Home Uncategorized LUC EYMAEL AANIKA MAPEMA KITAKACHOMUONDOA YANGA

LUC EYMAEL AANIKA MAPEMA KITAKACHOMUONDOA YANGA


KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael raia wa Ubelgiji ametangaza kwamba ataikimbia Ligi Kuu ya Tanzania Bara mapema kama wapinzani wao anaokutana nao wataendelea na staili ya kujiangusha na kupoteza muda ambayo kwake hajawahi kupendezwa nayo.

Kocha huyo ambaye ana wiki moja tangu alipotua nchini kuja kuziba nafasi ya Mkongomani Mwinyi Zahera amesema hatajali muda gani ambao atakaa ndani ya kikosi hicho lakini kama wapinzani anaokutana nao hawatabadilika na kucheza soka zuri, ataondoka na kuacha kufundisha.

Eymael ameweka bayana hilo baada ya kikosi chake kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Mbelgiji huyo ameliambia Championi Ijumaa kuwa ataacha kufundisha soka Tanzania na ataondoka mara moja kutokana na kutofurahiswa na aina hiyo ya uchezaji wa wapinzani wake ambapo anataka wacheze soka la kuvutia.

“Kama timu ambazo nitacheza nazo wataendelea kuanguka na kujilaza kwa ajili ya kupoteza muda nitaondoka na nitaacha kufundisha hapa Tanzania kwani ninapenda soka la kuburudisha.

“Wale tuliocheza nao (Kagera Sugar) kipa wao alikuwa anajiangusha bila hata sababu ya msingi, lakini hata wachezaji wao mimi sifurahishwi na hilo. Hata kama tunafungwa basi timu itawale na icheze soka zuri kama ambavyo sisi tunafanya na siyo vinginevyo,” alisema Eymael.

SOMA NA HII  IBRAHIM AJIBU ATOA LA MOYONI KWA YANGA