Home Uncategorized UAMUZI KESI YA KABURU, AVEVA YAIVA

UAMUZI KESI YA KABURU, AVEVA YAIVA


HATIMAYE kesi inayowakabili waliokuwa viongozi wa Simba, Evans Aveva na wenzake, inatolewa uamuzi Septemba 17, kama wana kesi ya kujibu au la na upande wa serikali jana ulifunga ushahidi.

Kesi hiyo inawakabili aliyekuwa Rais wa Simba, Evans Aveva, makamu wake Godfrey Nyange na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zachariah Hans Pope.

Katika kesi hiyo, mashahidi wapatao 10 wametoa ushahidi wao kwa nyakati tofauti mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar.

Shahidi namba tisa na namba 10 walitoa ushahidi wao mbele ya mahakama jana katika kesi hiyo ambayo inaongozwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Shahidi namba tisa, E9955 Detective Sergeant (DT), Faustine Emmanuel Mashauri ambaye anatoka katika Maabara ya Uchunguzi wa Maandishi ya Polisi Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Aliieleza mahakama kuwa, Septemba 4, 2017 akiwa kwenye maabara ya uchunguzi alipokea bahasha iliyofungwa ikitokea kwa Mkurugenzi wa Takukuru na kukuta kuna vielelezo pamoja na barua ya maombi ya uchunguzi. Vielelezo hivyo ilikuwa ni pamoja na hundi ya CRDB, fomu ya kuhamisha fedha kutoka CRDB kwenda benki nyingine pamoja na sahihi na majina.

Shahidi aliiambia mahakama kuwa alianza uchunguzi na aligundua kuwa zile sahihi zilifanana kabisa na wahusika ambao ni Nyange na Aveva na akaandika ripoti na kuirudisha Takukuru.

Kwa upande wa shahidi namba 10, Ledson Gideon Kasulwa kutoka Kampuni ya WAFEM Tanzania Ltd ambaye anadili na mizigo kutoka nje kupitia Bandarini alisema Simba ilikuwa ni mteja wake na ilimpa ombi la kutolewa nyasi zao bandia bandarini na ambaye alileta nyaraka za kutolea mzigo aliagizwa na Aveva.

Baada ya ushahidi huo, Hakimu Simba alisema kuwa kesi hiyo itatolewa maamuzi na kufahamu kama washitaki wanakesi ya kujibu au la Septemba 17.

SOMA NA HII  MGOMBEA SIMBA APEWA MILIONI