Home Uncategorized AHADI ZA FEDHA KWA WACHEZAJI YANGA VS SIMBA NI KUONYESHA TUMEPITWA NA...

AHADI ZA FEDHA KWA WACHEZAJI YANGA VS SIMBA NI KUONYESHA TUMEPITWA NA WAKATI

NA SALEH ALLY
WAPENDA soka lazima watakwenda Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakiwa na mambo mengi kichwani tayari kuishuhudia mechi ya watani wa jadi Yanga watakaokuwa wenyeji wakiwakaribisha Simba keshokutwa Jumapili.
Bila shaka itakuwa mechi nyingine ambayo inajitegemea kama ambavyo zimekuwa mechi nyingi za watani wa jadi wanapokutana.
Haiwezi kufanana na mechi nyingine kwa kuwa kila mechi ya watani inakuwa na sababu zake za kupatikana au kufanyika.
Katika mechi ya keshokutwa, Yanga watakwenda uwanjani kikubwa zaidi wanakitaka ni heshima na kidogo kujaribu kuikamata Simba, jambo ambalo kiuhalisia linaweza kuwa na wepesi tu kama Simba watakuwa si makini katika mechi zao zilizobaki za Ligi Kuu Bara.
Ndio maana nikasema, Yanga watataka heshima lakini pili ni kuthibitisha kwamba ile sare ya mabao 2-2 baada ya tambo nyingi za Simba, kwao haikuwa ya kubahatisha.
Hayo ni mawazo ya tambo za soka lakini hebu tujadili kuhusiana na hizi ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa kila unapofikia mchezo wa watani wa jadi.
Umesikia wewe mwenyewe kuwa klabu moja imewaahidi wachezaji wake kiasi fulani cha fedha kama wakiifunga Yanga au Yanga wakiifunga Simba.
Viongozi wanalazimika kuweka dau mezani ili wachezaji wacheze vizuri na kuhakikisha wanapata ushindi, binafsi naona ni jambo la kufedhehesha mpira wenyewe na hili linatubakiza nyuma sana sisi katika mchezo wa soka.
Wachezaji wanaijua kazi yao, wanatambua wajibu wa kuifunga Simba au Yanga na wanajua umuhimu wa ushindi ndio maana hufanya mazoezi kwa juhudi kubwa, husikiliza maelekezo ya mwalimu kwa usikivu wa juu ili kuhakikisha wanafanikisha ushindi.
Juhudi zao pamoja na kujua watapata pointi tatu ambazo ni muhimu lakini wanajua namna inavyokuwa heshima kushinda dhidi ya mtani wao kwa kuwa mashabiki ambao huwaunga mkono wanahitaji ushindi huo kwa nguvu zote na lazima kuwafurahisha.
 Angalia, wakati unawafurahisha watu unaotegemea wakuunge mkono, wakati huohuo unapata pointi zako muhimu ambazo zinaifanya kazi yako kuwa imetukuka. Sasa kuna haja gani ya kuongezewa dau la fedha ili uifanye kazi yako kwa ufasaha?
Binafsi huwa sioni ni jambo sahihi na wakati mwingine tunapaswa kwenda na wakati na kujifunza kutengeneza wachezaji wanaojitambua kwa kuwaacha wafanye kazi yao kwa weledi na viongozi wafanye yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawalipa fedha zao kwa maana ya posho na mishahara kwa wakati.
Tunaweza tukawa tunaona jambo hili ni dogo kwa kuwa tu ushabiki umewazidi wengi nguvu lakini hili jambo ni ugonjwa mkubwa sana ambao huenda tiba yake inaweza ikachukua muda mrefu sana kupatikana.
Wachezaji wanapaswa kulipwa vizuri na kupata kila kinachostahili ili wafanye vizuri. Wakati mwingine klabu zinalazimika kuwa watumwa kwa kuomba fedha kwa wafadhili ambao wakati mwingine nao wanakuwa na masharti yao baadaye, jambo ambalo si sawa.
Klabu zinalazimika kuwa watumwa kwa kuwa zinahitaji fedha za “kuwanunua” wachezaji wake ili waweze kuifanya kazi yao vizuri ya kumfunga mtani kwa kuwa kama watapoteza viongozi watakuwa katika wakati mgumu na hawaitaki hiyo presha.
Mikataba ya wachezaji na klabu haionyeshi hilo kwamba lazima wapewe fedha ndio wacheze vizuri dhidi ya Yanga au Simba. Kuendelea hivi ni kuendelea kutengeneza furaha ya kipindi hiki tu lakini uhalisia, tunatengeneza bomu kwa muda mrefu sana na kuna siku litakuwa tatizo kubwa ambalo kulimaliza kutahitaji nguvu nyingi sana.
 Mfano, klabu imeahidi Sh milioni 150 kwa wachezaji waifunge Yanga au Simba, kwa nini fedha hizo zisingetumika kutengeneza uwanja au kuwakuza vijana kwa kuwanunulia vifaa sahihi wachezaji wa vijana au ziwe mishahara au posho za wachezaji wa timu za vijana na wanawake kwa muda wa miezi mitatu, minne kuliko iishe siku moja kwa kuwalipa wale ambao walishalipwa kwa mujibu wa mkataba!

Nawakumbusha, tuliache hili kwa kuwa kuendelea kulifanya ni kufanya mambo ya leo tu bila ya kuangalia kesho ya mpira itakuwaje.
SOMA NA HII  SIMBA WAANZA KUIVUTIA KASI MBEYA CITY LEOLEO