Home Uncategorized CHONDE YANGA HAWA TOWNSHIP ROLLERS SI WATU WA KUBEZA HATA KIDOGO

CHONDE YANGA HAWA TOWNSHIP ROLLERS SI WATU WA KUBEZA HATA KIDOGO


NA SALEH ALLY
KESHO Yanga watakuwa kazini kuwawakilisha Wanayanga na Watanzania katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Township Rollers kutoka nchini Botswana.

Rollers si wageni hapa Tanzania, mara ya mwisho walicheza na Yanga katika michuano hiyohiyo na kuwatoa kwa jumla ya mabao 2-1. Pamoja na hivyo, Rollers walionyesha soka safi na la kuvutia na kutuacha Watanzania tukitafakari, kwamba itakuwaje katika mechi ya pili.

Kwamba kama Yanga wamelala nyumbani kwa mabao 2-1, huku Waswana hao wakitandaza soka la kiwango cha juu, kwao itakuwaje. Yanga walisafiri na kwenda kupata sare ya bila mabao huku wengi tukiamini kwamba mechi ilikuwa ngumu sana na wasingeiweza.


Wakati wanakutana na Yanga, Rollers walikuwa wamewashangaza wengi baada ya kuwang’oa katika Ligi ya Mabingwa Afrika moja ya vigogo kutoka Sudan, El Merreikh. Walishinda jumla ya mabao 4-2 baada ya ushindi wa mabao 3-0 kwao Botswana na kupoteza kwa 2-1 ugenini Khartoum.


Walipokutana na Yanga na kuwatoa kwa jumla ya mabao 2-1, wakavuka na kuingia hatua ya makundi ambako walikutana na vigogo Al Ahly na Esperance ambao walihitimisha safari yao. Mfano Al Ahly waliwafunga Rollers mechi zote mbili, mechi ya kwanza wakiwatwanga 3-0 Cairo halafu Gaborone, wakawapiga 1-0.

Katika mechi 30 ligi kuu, Rollers walifanikiwa kushinda 20, sare nane na kupoteza mara mbili. Mwisho wakajikusanyia pointi 68 na kubeba ubingwa, wakiwaacha kwa pointi mbili tu Jwaneng Galaxy waliopata 66 na kubaki katika nafasi ya pili.

Rollers si timu nyepesi lakini si kweli kwamba haifungiki, inawezekana kabisa lakini ni vizuri sana kuamini kwamba ni timu imara na inajitambua kwa maana ya kuwa na uongozi uliojipanga au unajua unachofanya.

Hivi karibuni, tumewaona Rollers wakiwa nchini Afrika Kusini kuweka kambi kwa ajili ya msimu mpya na walicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Simba na kutoka sare ya bao 1-1. Kwao ilikuwa na faida kwa kuwa wamecheza na timu ya Tanzania, watakuwa wamepata ladha ya Kitanzania, tayari kuwavaa Yanga.

Kwa Yanga, hawapaswi kuwabeza lakini hawapaswi kuhofia badala yake wajiandae kupambana na kushinda. Wanaokutana nao ni bora lakini ni lazima kuwapa presha kubwa ili kuwaondoa kwenye utulivu.

Kama Rollers watakuwa katika utulivu, kuna nafasi ndogo Yanga kufanya vizuri. Hivyo lazima mzigo wa presha utengenezwe kuanzia ndani ya uwanja kwa maana ya sehemu ya kuchezea hadi majukwaani.

Yanga wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu hiyo lakini Watanzania wengine wapenda mpira ambao wanaamini hata kama si mashabiki wa Yanga, watakuwa wazalendo kwenda tu uwanjani litakuwa jambo zuri.

Rollers wanataka presha hasa, wanatakiwa kutolewa katika utulivu ikiwezekana kushambuliwa mfululizo kwa kiwango kitakachowafanya wapoteane na kutoa nafasi ya Yanga kufunga angalau mabao matatu.


Yanga lazima ishinde mechi ya kwanza ili kumaliza mchezo. Kama itapata ushindi mnono Dar es Salaam, maana yake Rollers watarejea kwao na presha ambayo Yanga wataweza kuitumia kumaliza mchezo watakapokuwa ugenini.
Kunatakiwa kazi kubwa ya ziada ifanyike kuwazuia viungo wao mahiri kama Joel Mogorosi, Ivan Ntege, Tsepo Matete, Ofentse Nato au Segolane Boy, wengi ni wazuri wa pasi katika uchezeshaji lakini hata zile za mwisho. Hivyo ni rahisi kumaliza mchezo kiulaini na hasa ukiwapa nafasi ya kucheza.


Mwisho niwakumbushe, Yanga ni ya Tanzania na kwa kuwa sasa tuna timu nne katika michuano ya kimataifa, vizuri kuziunga mkono ili zisonge mbele na kututengenezea dira mpya ya mwenendo wa mpira wetu.
SOMA NA HII  KISSU ATAFUTIWA MBADALA WAKE NDANI YA AZAM FC