Home Uncategorized ZAHERA AJA NA MIKAKATI MIPYA KABAMBE YANGA, TIMU KUWEKA KAMBI MOROGORO

ZAHERA AJA NA MIKAKATI MIPYA KABAMBE YANGA, TIMU KUWEKA KAMBI MOROGORO


Wakati Yanga ikianza maandalizi ya msimu ujao kesho Jumapili, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera amekuja na mkakati mpya kuhakikisha timu hiyo haifungwi mabao mengi msimu ujao.

Yanga mpaka sasa imesajili wachezaji 13 wapya na leo Jumapili watakwenda mkoani Morogoro kuanza kambi ya pamoja kujiandaa na msimu mpya.

Zahera ambaye kwa sasa yuko mapumzikoni baada ya timu yake ya Taifa ya DR Congo kutolewa kwenye Kombe la Mataifa Afrika huku yeye akiwa kocha msaidizi, atajiunga na Yanga baadaye lakini tayari ameshatoa maelekezo kwa msaidizi wake, Noel Mwandila.

Chanzo kutoka ndani ya benchi la ufundi kimeliambia Championi Jumamosi kuwa, Zahera ameamua kufanya mabadiliko katika ufundishaji wake kwa kuja na mikakati ya kuhakikisha kila safu ya uchezaji ndani ya kikosi hicho inakuwa imara.

Taarifa zinasema, Zahera amepanga kuanza kuboresha safu yake ya ulinzi ambayo inaongozwa na Kelvin Yondani ambaye pia ameletewa majembe mengi mapya kikosini humo.

Wachezaji wengine ambao wanaunda safu hiyo ni Juma Abdul, Paul Godfrey ‘Boxer’, Andrew Vincent ‘Dante’, Lamine Moro (Ghana), Msatapha Suleimani (Burundi) na Ally Sonso.

“Keshokutwa tunaanza maandalizi yatu ya Ligi Kuu Bara msimu ujao na kesho (leo), baadhi ya wachezaji wetu wa kutoka nje ya nchi wataanza kuwasili nchini kwa ajili ya maandalizi hayo.

“Hivi karibuni niliongea naye ambapo mikakati yake amepanga kuanza kuimarisha kwanza safu ya ulinzi na baada ya hapo ataendelea na safu nyingine ikiwemo ile ya ushambuliaji.

“Kama mikakati hiyo itaenda kama ambavyo Zahera amepanga, naamini kabisa msimu ujao tutafanya vizuri sana.” Alipotafutwa Zahera kuzungumzia hilo, hakupatikana lakini Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten alisema: “Ni kweli Jumapili timu itaanza mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa ligi kuu lakini mambo mengine yote yanayohusiana na ufundi hayo anapaswa kuzungumziwa na kocha mwenyewe.”

SOMA NA HII  WINGA AS VITA: NIMEFANYA MAZUNGUMZO NA YANGA