Home Uncategorized LIGI NDIYO INAANZA, KUNA MENGI YA KUJIFUNZA

LIGI NDIYO INAANZA, KUNA MENGI YA KUJIFUNZA


LIGI Kuu Bara msimu wa 2019/20 inatarajiwa kuanza wikiendi hii kwa baadhi ya timu kupambana kwenye viwanja tofauti baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii kuchezwa wikiendi iliyopita. Simba na Azam zilicheza mechi ya Ngao ya Jamii ambapo mchezo huo ulikuwa mzuri na wenye kuvutia, mwisho wa siku akapatikana mshindi.

Kila timu ilipambana kwa kadiri ambavyo iliona inawezekana na mwisho wa siku mshindi akapatikana ambaye ni Simba. Simba wanastahili pongezi kwa juhudi ambazo wamezionyesha, hii inamanisha kwamba ilijiandaa vema kukabiliana na wapinzani wao ambao nao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) msimu uliopita.

Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, walitumia makosa ya wapinzani wao kuwaadhibu na mwisho wa siku wakawa washindi, hivyo ndivyo ulivyo mchezo wa soka.

Kila kosa ndani ya uwanja kwa mpinzani ni faida kwa yule atakayetumia vema makosa hayo na kupata ushindi ambao ni nia ya kila timu.

Mchezo wa Ngao ya Jamii wa Simba na Azam kwa miaka ya hivi karibuni unaingia kwenye rekodi ya mechi bora zenye ushindani. Katika mechi 12 za Ngao ya Jamii, haijawahi kutokea mchezo ukakamilika kwa mabao mengi ndani ya dakika 90 kama ilivyokuwa katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba kushinda 4-2.

Mchezo ulikuwa ni wa uwazi kwa timu zote mbili na hakukuwa na makosa ambayo wengi tumezoea kuyaona yakitokea kwa timu kushindwa kujiamini. Hakukuwa na hofu kwa timu hata moja, sio Simba wala Azam, wote waliingia uwanjani vifua mbele wakihitaji jambo moja tu, kushinda na kutwaa Ngao ya Jamii. Kila mmoja alikuwa ana hesabu zake kichwani na ndio maana kila timu ilikuwa inafunguka na kushambulia mwanzo mwisho.

Azam FC walianza kwa kasi kipindi cha kwanza na waliendelea kwa muda kabla ya kupoteza umakini kidogo kila wanapofika eneo la hatari la Simba. Hapo pana tatizo kidogo ambalo linapaswa lifanyiwe kazi kabla ya mechi yao ya kimataifa ya marudiano dhidi ya Fasil Kenema ya Ethiopia. Sasa ni wakati wa Benchi la Ufundi la Azam kufanyia kazi yale makosa ambayo yameigharimu timu na kupoteza mchezo wao dhidi ya Simba.

Ni ukweli usiopingika kwamba Azam walikuwa kwenye ubora isipokuwa umakini wa washambuliaji kumalizia nafasi walizotengeneza ulikosekana, lakini pia safu yao ya ulinzi na kiungo ilizidiwa ujanja. Simba kilichowabeba ni uzoefu wao pamoja na kuwa na wachezaji ambao wamekomaa kwa kucheza michezo mingi migumu na ya ushindani.

Kazi kubwa ambayo imefanywa na safu ya kiungo ya Simba imeleta matokeo chanya na yamepeleka furaha Mtaa wa Msimbazi. Ubora wa mchezo unapaswa uendelee kuonekana kwa kuboreshwa zaidi ya pale ambapo wachezaji wamecheza kwani kazi ya mchezaji ni kuhakikisha analinda kiwango chake kila iitwapo leo.

Wachezaji wengine ambao wamepata nafasi ya kuona namna mchezo ulivyokuwa iwape hasira ya kufanya vema kwenye michezo yao inayofuata na kurekebisha makosa waliyoyaona.

Mashabiki wa timu zote wanapenda kuona timu zikicheza kwa kuonyesha ubora na uwezo halisi huku wakipata mabao ambayo hayana utata. Kikubwa kinachotakiwa ni kujipanga kwa kila mchezo bila kujali ni aina gani ya mchezo ambao timu itacheza. Pongezi pia kwa mashabiki ambao walijitokeza kushuhudia burudani, tumeona vitendo vya kiungwana ambavyo vinaendelea kwa sasa.

Kitu kizuri ni kwamba tayari muunganiko umeanza kuonekana na mashabiki wameachana na utamaduni huo wa kizamani. Ni muda wa kuzikana tabia ambazo hazina manufaa kwa mashabiki bali kufanya mchezo uwe sehemu ya burudani na utani kiasi.

Pongezi pia kwa Shirikisho la Soka Tanzana (TFF) kwa kusimamia mchezo kwa usawa na kuupa matangazo ya kutosha. Isiishie kwenye michezo ya Simba na Azam pekee bali iwe kwa timu zote hasa ukizingatia kwamba ligi inatarajiwa kuanza kutimu vumbi hivi karibuni.

Kwa kila mchezo uchukuliwe uzito mkubwa ili kuongeza hamasa na kurejesha mpira mikononi mwa mashabiki siku zote. TFF isisahau kwamba ligi inakaribia kuanza huku suala la mdhamini na mpangilio wa ratiba ukiwa bado upo hewani, mbali na haya kuna masuala mengi yaliyopita msimu ulioisha yanatakiwa yafanyiwe kazi.

SOMA NA HII  CHAMA NI MWENDO WA MATIZI TU, AKOSA MECHI MBILI BONGO