Home Uncategorized HASSAN KESSY KAMA KICHUYA TU MSIMBAZI..!!

HASSAN KESSY KAMA KICHUYA TU MSIMBAZI..!!

NYOTA wa Nkana FC ya Zambia, Hassan Kessy ni miongoni mwa wachezaji watakaokipiga katika kikosi cha Yanga msimu wa 2020/21, huku ikielezwa anafuata nyayo za kile kilichotokea kwa winga wa Simba, Shiza Kichuya.

Kessy alijiunga na Nkana mwaka 2018 kwa mkataba wa miaka miwili utakaofika ukingoni mwishoni mwa msimu huu, huku tayari mazungumzo ya nyota huyo kurejea mitaa ya Jangwani msimu ujao, yakiwa yameshafanyika.

Kama iliyokuwa kwa Kichuya kipindi aliposajiliwa na timu ya Pharco ya Ligi Daraja la Pili kisha kutolewa kwa mkopo ENPPI ya Ligi Kuu Misri, alionekana kuwa na kiwango kizuri kabla ya kuporomoka na kuvunjiwa mkataba wake kisha kurejea Tanzania kujiunga na Simba kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huu.

Taarifa mabazo gazeti la BINGWA limezipata, kilichomkuta Kichuya ndicho ambacho kinatokea kwa Kessy.

Kessy baada ya kujiunga na Nkana, alionekana kuwa na kiwango bora na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza, lakini baada ya msimu mmoja, aliporomoka kiasi cha kuondolewa katika timu.

“Kessy alitemwa kabisa katika kikosi cha Nkana, lakini wakala wake anayeishia Dar es Salaam, alilazimika kwenda Zambia kuzungumza na mabosi wa timu hiyo ili aweze kumaliza mkataba kwa sababu katika mkataba walioingia naye, una kipengele kinachoeleza kuwa mchezaji akiwa chini ya kiwango amejifukuzisha mwenyewe,” alisema.

Mtoa habari huyo aliongeza wakati Nkana wakisubiri mabadiliko ya Kessy, ndilo lilipotokea janga la virus vya corrona vilivyosababisha kusimama kwa ligi na Kessy kurejea Tanzania kabla ya mipaka kufungwa.

“Hivi sasa Kessy amekubali kuvunjwa kwa mkataba wake na Nkana, huku akifanya mazungumzo ya kurudi Yanga, nao kwa sababu aliondoka vizuri, wamekubali kumpokea, hivyo msimu ujao atakuwa Jangwani.”

Baada ya gazeti la BINGWA kupata taarifa hizo, lilimtafuta Kessy, lakini hakupatikana, huku Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Simon Patrick, akikiri: “Kessy alikuwa mchezaji wetu na alifanya kazi nzuri, kama atatakiwa kurudi, tutampa nafasi kwa sababu wachezaji wetu wengi wanaoondoka vizuri hatujawahi kuwakatalia kurudi.”

SOMA NA HII  VIDEO; MABAO YA DAVID MOLINGA NA SIBOMANA MBELE YA MBAO FC IKIWAPIGA 2-0