Home Uncategorized KOCHA MATATA YANGA AANIKA KINACHOMUUMIZA KICHWA

KOCHA MATATA YANGA AANIKA KINACHOMUUMIZA KICHWA


MOJA ya kitu kinachomuumiza kichwa Kocha wa Yanga, Luc Eymael ni namna ya kutengeneza kikosi bora chenye ushindani kitakachopata matokeo kwa kila mechi.

Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni Kocha huyo Mbelgiji alisema kuwa anahitaji kuimarisha kila kitu kuanzia nidhamu ya wachezaji na kuingiza mifumo yake itakayowapa matokeo mazuri katika mechi zao zilizobaki.

Alisema ametumia muda mwingi kuwasoma wapinzani wao wajao ili kujua ataingia na mbinu gani za kuwabana na kupata matokeo muhimu yakayowasaidia kutimiza malengo waliyojiwekea.

“Nimeshafahamu mashabiki wa Yanga wanataka nini, natengeneza kikosi chenye ushindani kitakachopigania matokeo mazuri kurudisha nguvu kwa watu kuja kwa wingi uwanjani na kuiunga mkono timu”alisema.

Kocha huyo alisema tayari ameshajua mapungufu yapi yaliyopo katika kikosi chake hasa katika safu ya ulinzi akiahidi kuyafanyia kazi kwa kila mchezo kutoruhusu kufungwa ovyo.

Safu ya ulinzi ya kikosi hicho imeruhusu kufungwa magoli 15 katika michezo 15 jambo linaloonyesha wazi kuna tatizo. Tangu ajiunge na timu hiyo ameiongoza Yanga katika michezo minne ambapo kati ya hiyo, ameshinda miwili dhidi ya Singida naTanzania Prisons na kufungwa miwili dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC.

Licha ya kupoteza michezo hiyo alisema hawatokata tamaa kuwania taji la ubingwa wa Ligi Kuu akiamini bado kuna michezo mingi iliyoko mbele yao. Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa.

Mabingwa hao wa kihistoria wanashika nafasi ya nne baada ya kucheza michezo 15, kushinda nane, sare nne, kupoteza michezo mitatu ikiwa na pointi 28
SOMA NA HII  NAMUNGO FC YAMALIZANA NA JEMBE LA KAZI KUTOKA KENYA