Home Uncategorized TAZAMA MSIMAMO WA LIGI KUU BARA, UTAELEWA MAANA YA TIMU ZA MAJESHI

TAZAMA MSIMAMO WA LIGI KUU BARA, UTAELEWA MAANA YA TIMU ZA MAJESHI




NA SALEH ALLY
MECHI zilizobaki katika Ligi Kuu Bara ni nane hadi tisa ambazo ndio nyingi sana. Wakati timu nyingine zilitarajia kucheza jana, unaona kuna funzo ndani ya msimamo huo.

Funzo hilo ni namna timu zilivyojipanga na namna ambavyo unaweza kujifunza jambo kulingana na timu zinazoshiriki ligi hiyo na mimi, ninaweza kusema angalia timu za jeshi na nyingi zinazomilikiwa na mashirika au watu binafsi.

Timu hizo tayari zimejitenga katika makundi matatu ndani ya ligi hiyo na makundi yote yanazungumza lugha tofauti ambazo zinaweza kukupa funzo.

Funzo hilo linaweza kuwa kwa ajili ya msimu huu na mambo yakabadilika msimu ujao au yalikuwa tofauti msimu uliopita lakini uhalisia unasema hivi, utajifunza jambo.

Ukiangalia timu ya kwanza hadi ya mwisho, utaona kuna timu tatu za juu kutoka jijini Dar es Salaam ambazo ni Simba, Azam FC na Yanga. 

Mbili zinazofuatia ni timu za mikoani ambazo wenyewe wanaonyesha wako makini, hapa ni Namungo FC kutoka Lindi na Coastal Union ya Tanga.

Baada ya hapo ni kundi la pili, timu ya sita hadi ya 12 ambazo zote zimevuka pointi 35, timu ya chini ni KMC ambayo ina pointi 36.

Humu kuna timu za mikoa lakini inaonekana timu za majeshi ndio zimesimama vizuri zaidi kuanzia nafasi ya sita, saba na nane, zote ni timu za majeshi ukianza na JKT Tanzania halafu Polisi Tanzania, zote zina pointi 46 kila moja, Tanzania Prisons ina pointi 41. 

Baada ya hapo ni timu za mikoani ambazo ni Kagera Sugar yenye pointi 41 na Biashara United ya Mara yenye pointi 40. Halafu 11 ni timu ya jeshi pia, Ruvu Shooting, yenye alama 40 na nafasi ya 12 inafungwa na KMC ya Manispaa ya Kinondoni, Dar yenye pointi 36.

Kuanzia namba 13 hadi 20, timu zote zina hofu kubwa ya kuteremka daraja, kwa kuwa nyingi zina pointi kuanzia 33 kushuka chini. Singida United wenye pointi 15 ambao kama watabaki Ligi Kuu Bara msimu huu, basi ni muujiza mwingine.

Unajifunza nini? Kwamba timu chache za mikoani ndio zimepata nafasi ya kuwa kati ya timu zilizo katikati ya msimamo wa ligi na maana yake ziko makini au siriaz.

Ndio maana unaona hata KMC baada ya kuona hawakuwa makini, wamebadilika kabisa na sasa unaona mwendo wao, huenda wakapanda hata nafasi za juu kama watandelea hivi katika mechi zilizobaki.

Kwa timu za majeshi kuwa katikati ya msimamo, maana yake ziko makini, zinafanya kazi zao kwa mpangilio, kama ni mpira vitu vinapelekwa kwa mpangilio na wamekuwa wapinzani wakubwa wa timu zilizo katika kundi la kwanza la timu sita, wale vigogo.

Hii maana yake tukubali, umakini wa timu za jeshi huenda kama ungekuwa katika timu nyingine za mikoani ambazo ni za mashirika au wananchi tu, basi hatua ingekuwa kubwa sana.

Tukubali timu za majeshi, zina wachezaji wake wa kawaida, wasiosajiliwa kwa fedha nyingi sana wala kulipwa mishahara mikubwa sana lakini wanachapa kazi yao kwelikweli na wanaongeza utamu wa ligi.

Inawezekana kuna sehemu wanakosea lakini lazima tukubali kuwa wamekuwa sehemu ya mabadiliko na mwendo mzuri ndani ya Ligi Kuu Bara na ndio maana ligi imefikia ukingoni.

Hawana hata mmoja wenye hofu kubwa ya kuteremka daraja na bahati mbaya ni moja tu, huwa hawana timu inayowania ubingwa karibia kila msimu. Sijui kwa nini!
SOMA NA HII  JESHI LA YANGA LITAKALOANZA LEO DHIDI YA POLISI TANZANIA