Home Uncategorized YANGA YAPANGUA FITNA

YANGA YAPANGUA FITNA


Yanga wameamua. Wameanzisha kampeni maalum ya kuujaza Uwanja wa Taifa na kuwadhibiti wenzao wa Simba ambao wamepanga kuisapoti Zesco United ya Zambia katika mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga wamesisitiza kwamba watajaza sehemu zote muhimu za jukwaa kuu upande wao na ule wa Simba kuanzia saa mbili asubuhi Jumamosi ya Septemba 14, ili kuhakikisha wachezaji wao hawavurugwi na kelele za Mnyama.

Simba wakiongozwa na msemaji wao wa klabu, Haji Manara wamekuwa wakihamasishana kwenye mitandao ya kijamii kuisapoti Zesco ya Kocha George Lwandamina kutokana na Yanga kuwazomea kwenye mechi ya UD Songo na wakatolewa kwenye Uwanja wa Taifa.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alisema wameweka mikakati thabiti ya kuzuia fi tna kwa kuhakikisha wanaujaza uwanja huo na mpaka sasa wana uhakika wa mashabiki 30,000 kupitia makadirio ya matawi yao mbalimbali na vikundi vya uhamasishaji.

“Tunafahamu mipango yao yote wanayoendelea nayo watani wetu na kama viongozi tayari tumechukua tahadhari ya haraka kuhakikisha tunapangua fi tna na hujuma wanazoendelea kuzifanya.

“Uongozi tayari umekutana na viongozi wa matawi na kufanya nao kikao na kikubwa ni kuweka mikakati ya mchezo wetu dhidi ya Zesco, hivyo tumewataka viongozi hao kwenda kuwahamasisha wanachama wao ili wajitokeze kwa wingi uwanjani kuanzia saa mbili kamili asubuhi wakiwa wamevalia jezi zao zenye rangi ya kijani na njano watakaoanza kukaa kwenye majukwaa ya Simba.

“Katika hilo ninaamini tutafanikiwa. Mashabiki wa Simba hawawezi kutuzidi Yanga na lengo kubwa ni kuona tunapata matokeo mazuri ya ushindi hapa nyumbani kabla kwenda kwao Zambia kurudiana nao,” alisema Mwakalebela.

Spoti Xtra, lilimtafuta Mhamasishaji wa Matawi ya jijini Dar es Salaam, Abbas Abeid maarufu kwa jina la Abbas Manzese wa Tawi la Manzesse alisema kuwa: “Niwape tahadhari mashabiki wa Simba waliopanga kuja uwanjani kuisapoti Zesco, hawatapata nafasi hiyo siku hiyo.”

“Tumekutana na viongozi wa timu akiwemo mwenyekiti wetu, Msolla (Mshindo) na mengi tumejadili ikiwemo mikakati ya kuzuia watani wetu wasipate nafasi ya kujazana uwanjani kuishangilia Zesco. “Tumewaandaa watu kutoka kwenye kila tawi hapa nchini watakaohakikisha mashabiki wa Simba hawapati nafasi ya kutamba siku hiyo, ili ukae jukwaani ni lazima uwe na jezi ya Yanga.

“Tunataka kuona majukwaani kukiwa na rangi za kijani na njano pekee na siyo nyekundu, tumeandaa operesheni maalum ya jaza uwanja, mashabiki wetu tunawaomba kuingia uwanjani kuanzia saa mbili asubuhi kama tulivyokubaliana na viongozi wetu katika chetu tulichokaa,” alisema Abbas.

MAYAY AWAITA SIMBA

STAA wa zamani Yanga, Ally Mayay ameunga mkono kitendo cha Simba kutishia kuivuruga Yanga kwenye mechi hiyo .

“Naungana na Manara kwa kauli yake sababu italeta motisha ya mashabiki watakaoenda kwa wingi uwanjani hata kama hawaendi kuishangilia Yanga.

“Moja ya faida kubwa kwa Manara ni mtu mwenye hamasa ambaye atasaidia pia Yanga kuwapa mapato sababu watakuwa wenyeji wa mechi, hivyo naungana naye kwa asilimia mia moja na namsapoti kwa alichokisema.

“Utani wa jadi kwa timu kama Simba na Yanga ni jambo la kawaida kabisa, ukienda hata Misri kuna timu za Al Ahly na Zamalek ambazo zimekuwa na utamaduni wa kutopeana sapoti pale mmoja anapocheza dhidi ya mwingine,” alisema Mayay.

YANGA KANDA YA ZIWA

Katibu Mkuu wa Yanga, mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mhando Madega amesema kuna kamati maalumu wameunda kwa ajili ya kuwakabili Simba na Zesco kwenye mechi hiyo na ndio maana wameomba timu ya Yanga iende Mwanza.

Alisisitiza kamati hiyo inaendelea na kazi zake na watakuwepo Taifa mapema kabisa kuhakikisha Yanga haipotezi mchezo huo. “Siwezi kukwambia mambo yetu ya ndani…ila amini kwamba kwa kazi itakayofanyika Mwanza Zesco hatoki kabisa Uwanja wa Taifa, wataumbuka na Simba wao.”

MASHABIKI KUMCHANGIA ZAHERA

Kundi kubwa la mashabiki wa Yanga jijini Dar, kuanzia juzi jioni lilikutana na kupanga mikakati ya kumchangia kocha wao, Mwinyi Zahera faini ya TFF ya Sh 500,000. Zahera alipigwa faini hiyo kutokana na kuvaa pensi uwanjani na kukaa kwenye benchi kinyume na kanuni mpya za TFF ambazo zinawataka makocha kuvaa mavazi nadhifu wakiwa kwenye benchi lao.

Hata hivyo Zahera alipozungumza na Spoti Xtra alisema, amekubali kulipa faini ya Sh 500, 000 huku akitamba kuwa sasa ataanza kutupia pamba za kufa mtu. “Nitawalipa faini hiyo ya Shilingi 500, 000 na kuanzia kwenye mechi zijazo nitaanza kuvaa wanavyotaka ili wafurahi.”

SOMA NA HII  WANA KINONDONI BOYS 'KMC' HAWALALI, WASAJILI MASHINE SABA MIAKA MITATU