Home Uncategorized KUNA UMUHIMU WA HAKI KUTENDEKEA KWA UPANDE WA WAAMUZI WA BONGO

KUNA UMUHIMU WA HAKI KUTENDEKEA KWA UPANDE WA WAAMUZI WA BONGO

SIKU hizi vijiwe vyote mada ni moja tu, suala la waamuzi kuboronga kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, hakuna kingine.
Niko kwenye kijiwe kimoja cha kahawa hapa jijini Dar es Salaam, stori ni hizo hizo na swali hapa, je, nani atamfunga paka kengele?
Swali linakuwa zito, linakosa majibu, mmoja wetu anakuja na hoja ya kusema uovu huu si tuliulea wenyewe, acha utumalize.
Na unatumaliza kwelikweli na kama binadamu mwenye akili timamu anaamua kufanya maovu waziwazi tena mbele ya kamera, ujue tumefika pabaya.
Tusipoangalia inawezekana huu ndio ukawa mwisho wetu maana hali ni mbaya na lazima tulitafutie tiba kwa haraka.
Mbaya zaidi hivi sasa kila mtu ameshika upande wake, hakuna anayetaka kutenda haki au kuiangamiza timu yake.
Kuna pande mbili hapa za Simba na Yanga na kila mmoja anamnyooshea mwenzake kidole hakuna anayetaka kufuata ukweli zaidi ya kuongozwa na hisia.
Hilo ndilo baya sana na ndio litakalomaliza soka letu ingawa wenyewe tunakuwa wabishi.
Twende kwa waandishi wa habari ambao wanategemewa na jamii kuwalisha kilicho chema kabisa, nao wameingia kwenye huo mtego wa kuongozwa na hisia, yaani mapenzi na mahaba yamechukua nafasi kwao.
Hili ni tatizo tena kubwa, yaani hivi sasa mtu anaona mahaba yake na timu fulani ni muhimu kuliko kutenda haki.
Kwenye mitandao ya kijamii huko imekuwa ni vurugu tupu na baadhi ya waandishi wameamua kujianika kabisa kuwa wako upande gani na hadi mishipa inawatoka kutetea timu zao wanazozipenda kuliko kutenda haki.
Ndugu zangu tutende haki na mahaba tuyaweke kando ili kuisaidia jamii ambayo inataka kulishwa habari njema.
Jamii ya wapenda soka imepasuka na ipoipo tu inasubiri angalau wanahabari watende haki japo wapate pa kushikilia lakini nao wameingia kwenye huu mtego ambao ni mbaya.
Kwa ujumla hali ni mbaya na ni janga kubwa ambalo linahitaji matibabu makubwa ingawa wenyewe tunachukulia poa tu.
Wote tujue kuwa hii ni dhambi ambayo kama hatutajisafisha itakuja kutumaliza tena sio muda mrefu sana wote tutalaumiana kwa uzembe tulioufanya.
Tujue fika tuna kazi ya kufanya kuisaidia na kuiokoa jamii na tuweke kando mapenzi yetu.
Tukiendekeza haya mapenzi yetu, basi tutaupeleka sehemu mbaya sana mchezo wa soka kwa hapa nchini.
Nitoe pongezi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuliona jambo hilo kwani hivi karibuni rais wake, Wallace Karia, alitoa agizo la viongozi wa Bodi ya Ligi na wale wa TFF kukutana kulijadili.
Wakati Rais Wallace Karia akisema hivyo, Serikali nayo kupitia kwa wizara yenye dhamana ya michezo nayo ikapigilia msumari wa kutaka malalamiko yaliyopo juu ya waamuzi yafanyiwe kazi haraka iwezekanavyo.
Tumeona Kamati ya Saa 72 ya TFF ilitoa adhabu ya kumfungia miaka mitatu mwamuzi namba mbili aliyechezesha mechi ya Simba na Namungo ambaye alilikubali bao la Meddie Kagere wa Simba.
Hapo nyuma tayari kuna mwamuzi alipewa onyo kali. Ni jambo zuri kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kuondoa tatizo hili.
SOMA NA HII  MBABE WA YANGA CAFCC AJIUZULU