Home Uncategorized CORONA IMEZUIA SHEREHE YA NDOA YANGU

CORONA IMEZUIA SHEREHE YA NDOA YANGU

NA LUC EYMAEL
KATIKA gazeti la Championi jana nilizungumzia mambo kadhaa kuhusiana na mpira wa Tanzania nikjaribu kulinganisha mambo kadhaa kutokana na uzoefu wangu katika soka la Afrika.

Yako ambayo yanafanana kama nilivyotoa mfano kati ya DR Congo na Gabon ambayo ni sawa na hapa, mfano kukosa hata vyumba bora vya kubadilishia nguo. Kama ambavyo nilieleza vyumba kwenye Uwanja wa Namungo, ombi lilikuwa ni kufanya mabadiliko kwa kulenga kuusaidia mpira wa Tanzania.

Tunaweza kuusaidia mpira wa Tanzania kwa kufanya mambo kwa vitendo lakini kwa kuelezana ukweli. Ndio maana nimeona ni sahihi kuelezea hayo nikiamini wahusika watayachukulia chanya na kuusaidia mpira wa Tanzania ambao hauwezi kusema unajengwa na timu ya taifa tu, unasaidiwa kwa njia nyingi na makocha wa klabu zote wanahusika sana kwa kuwa wao ndio hutoa wachezaji wa timu za taifa.

Tanzania kwa sasa imecheza Afcon, hili ni jambo kubwa sana na si la kulichukulia kawaida. Pamoja na hivyo unaona timu iliishia katika hatua za awali kabisa na sasa Tanzania inapaswa kufikiria mambo mawili, kwanza kufuzu tena lakini ikifanikiwa kuhakikisha inasonga katika hatua za mtoano jambo ambalo linahitaji maandalizi ya muda mrefu.

Leo nitazungumzia kuhusiana na suala la kwa nini nimeamua kuoa, jambo ambalo huenda bado halijawekwa vizuri na watu wanaweza kuwa wanashangaa kwa kuwa wanasikia tu, hapa Championi naweza kuwa na nafasi zaidi ya kuelezea.


Nimeamua kuoa Jumamosi ya Machi 28, huyu atakuwa mke wangu wa tatu baada ya kuwa nimeoa wengine wawili na tuliachana kwa sababu mbalimbali kama ambavyo imewahi kuwatokea wengine.

Kwa nini naoa? Ni kawaida tu kama mwanadamu kwa kuwa niko mwenyewe, nahitaji kuwa na mwenzangu na hili ni jambo la kawaida kabisa.

Kabla nilipata watoto wawili, mkubwa na umri wa miaka 33 na nina wajukuu wawili. Mimi ni mtu mzima sasa, ni babu wa wajukuu.

Nakumbuka nilizungumza na uongozi niondoke wakati wa mapumziko katika ratiba ya Fifa ambako kungekuwa na mechi za timu ya taifa. Lakini mambo yalikuja kubadilika kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona, unajua nchini kwangu Ubelgiji ni moja ya sehemu ugonjwa huo upo, si kama hapa.

Kwa kuwa tayari tulikuwa na ratiba ya harusi na watu wamejipanga, niliwasisitizia kwamba nitakwenda tu ili kufanikisha na kushughulikia mambo yote. Hivyo tumepanga harusi ifanyike kama ilivyopangwa lakini haitakuwa na sherehe kutokana na hali hii ya masuala ya Corona.

 Tutakwenda kanisani kukamilisha mambo yetu na kila kitu baada ya hapo shughuli itakuwa imeisha. Sitakaa muda mrefu baada ya hapo nimepanga kurejea Tanzania na kuendelea na kazi na ninaamini kila kitu kitakuwa kimerejea katika hali yake.

 Hivyo hii ni sababu ya mimi kuamua kuoa tena na baada ya hapo akili itakuwa ni kuhakikisha Yanga inaendelea kuimarika na matumaini yangu makubwa ni kumaliza katika nafasi ya pili na baada ya hapo msimu ujao ni kupambana kuhakikisha tunakuwa mabingwa.

 Watu wengi huenda wanaweza kuona ni kama uoga lakini napenda kuwa mkweli kwa kuwa unapoamua kusema ukweli kunakuwa na kazi nyepesi kidogo katika kurekebisha mambo kwa kuwa unakishughulikia kitu kulingana na uhalisia na si kujidanganya hata wewe mwenyewe.

 Tokea mwanzo mimi nimesema wazi, shughuli ya ubingwa si yetu sisi. Sasa kwa ajili ya morali na kujiweka vizuri kwa ajili ya msimu ujao basi tuhakikishe tunashika nafasi ya pili ili msimu ujao tuanze mapema safari ya ubingwa.

Hatuwezi kuiondoa Simba kileleni, unaona hata tukishinda mechi moja iliyobaki tutakuwa na pointi 54, hapa itakuwa ni tofauti ya pointi zaidi ya 15 na mechi mkononi ni 10. Pointi 15 ni mechi 10, sasa anayekuzidi kwa idadi hiyo na ligi ipo ukingoni, anatakiwa kushinda mechi tano kati ya 10 alizobakiza achukue ubingwa na mwendo wake ni mzuri kuliko wako, kama ni msemakweli na unafuata weledi wa kazi hasa ya ukocha, lazima utakuwa mkweli.

Vizuri kila tunavyokwenda tunaona makosa, wapi turekebishe, nini tupunguze na kuongeza. Tunaona namna tunachotakiwa kufanya katika mipango ya muda mfupi, pia muda mrefu lakini suala la ubingwa kwa sasa waachie Simba wenyewe.

Nimeulizwa maswali mengi sana kuhusiana na kipi ninachotaka kukirekebisha katika kikosi changu ili kiwe imara kama ninavyoamini, yako mengi tu.
Nimefanya kikao na uongozi, wanajua ninachokitaka kwa ajili ya kuiona ile Yanga ambayo ninaitaka mimi. Lakini yapo yanabaki kuwa mambo ya ndani ya Yanga na mengine naweza nikayaeleza, mfano huo ubora nimeuona kutoka kwa baadhi ya timu kama Azam, Namungo na Simba na ninataka nini.

 Ninaamini tukikutana tena hapahapa Jumatatu, nitaeleza namna ambavyo Yanga inaweza kuwa bora kabisa na hili linawezekana, nafasi hiyo ipo. Tukutane keshokutwa.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI