea Simba baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Gadiel atakuwa mchezaji wa pili kutoka Yanga kujiunga na Simba kwa ajili ya msimu
ujao, mwingine ni kipa Beno Kakolanya ambaye tayari ametambulishwa.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Gadiel amegomea mkataba wa miaka miwili aliowekewa mezani wa shilingi milioni 50 akidai ni ndogo huku akiomba shilingi milioni 60.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, baada ya beki huyo kugomea mkataba huo kwa mara ya pili mfululizo, uongozi umechukua maamuzi ya haraka ya kuachana naye huku wakiwa kwenye taratibu za mwisho za kukamilisha mipango ya kumbakisha Mwinyi atakayesaidiana na Ally Mtoni ‘Sonso’.

Aliongeza kuwa, awali yalikuwepo majina matatu waliyokuwa wanayashindanisha ambayo ni Eric Rutanga anayekipiga Rayon Sports, Asante Kwasi aliyemaliza mkataba wake Simba, David Luhende wa Kagera Sugar kabla ya kumrudia Mwinyi kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

“Uongozi rasmi umeachana na mipango yake ya kumuongezea mkataba mwingine wa miaka miwili, ni baada ya kugomea kusaini mpya kwa mara ya pili mfululizo mara alipofuatwa na mabosi wa Yanga Misri ilipokuwa timu ya taifa, Taifa Stars.

“Mara ya pili ni hii ya juzi, mara baada ya mmoja wa mabosi wa Yanga aliyekwenda Misri kwenda kukamilisha usajili wa Sonso na Shikhalo (Farouk), yeye alikataa kusaini huku akiomba muda zaidi bila ya
kufahamu kuwa viongozi tayari wameshtukia kuwa anataka kusaini Simba.

“Hivyo, basi uongozi ulichofanya ni kama kwa Ajibu (Ibrahim) kuachana naye rasmi na kumtakia kila la heri huko aendako na badala yake haraka uongozi umetafuta mrithi wake na kufikia muafaka wa kumbakisha Mwinyi,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla kuzungumzia usajili alisema: “Usajili wetu umekamilika kwa asilimia kubwa kwa kuwasajili wachezaji wote ambao kocha Zahera amewapendekeza. “Kama ikitokea kuna uboreshaji wowote utakaohitajika katika timu kwa kuongeza mchezaji, basi haraka tutafanya.”

SOMA NA HII  KOCHA MBAO FC APIGA BONGE MOJA YA MKWARA